April 16, 2018





NA SALEH ALLY
NINAAMINI utakuwa umewahi kusikia ule msemo maarufu kwamba amekula chumvi nyingi. Maana yake sasa ni mtu aliyeishi kwa muda mrefu au mwenye umri mkubwa.

Dhana ya msemo haiendi katika maana ya mapokezi ambayo huwa amekula chumvi nyingi, haraka anayepokea hufikiri mhusika, amebwia au kumeza chumvi nyingi na huenda atakuwa katika wakati mgumu au inawezekana ni mtu wa kumshangaa, kwa nini ale chumvi nyingi.

Kula chumvi nyingi, ni kuishi kwingi ambako ndiyo kuona mengi. Kila unapoona mengi basi lazima utajifunza mengi ingawa uwezo wa kujifunza unatokana na mhusika, inawezekana akawa kaishi muda mrefu asijifunze mengi sana kama aliyeishi muda mfupi au akajifunza lakini asiwe na uwezo wa kuyafanyia kazi kwa uhakika.

Inawezekana nimeanzia mbali kidogo, lakini ninapotaka kulenga ni kuhusiana na wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ambao ni Yanga, hawa ndiyo mabingwa wa Tanzania.

Yanga watakuwa kazini keshokutwa, kumalizia ngwe ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Wolaitta Dicha ya Ethiopia na kama watafuzu, basi watakuwa wameingia hatua ya makundi.

Hili ni jambo ambalo wadau wanaopenda michezo na wanaoipenda nchi yao ya Tanzania watakuwa wanalisubiria kwa hamu kubwa hasa kuiona Yanga ikifuzu na kuingia katika hatua ya makundi.

Ikifuzu Yanga, sidhani kama itakuwa ni faida ya furaha pekee au faida kwa mashabiki wa Yanga, badala yake ni kwa wapenda mpira wa Tanzania lakini hata Serikali ya Tanzania pia.

Kama Yanga itafuzu, timu itakazopangiwa nazo, zote zitakuja Tanzania na kila zitakapokuwa nchini zitaingiza fedha katika sehemu mbalimbali. Mfano hoteli, hazitajali mmiliki ni Yanga au Simba.

Lakini wachezaji na viongozi wao watanunua vitu mbalimbali, hawa pia hawatajali kuhusiana na anayewauzia ni Yanga au Simba. Hivyo ujio wa zile timu itakuwa ni biashara.

Mbali na hivyo, burudani itakuwa ni kubwa sana. Hata kwa wale ambao watakuwa wanataka Yanga ifungwe, watapata nafasi ya kuburudika na kwenda uwanjani kwa namna wanayotaka.

Kumbuka, runinga zitaingiza fedha kwa kurusha matangazo ya mechi hizo na zenyewe zitailipa Yanga na tunajua fedha ya Yanga wakilipwa wachezaji na benchi la ufundi nao hutoa kwa ajili ya kupata vitu mbalimbali ili kuendesha maisha yao na haijawahi kuwa wanaangalia anayewauzia ni Yanga au Simba.

Yanga watapewa mamilioni ya fedha kwa kufuzu, fedha hizo pia zitatumika hapa nyumbani na kitaalamu zitaingia katika mzunguko wa fedha wa hapa nyumbani. Bila ubishi, zitakuwa na faida kwa wananchi wa Tanzania bila ya kujali wanapenda mpira au la, ni Yanga au Simba.

Kuna kamsemo kameanzishwa hivi karibuni, binafsi ninauona ni msemo wa kijinga sana na wanaopenda kuutumia si watu wanaojitafakari na wakati mwingine huwa naamini ni wavivu kujifunza mambo mapya kwa kuwa dunia inakwenda kwa kasi kubwa sana na inawaacha.

Wanasema: “Haki ya shabiki ni kushangilia au kuzomea”, hii ni sawa na kumfanya kila shabiki anafanana na mwingine au kuamini mashabiki ni watu wajinga sana, hivyo wakiwa uwanjani wanaweza kushangilia na kuzomea tu.

Shabiki anaburudika, shabiki anajifunza, shabiki anasaidia, shabiki anaweza kugundua jambo kupitia kile anachokiona uwanjani na kudadavua vitu na baadaye akawa mtoa maoni anayeweza kusaidia mabadiliko. Kwenda kushangilia na kuzomea ni jambo moja tu, lijumuishe liite kushangilia, maana kila mmoja ana aina yake lakini ni sehemu ndogo sana ya maana ya kuwa shabiki.

Wewe si shabiki wa Yanga, lakini kumbuka Yanga inatokea Ethiopia, wachezaji wao watakuwa ugenini kuipigania klabu yao iliyobeba jina la nchi yetu, badilika na ondokana na hao wenye haki ya kuzomea na kushangilia tu, tafakari nje ya boksi. 

7 COMMENTS:

  1. Kaka huo ulioandika ni UCHUMI umetoka kidogo kwenye MPIRA umejitahidi kushawishi lakini kwangu mimi furaha yangu ni yanga kufungwa kuliko hizo pesa unazoongelea acha tu Yanga apambane na hali yake SIWEZI IOMBEA MAZURI YANGA.

    ReplyDelete
  2. Wacha propoganda zisizokuwa na maana.Waache wapenzi waamue wanachotaka kukifanya. Hata nchi zingine huwezi kukuta timu pinzani zinaombeana kheri.Wapenzi wa Liverpool hawawexi kushangilia maendeleo ya Man United na vice versa. Magazeti ya Katalonia huko Spain yalimlaani sana Michael Oliver kuipa penalti Real Madrid. Wapenzi wa Madrid walishangilia kutolewa kwa Barecelona. Umelivalia njuga sana.Wapenzi watafanya kile wanachotaka mradi hawavunji sheria. Dharau na kejeli haiwezi kubadili kitu chochote.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kwa upande wangu niko tofauti kidogo na ww kiongozi, ni kweli hata huko kwa wenzetu huwezi kuta timu pinzani zinaombeana mazuri, ila nadhani kwa sisi bado hatujafikia hatua walizopiga wenzetu..wako mbali sana, wale wameshinda kila kitu..hawana cha kupoteza, leo isipokuwa Barca basi itakuwa Madrid, leo hii isipokuwa Man u basi itakuwa man city, sisi bado tuko nyuma sana tunahitaji kusapotiana ili tuweze kupiga hatua, leo Yanga akishinda basi itakuwa nafasi nzuri kwa Simba na timu zingine kusogea, lakini hata kwenye inshu ya uchumi nayo itasaidia kwa kiasi flan. Sina hakika, ila nimeshasikia miaka ya nyuma huko Yanga alishawahi kuisiaida Simba isishuke daraja, kama ni kweli basi waliona impact ya Simba kushuka daraja, ingewaathiri hadi wao. Mimi ni shabiki wa Simba na najua Yanga wakipita wataongea sana ila kwa upande wangu bado nawaombea kila kheri

      Delete
    2. ni mawazo yake yaache yalivyo na wala si dhambi kufurahia yanga isifuzu.

      Delete
  3. Kama si timu yangu nawaombeaje wafanye vema? Adui mwombee njaa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic