March 9, 2018



NA SALEH ALLY
YANGA ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na watani wao wa jadi Simba wao wanaiwakilisha nchini yetu katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

 Hawa ndiyo wawakilishi wetu wawili ambao hatua za awali wamevuka vizuri tu lakini tayari wameanza kuliona joto la hatua ya kwanza kwa kuwa ugumu sasa uko wazi.

Yanga imekutana na Township Rollers ya Botswana na katika mechi ya kwanza tu wamejikuta wakilala nyumbani kwa mabao 2-1, jambo ambalo linaonekana kuwakatisha tamaa wengi.

Upande wa Simba, wao pia wakiwa nyumbani wameambulia sare ya mabao 2-2 licha ya mechi kwisha kwa tafrani kubwa la umeme kukatika huku mvua kubwa ikinyesha kupindukia.
Kilichopo sasa ni gumzo ya mechi hizo hasa baada ya Yanga kupoteza na siku iliyofuata, mashabiki wengi wa Yanga nao walitaka Simba wapoteze ili wafanane, haikuwa hivyo wakaambulia hiyo sare.

Simba walitangulia kufunga, Al Masry wakasawazisha kwa uzembe wa ulinzi wao na Simba wakasawazisha pia kwa mkwaju wa penalti baada ya beki kuunawa mpira kama ilivyokuwa katika bao la kwanza.

Kinachoendelea sasa na magumzo ya wapenda soka ni kutishana na kila upande ukijaribu kuutisha mwingine kwamba safari imefikia mwisho.

Kila upande unajaribu kuuonyesha mwingine utakavyoumia kutokana na kipigo utakachokipata ugenini kwa kuwa wenyeji wao ni timu bora kuliko wao.

Hatuna sababu ya kukataa kwa maana ya ubora wa maandalizi, Rollers hauwezi kuwalinganisha na Yanga kama ilivyo kwa Simba na Al Masry.

Lakini ukweli unasema kuelezana ukweli ni jambo zuri lakini hakuna kisichowezekana kulingana na maandalizi.
Kuendelea kuwatisha Yanga au Simba, wala si jambo la msingi sana tena linalenga kulazimisha kuzitoa timu zetu hata kabla ya mashindano.

Hakuna lisilowezekana, mfano Yanga kufunga mabao zaidi ya moja ikiwa ugenini. Hakika Rollers ni timu nzuri, hakuna sababu ya kumung’unya maneno. Lakini tukubali, Yanga inaweza kupambana nayo.

Kama ingekuwa bora kwa kiasi kikubwa, Yanga ingefungwa hata mabao saba. Tuliona Rollers wakitawala lakini tuonyeshe mapenzi kwa vyetu hata kama vina mapungufu.

Yanga, wale Waswana ni wazuri sana lakini tayari mmewasoma mchezo wao. Mnajua ubora wao uko wapi, upungufu wao ni upi, aina ya uchezaji na utamaduni wa mwendo wao.

Hali kadhalika upande wa Simba nao sasa hawawezi kuhadithiwa kuhusu Al Masry na Kocha Mfaransa, Pierre Lechantre atakuwa ameona na kuanza kuyafanyia kazi mapungufu na atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuonyesha mbinu zake dhidi ya Al Masry.

Lazima tuambieni ukweli kutokana na hali tunayoitegemea lakini tukumbuke kwamba hakuna timu isiyofungika. Simba na Yanga wana uwezo wa kushinda ugenini.

Masuala ya makocha sasa hapa ni muhumu kupanga mbinu sahihi kwa kuwa sote tunajua Al Masry na Rollers ni timu nzuri na upinzani wake utakuwa wa kiwango cha juu.

Kocha George Lwandamina  na Lechantre wana nafasi ya kuoyesha ubora katika hili kwa kuwa uchezaji wa Al Masry na Rollers hauwezi kuwa ule wa Dar es Salaam.
Kweli ni ngumu lakini inawezekana. Hiki ndicho wanapaswa kukijua wachezaji na makocha wao na tukubali, ubora unajengwa na ushindani sahihi ambao sasa Yanga na Simba wameufikia.

Wachezaji wa Yanga na Simba wasisikilize maneno ya vijiweni, waende Cairo na Gaborone wakijua kuna ugumu lakini wakipambana kiume kwa mipango sahihi, maelekezo ya makocha yafuatwe kwa uhakika na nia ya ushindi, basi itawezekana.

Kuamini haiwezekani basi hakuna haja ya kwenda, kuamini haiwezekani ni sawa na kwenda na kugoma kuingia uwanjani. Mimi naamini inawezekana lakini Yanga na Simba zijipange haswa.


1 COMMENTS:

  1. Ushauri mzuri wa Mhariri wetu. Natamani siku zote ungekuwa hivi , positive thinking.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic