March 26, 2018





NA SALEH ALLY
ANAYEKAIMU nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao ndiye amekuwa gumzo zaidi ukiachana na Michael Wambura ambaye amefungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka.

Binafsi bado nataka kuona msisitizo na uwazi wa mambo, sitaki kujiingiza katika mkumbo wa kuishangilia TFF ilichofanya wala kuwa mtetezi wa Wambura kwa kufanya kampeni ambazo hazina msingi kwa lengo tu la kuamini ameonewa.

Kwanza lazima kujiridhisha, ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza, lazima TFF wawe wazi katika mambo yao kama kweli Wambura ana hatia, bila shaka wala uoga aadhibiwe na iwe adhabu kubwa kweli.

Lakini kama hatakuwa amefanya anachoadhibiwa nacho, basi apewe haki yake, haki itendeke kwa kuwa mara zote nimekuwa nikisisitiza suala la haki kwa kila mtu. Hatuwezi kuwa tunaoneana halafu tukasisitiza upendo na kupiga hatua kwenda katika maendeleo.

Hili tunawaachia TFF na Wambura mwenyewe, acheni kampeni za chinichini na kila kinachoendelea wekeni wazi wadau tuone ili siku ya mwisho tujue nini hasa kinaendelea na usahihi ni upi.

Wakati tunaendelea kusubiri suala la Wambura ambalo tumepewa taarifa Kamati ya Utendaji ya TFF, imemteua Athumani Nyamlani kukaimu umakamu rais wa shirikisho hilo, leo Metodo italenga kwa Kidao.

Kidao si mgeni miongoni mwa wapenda mpira akiwa mwanafunzi, bahati nzuri nikiwa katika timu ya Kanda ya Magharibi ya Michezo ya Shule za Sekondari (Ummiseta), niliwahi kucheza naye timu moja ya Magharibi tukiwa na Renatus Njohole.

Wenzangu walijiendeleza na soka na kufikia kucheza kiwango cha juu katika timu kubwa kama Simba na timu ya taifa. Hivyo kwa wapenda soka, Kidao ni mtu anayejulikana.

Nimemzungumzia katika kiwango cha uchezaji huenda ninamjua hivyo, lakini kuhusiana na uongozi sijui. Lakini nimekuwa nikisikia na ninajua kidogo kwamba ni mtu mwenye misimamo sana na wakati mwingine ni mgumu kubadilika.

Kitu kingine nje ya mpira kwa Kidao najua si mtu mwoga, anapenda kuamini anachotaka kufanya na ikifikia hivyo, basi atafanya hata kama atakuwa anawaudhi wengine, ili mradi anajua kitu hicho ni sahihi.

Wanaofanya kazi na Kidao, wanaweza kuwa watu wazuri kutufungulia tuone mambo zaidi kwa kuwa kwa kipindi sasa tokea ameanza kukaimu nafasi ya katibu mkuu, kumekuwa na maneno mengi kwamba hafai, ameingia kwa njia isiyo sahihi na kadhalika.

Suala la Kidao limekuwa likiendelea kuchukua sura nyingi, wako wanaosema wanaburuzwa, wako wanaosema anaifanya TFF kama yake na kadhalika. Lakini hakuna ambaye amewahi kuchanganua hoja zake na kuzifanya tuone ubaya wake.

Tanzania inatakiwa kuendelea kuwa nchi ya haki kama tulivyozoea, kama Kidao atakuwa anaonea watu na hakuna usawa au haki. Basi ni jambo zuri watu wawe wazi, ubaya au upungufu wake ujulikane na mara moja tumueleze bila ya kumuogopa.

Msisitizo wa kile ambacho nimekuwa nikisema, TFF si ya mtu, TFF ni ya Watanzania kwa kuwa ni chombo cha umma na utaona ile T katika TFF ni Tanzania ambayo inatujumuisha mimi na wewe ambao ndiyo wamiliki wa shirikisho hilo.

Lakini lazima tukubali lazima tuwe na watu imara, watenda haki na wanaofuata weledi kuliendesha shirikisho. Kidao ni kati ya waliopewa dhamana hiyo, hivyo lazima atende haki.

Wako hawajatendewa haki, wako wanaona anakosea, acheni majungu na unafiki, semeni wazi, tatizo lijulikane na kufanyiwa kazi.

Ila ikiwa hana tatizo, basi kuweni waungwana, muacheni afanye kazi yake kuleta maendeleo. Maana isije ikawa amebana mirija mliyokuwa mnaitumia kujipatia kipato, sasa mnatoa sababu nyiiiingii ambazo zinataka kuwasaidia kurudisha uhai wa mirija yenu. Haya, wekeni hadharani upungufu wake, ili aufanyie kazi fasta.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic