January 12, 2018





Huku Rais wa Simba, Evans Aveva akiendelea kuugua mahabusu, Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iwaruhusu kwenda kumhoji, makamu wa rais wa timu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha kiasi cha dola 300,000 za Kimarekani.

Katika kesi ambayo iliitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama ya Kisutu, Victoria Nongwa, ambapo mshitakiwa namba moja, Evens Aveva hakuweza kutokea baada ya Askari wa Jeshi la Magereza kuiambia mahakama kuwa bado anaumwa hali iliyosababisha Kaburu kuwa peke yake.

Mbali na Aveva kushindwa kufika mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leornad Swai ameambia mahakama kuwa bado upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika lakini pia mpaka sasa wameshindwa kupata baadhi ya nyaraka walizoziomba kutoka kwenye ofisi nyingine za Aveva kwa kuwa bado imefungwa.

Swai alisema bado hawajakamilisha upelelezi wa kesi hiyo lakini pia hajafanikiwa kuzipata nyaraka nyingine kutoka kwa mtuhumiwa namba moja kwa kuwa ofisi yake imefungwa licha ya kuomba kwa muda mrefu. 

Mwendesha mashitaka huyo aliendelea kuiomba makahama iwaruhusu kwenda gerezani kumhoji kwa mara nyingine mshitakiwa namba mbili, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwa ajili ya uchunguzi wao ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama hiyo.
Hoja hizo zilikubaliwa na mawakili wa upande wa utetezi waliokuwa wakiongozwa na  Evodius Mtawala kabla ya Hakimu Nongwa kusogeza mbele kesi hiyo hadi Januari 25, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa tena. 



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic