April 13, 2018






NA SALEH ALLY
KOCHA George Lwandamina ameamua kuondoka na kurejea kwao Zambia akiwa ameandika barua ya kuachia ngazi kuinoa Yanga.

Lwandamina kaandika barua yake akieleza wazi uamuzi wake wa kuondoka Yanga huku akisisitiza kwamba anafurahi kupewa nafasi kubwa ya kuinoa Yanga kwa kuwatumikia pamoja na mashabiki wao.

Mwisho, Lwandamina raia wa Zambia amekumbusha kwamba taratibu za kuvunja mkataba ni anayevunja kulipa na yeye yuko tayari hilo lifanyike.

Hivyo amewataka Yanga, kumkata kile kinachotakiwa kukatwa kutokana na kile anachodai na baada ya makato hayo, basi atumiwe kile kilicho chake.

Huenda ni mara chache kuwa na ustaarabu wa namna hii na kwangu naendelea kumuona Lwandamina alikuwa tofauti sana na makocha wengi tunaowajua au niliowahi kuwajua.

Kama mwadanamu lazima atakuwa na upungufu wake katika maeneo fulani lakini nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba kwa maana ya ufundi na uvumilivu ni kati ya makocha wanaostahili sifa sana.

Uondokaji wake umeuona, kwanza pamoja na mambo mengi kwenda kwa kusuasua ndani ya kikosi cha Yanga, Lwandamina aliendelea kuwa mkimya na kupambana akiifanya kazi yake vizuri.

Angalia leo ameondoka, bado hakuna aliyejua kwamba anadai, hakuwa aliyekuwa anajua shida alizokuwa akipata kwa kuwa alionyesha yeye ni sawa na mzazi kwa kuongoza kundi lenye manung’uniko mengi, lakini mbele ya watu likaonekana liko tayari kupambana na lenye furaha ya kutaka ushindi na mafanikio.

Kwa yule anayetaka kuamini Lwandamina ni adui kwa kuwa ameondoka, basi ni mbinafsi kama ilivyo kwa mashabiki wengi wabinafsi ambao wanaamini watu wapo duniani kuwafurahisha wao tu.

Lwandamina ni mwanadamu, ana ndoto zake na ana familia anayotaka kuiendesha. Hakuja Tanzania kufurahisha watu tu wakati nafsi yake ikiwa haina amani au akiendelea kuwa na maumivu ya moyo tena bila sababu za msingi.

Onyesheni heshima kwa Lwandamina, kocha ambaye aliifundisha Yanga katika wakati mgumu na kuitengenezea sura ya matumaini huku ikiwa na muonekano wa maisha bora.
Yeye ndiye alikuwa ngao ya matatizo ya wachezaji na yale ya uongozi. Maana wachezaji walikuwa wanaudai uongozi fedha zao na uongozi una matatizo ya kutokuwa na fedha za kutoa kwa wakati mwafaka.

Lwandamina alibaki katikati, mtatuzi wa kero za wachezaji kwenda kwa viongozi na mtatuzi wa kero za viongozi kurejea kwa uongozi. Na mambo yakawa yanaendelea kusonga mbele kama vile kila kitu kipo sawa.

Si sahihi kumvurumishia matusi au maneno ya dharau na mara zote nimekuwa nikieleza wale wanaoona kutukana ndiyo kujenga hoja ni watu wasio na uwezo wa kujenga hoja sahihi kulingana na muda husika, hivyo kwa kuwa wanaona wanataka kushiriki mjadala na wanataka kulazimisha, basi uwezo wao unakuwa ni kutukana tu.

Kingine ambacho hakika Yanga wanapaswa kufanya ni kuonyesha wamepevuka kibusara. Wana michuano ya Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa wakiwa ndiyo wawakilishi pekee.

Badala ya kuanza kulumbana na kutengenezeana makundi, basi watumie muda wao kupambana na kuhakikisha Yanga inafanya vizuri katika hali ya utulivu.
Yanga wanaweza wakawa wanatengeneza bomu wenyewe katika kipindi ambacho kinahitaji utulivu na mipango sahihi ili kukaa katika njia sahihi na mwisho warejee katika sehemu sahihi.
Kuendelea kujenga uadui na kuwekeana visasi sasa, ni kutengeneza hofu ya baadaye.
Yanga mshukuruni Lwandamina na onyesheni mmepevuka kwa kuyanabiri mattaizo yenu badala ya kulaumiana.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic