March 26, 2018


Licha ya kuanza mazoezi, kiungo mnyumbulifu wa Simba, Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda, ameibuka na kuweka bayana kwamba mashabiki wa timu hiyo wasimhesabie kuanza kucheza katika kikosi cha kwanza kwa sababu bado hajapona vizuri majeraha yake.

Niyonzima aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Yanga, hajawa na msimu mzuri baada ya kupata majeraha ambayo yamemuweka nje kwa zaidi ya miezi miwili ndani ya kikosi hicho kilichopo mikononi mwa Mfaransa, Pierre Lechantre.

Kiungo huyo hivi karibuni alianza mazoezi ya kujifua ufukweni kabla ya kuhamia katika gym ambapo alifanya sambamba na wachezaji kadhaa wa Yanga, wakiwemo Thaban Kamusoko na Amissi Tambwe ikiwa ni njia ya kujiimarisha.

Mnyarwanda huyo ambaye ni baba wa watoto mapacha, alisema kuwa licha ya kuendelea na mazoezi mbalimbali lakini hali yake bado haijatengemaa na kuanza kukitumikia kikosi hicho kwenye michezo yake 10 iliyobakia ya Ligi Kuu Bara.

“Unajua watu wanaongea sana bila ya kufahamu mtu yukoje, hawajui kwamba mtu anaweza kufanya mazoezi hata na timu lakini asiweze kucheza mechi, mimi bado sijapona ingawa nafanya mazoezi mara nyingi ikiwemo yale ya ufukweni na sasa gym na muda siyo mrefu naweza kuungana na wenzangu kwenye timu kwa ajili ya mazoezi.

“Ni ngumu kwa mtu ambaye ametoka majeruhi halafu akaanza kucheza tu kwenye mechi moja kwa moja kama ilivyo kwangu, siwezi kulazimisha kwamba nicheze wakati nikiwa mgonjwa kama watu ambavyo wamekuwa wakiongea kwenye mitandao kwa sababu tu wameona ninafanya mazoezi.

“Wanatakiwa kusubiri hadi nikipata ruhusa ya kuambiwa nicheze ndipo nitacheza lakini siyo kama mashabiki wengi ambavyo wao wamekuwa wakisema kwenye mitandao huko,” alisema Niyonzima.

Niyonzima ameanza mazoezi baada ya kuepuka kufanyiwa upasuaji ambao ungemweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.

Dalili sasa zinaonyesha kuwa ana uwezekano wa kucheza japo mechi chache msimu huu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic