Na Saleh Ally
KIUNGO wa Simba, Shiza Ramadhani Kichuya hakwenda kwenye benchi mara baada ya kufanyiwa mabadiliko na Kocha Inrambona Masoud Djuma wakati Simba ikiivaa URA ya Uganda katika mechi ya Kombe la Mapinduzi.
Kichuya alionyesha utovu wa nidhamu wakati akitoka, hakufurahia na hakutaka hata kumgusa Djuma aliyekuwa tayari kumpa mkono. Baadaye alionekana akizungumza na Msemaji wa Simba, Haji Manara na picha iliyosambaa ilisababisha watu wengi kumshambulia Manara pamoja na viongozi wengine wa Simba, kwamba Kichuya hakupaswa kubembelezwa kama ilivyoonekana Manara akifanya.
Baadaye Manara alijibu mtandaoni akiwalaumu waandishi kwa kushindwa kumhoji kwamba alikuwa akizungumza nini na Kichuya na badala yake wakasema alikuwa akimbembeleza.
Kawaida katika habari, picha huzungumza, lakini vizuri kupata uhakika kama alivyosema Manara kama sehemu ya weledi. Baadaye, Kocha Masoud naye alimtetea Kichuya akisema alimruhusu kwenda kukaa jukwaani yeye na kiungo Jonas Mkude na Mghana, Nicholas Gyan.
Ukirudi katika uhalisia, hilo la Manara na lile la Djuma haliwezi kufuta upuuzi ambao aliufanya kwa kuwa unaweza kuona watu hawaelewi jambo lakini ukasahau kama nilivyokueleza kwamba picha huzungumza au picha zina lugha zake.
Kichuya wakati akitoka, lugha ya mwili wake ilionyesha kilichokuwa kinatokea. Wakati akiwa jukwaani, bado lugha ya mwili kupitia picha ilionyesha tatizo kubwa, ndiyo maana hukuona lawama nyingi zikienda kwa Mkude na Gyan.
Inawezekana ni jambo zuri kuficha matatizo ya wanao ili uweze kuyazungumza kifamilia na kuwakanya kwamba walichokuwa wanakifanya si sahihi. Kuwa mkweli na kuwa tayari kukosolewa kwa nia ya kurekebisha, linaweza kuwa jambo zuri zaidi kuliko kung’ang’ania jambo ambalo si sahihi ukipigania kulionyesha lilikuwa jema na bila shida.
Alichofanya Kichuya ni kitu cha hovyo na huenda hii inaweza ikawa picha inayothibitisha kwamba maendeleo ya wachezaji wengi wa Tanzania yataishia hapa nyumbani tena kwa muda tu kwa kuwa kuna viongozi wataweza kuwabeba kwa kuonyesha mapungufu wanayofanya, ni jambo la kawaida kabisa.
Jiulize, kwa nini Kichuya afichiwe matatizo yake? Je, kwa kuwa ni kipenzi cha viongozi? Maana hata mashabiki ambao wanampenda kwa kuwa amekuwa akiifunga Yanga, hata wao walikerwa na kuonyesha wazi hawajafurahia ujinga alioufanya. Ndiyo maana baadhi walimzomea pale bandarini baada ya Simba kurejea Dar es Salaam ikitokea Zanzibar.
Viongozi wa Simba wako wapi, wanafanya nini kwa utovu wa nidhamu uliojitokeza hadharani? Mchezaji akibadilishwa anakwenda jukwaani, au anakwenda kukaa kwenye benchi na kuangalia makosa ya kile alichokosea hadi kocha akambadilisha wakati mwenzake anarekebisha?
Djuma kasema aliona wamechoka, hii ni propaganda tupu kwa kuwa baada ya mechi, Kichuya na wenzake wangekuwa na muda wa kufanyiwa masaji hata zaidi ya siku nzima na pale zilibaki si zaidi ya saa moja kuwa eneo la pale uwanjani!
Angalia hata walipofika bandarini, huenda lilikuwa jambo zuri kuingia kwenye basi na baada ya hapo, angalau waende hadi klabuni halafu watawanyike. Wachezaji wanatoka kwenye basi kwenda kurukia bodaboda, wengine wanakatiza mitaa na linaonekana ni jambo la kawaida kwa klabu kubwa kama Simba.
Suala kama hili tumelikemea sana kwa timu kadhaa ikiwemo Taifa Stars, lakini linaonekana ni kawaida, viongozi Simba hawana shida nalo na wanaweza kutumia nguvu kubwa kulitetea wakiamini ni sahihi sana.
Waungwana, si sahihi hata kidogo kutaka kuwaridhisha wachezaji waliofanya makosa mbele ya hadhira, mkalazimisha kuonyesha hakukuwa na tatizo. Hata mnaowatetea wanajua wamekosea, mnapowatetea mnazidi kuonyesha viongozi ni waoga na mnawahofia wachezaji wenu jambo ambalo ni kichekesho cha mdomo wa juu pekee.
Waambieni ukweli, wakumbusheni Simba ni kubwa kuliko wao, wasisitizeni kwamba wajue wamebeba dhamana ya mioyo ya watu wengi na mwisho, wajue bila ya nidhamu wataendelea kupiga mbizi Ligi Kuu Bara na baada ya hapo, itakuwa ni kurudi ‘rivasi’.
Mimi niliamini Kichuya anakua sasa, sikuwa ninajua kama ana kitu kikubwa cha kuweza kuonyesha kiburi hadharani na tusisikie kwamba aliomba radhi au kujutia upuuzi wake. Tusisikie Simba imeamua kukemea, kuonya na kuweka msisitizo.
Huenda Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amekuwa mkweli baada ya kukemea hilo. Simba lazima wajue wanaficha maradhi na kuna siku yatawaumbua na alichofanya Kichuya ndiyo mwanzo wenyewe.
Utovu wa nidhamu ndani ya Simba umekuwa ukizungumzwa, hata baada ya kuondolewa kwa Kocha Joseph Omog, wachezaji ilionekana ni sehemu ya tatizo. Leo siku chache akiwepo Djuma inaonekana kuna shida bado, lakini hata kama ya Omog akiwepo Jackson Mayanga bado kulikuwa kuna matatizo yanayofanana.
Kama Simba wataendelea kulea maradhi kwa kuwalea wachezaji wao “wapenzi”. Mwisho pamoja na kusajili vizuri, kulipa vizuri, kulipa kwa wakati wataanguka na mashabiki na wanachama watalia na wao viongozi.
Kiongozi bora huwa imara kusimamia nidhamu ambayo ikikosekana, jibu huwa ni kufeli. Viongozi, kama kweli mna nia njema, simamieni nidhamu, wasio na nidhamu waadhibiwe au kudhibitiwa na mwisho, masuala ya kuficha matatizo, yawe na mwisho.
Itafikia wakati tutaanza kutafuta kilichojificha kwa kuwa Simba si klabu ya viongozi, ni klabu ya wanachama wananchi wa Tanzania, hivyo Watanzania wana haki nayo na wana haki ya kujua, kukosoa na kukemea. Mlichopewa viongozi ni dhamana, basi itumieni vizuri kuendesha jahazi na muonyeshe tofauti ya uongozi na ushabiki.
0 COMMENTS:
Post a Comment