MUNICH, Ujerumani
BAYEN Munich ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Kama haitapoteza michezo miwili ijayo basi timu hiyo itatangazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo ikiwa ni mara yao ya sita mfululizo wanautwaa.
Lakini wakati vijana hao wanatafuta ubingwa huo, pia wanafanya kazi kubwa ya kutafuta kocha mbadala wa kuifundisha timu hiyo.
Kila kocha anataka kwenda kuifundisha Bayern Munich kwa kuwa kwa mashabiki wanaofuatilia ligi hiyo kupitia King’amuzi cha StarTimes wanafahamu ubora wa timu hiyo kwa miaka kadhaa sasa.
Tayari mabosi wa timu hiyo, wameshatangaza kuwa wanamtaka kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino kwa ajili ya kuchukua nafasi ya babu Jupp Heynckes, ambaye anaondoka kwenye timu hiyo baada ya msimu kumalizika.
Kocha huyo mzoefu alijiunga na Bayern katikati ya msimu ikiwa kwenye wakati mgumu wa kutwaa ubingwa msimu huu, lakini kuanzia alipoichukua timu hiyo amepoteza mchezo mmoja tu.
Hata hivyo, pamoja na kwamba Bayern walitaka kumpa mkataba mrefu lakini aligoma na kusema kuwa anataka kurejea mapumzikoni.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa timu hiyo, Karl-Heinz Rummenigge, Pochettino ndiye mbadala sahihi kwenye timu hiyo.
Pochettino ni kocha wa Tottenham Hortspur, lakini nguvu ya fedha na ushawishi wa kutwaa makombe vinaweza kumfanya kuwa na sifa kubwa zaidi kwenye ulimwengu wa soka, hivyo itakuwa rahisi kwake kujiunga na timu hiyo.
Taarifa zinasema kuwa kocha wa sasa wa Bayern, Heynckes, 72, ndiye aliyesema kuwa kocha huyo anaweza kuchukua mikoba yake na kufanya vizuri bila kuvuruga utamaduni wa timu hiyo.
"Nafahamu kuwa Bayern Munich wameshazungumza na Mauricio Pochettino na baada ya kumaliza kutwaa ubingwa atakuwa kocha wao," alisema mchambuzi wa Sky Sports, Dietmar Hamann ambaye ni mchezaji wa zamani wa Bayern.
Hata hivyo, mashabiki watapata wakati mgumu kumuona kocha huyo kwenye Bundesliga msimu ujao kwa kuwa ana mkataba na Spurs hadi mwaka 2021 na hivyo itakuwa lazima akubaliwe na mwenyekiti wa timu hiyo, Daniel Levy.
Levy amekuwa akivutiwa na utendaji kazi wa kocha huyo na anaamini kuwa ndiye pekee anayeweza kuisaidia timu yake kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu England kwa misimu ijayo.
Kwa sasa Spurs, inawania kumaliza kwenye nne bora kwa mara ya pili mfululizo jambo ambalo linaonekana kuwa mafanikio makubwa kwenye timu hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment