April 25, 2018






Kuna ule msemo wa kwamba soka ni furaha ya masikini wengi na wenye vipaji vya soka wengi hutokea katika familia za wale wenye uwezo wa chini kifedha, imetokea mara nyingi hata barani Ulaya.

Linapozungumziwa suela hilo, wengi hudhani hii inatokea Afrika au Amerika Kusini tu kutokana na mabara hayo kuwa na watu wengi ambao ni masikini. Lakini wako wachezaji wanaotokea barani Ulaya na wakawa mifano.


 Mfano mkubwa zaidi ya mchezaji aliyetokea katika familia ya kimasikini na kuibuka kuwa nyota katika soka duniani ni Cristiano Ronaldo ambaye baba yake alikuwa mtunza bustani huko kwao Madeira nchini Ureno.


Lakini Luca Modric, yeye anaweza kuwa mfano mwingine mzuri zaidi hata kwa wachezaji wa nyumbani Tanzania au kwa maisha ya kawaida kwa watu wengine.



Maana unamuona akiwa tegemeo katika kikosi cha Real Madrid, timu tajiri na mabingwa mara nyingi zaidi wa Ulaya, unaweza kudhani alifika hapo kwa ulaini.


Modric anaaminika kuwa mmoja wa viungo wenye maumbo madogo lakini vipawa vya hali ya juu barani Ulaya. Kwa sasa kila anapokosekana katika kikosi cha MAdrid anazua hofu.


Historia inaonyesha robo ya maisha yake, Modric mwenye umri wa miaka 32 sasa, aliishi kama mkimbizi katika hoteli ambazo zilikuwa zimelipiwa na Umoja wa Mataifa (UN).


 Asili ya Modric kama ilivyo kwa Zlatan Ibrahimovic ni nchi ya Yugoslavia ambayo hata hivyo baadaye ilisambaratiba. Wakati wa vita mwaka 1991, Modric na familia yake walilazimika kukimbia nchi.


Baba yake mzazi aliungana na jeshi la Croatia kusaidia mapambano na Modric na babu yake walisafirishwa hadi katika kijiji cha Jesenice kwa msaada wa jeshi la waasi.
Kuanzia hapo, Modric alikuwa ni mkimbizi na yeye na familia yake waliendelea kuishi katika hoteli iitwayo Kolovare. Aliishi katika hoteli hiyo kwa miaka saba.


Baadaye familia yake na wakimbizi wengine walihamishiwa katika mji wa Zadar wakati huo vita ikiendelea, nako wakaendelea na maisha ya kuishi hotelini.


Wakiwa katika mji wa Zadar, mara kadhaa mabomu ya jeshi la serikali na wakati mwingine waasi, yalidondoka katika mji huo na kuua au kujeruhi watu kadhaa.


Furaha pelee ya watoto katika enero hilo ilikuwa ni kucheza mpira. Hakukuwa na viwanja, hivyo wakalazimika kuwa wanacheza soka katika maegesho ya magari.


 Mechi zilizokuwa zinachezwa kwenye maegesho ya hoteli zilimfanya Modric kuwa maarufu sana enero hilo kutokana na umahiri aliokuwa akiuonyesha.


Hata ulipofika muda wa kuanza shule, alipelekwa katika shule iliyokuwa inafundisha soka ingawa ada yake ilikuwa juu na baba yake mdogo mara kadhaa alilazimika kuongeza fedha.


 Bosi wa Akademi ya NK Zadar, Tomislav Basic ndiye alianza kuona umuhimu wa kipaji cha Modric ambaye alipata upinzani mkubwa sana na wale walioamini wanajua zaidi mpira kwa kuwa Modric alionekana kuwa na umbo dogo.


Kwa umbo lake, ilionekana ni vigumu kufanikiwa. Lakini Basic aliendelea kujivunia kipaji chake na kasi ya hali ya juu aliyonayo. Aliendelea kumtafutia timu bila ya kuchoka hadi alipofanikiwa Hajduk na hapo ndipo alipotengana na familia yake na kuhamia katika mji wa Dalmatia, safari ya soka ikaanza.


Akiwa na miaka 16, alifanikiwa kujiunga na timu kubwa ya Dinamo Zagreb ambayo ililazimika kuanza kumtoa mkopo katika timu kadhaa, mara nyingine akirejea, inamtoa tena ili kuhakikisha anakuwa katika kiwango sahihi kwao.


Baba yake alibaki kuwa mwanajeshi, familia yake ilitoka katika ukimbizi na kuishi maisha ya kawaida na ya chini kabisa lakini kupitia soka, Modric amekuwa mkombozi.


Modric amecheza Tottenham kuanzia 2008 hadi 2012 na alicheza kwa juhudi kuu na mara kadhaa alisisitiza suala la kutaka kuiona familia yake  na furaha na maisha tofauti na yale ya zamani.


Hofu yake kubwa aliitangaza ni kuhusiana na familia yake, has awatoto wake hakutaka kuwaona wanaishi maisha ambayo alipitia yeye. Hivyo hakuwa kukubali achoke uwanjani au kushindwa kwa kuwa aliamini kushinda ndiyo mafanikio yatakayomjengea yeye maisha bora pamoja na familia yake.

Modric alitaka asumbuke yeye zaidi kuliko kuona familia yake inasumbuka. Aliamini akisumbuka na kupata mafanilkio, basi ndiyo amani ya familia yake.


MWaka 2012 alijiunga na Madrid na tayari ameichezea mechi 163 na kufunga mabao tisa tu lakini ni tegemeo kutokana na mambo mawili makubwa, ulinzi na kuunganisha timu.

Angalia ndani ya miaka sita na ushee akiwa na Madrid, tena akiwa tegemeo, Modric ameshinda makombe zaidi ya 10. Hii ni kuanzia Hispania hadi Ulaya kwa ujumla.


Amefanikiwa kushinda La Liga mara moja, Copa del Rey mara moja, Super Cuo ya Hispania mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, Uefa Super Cup mara tatu na Kombe la dunia la Klabu mara tatu.


Madrid sasa imefanikiwa kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pamoja na kwamba imedorora katika La Liga lakini nafasi ya Modric kufika fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ipo.


Mafanikio hayo makubwa na Madrid, yamemfanya Modric ambaye alikuwa ni mkimbizi kuwa shujaa wa taifa lake. Ndiye mfano wa kuigwa kwa vijana wengi wanaotaka mafanikio.


Modric ndiye mfano kwa wale walio katika maisha magumu katika nchi hiyo kuamini kesho inawezekana na mambo yanaweza kubadilika.


Silaha kubwa inayotumika kupitia mfano wake ni “Upendo Uliozaliwa na Kujituma”. Kwa kuwa Modric alikuwa muoga kuona familia yake inapaa shida kama aliyoipata yeye na wazazi na ndugu zake, hivyo akaongeza juhudi kila siku hadi kufikia mafanikio makubwa na baadaye kuwa shujaa wa taifa.


Yeye binafsi amewahi kushinda tuzo kadhaa kama mwanasoka bora wa Ligi Kuu ya Bosnia (2003), Tuzo ya Mwaka ya Matumaini ya Croatia (2004), mwanasoka Bora wa Croatia mara tano mfululizo (2013, 2014, 2015, 2016 na 2017).


Pamoja na fedha nyingi alizonazo na kuwa mmoja wa wanamichezo tajiri zaidi nchini Croatia, Modric anasifika kwa kutokuwa na maringo wala kuishi maisha yenye mbwembwe, jambo linalomfanya aonekane ni sawa na mwalimu kwani kwa kuwa aliishi maisha ya shida akiwa mkimbizi, baada ya kufanikiwa, huenda angeishi kwa mbwembwe akionyesha alipofikia lakini yuko tofauti kabisa.


Huyu ni Luca Modric, usiache haya yapite hivihivi bila yaw ewe kujifunza jambo linaloweza kukusaidia katika maisha yako.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic