Achana na shilingi milioni 623 watakazozipata kwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, Yanga imepanga kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ili ivune Sh bilioni moja.
Katika michuano hiyo, timu itakayofanikiwa kufika hatua ya nusu fainali inajizolea kitita hicho cha fedha kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) haijalishi hata kama itafungwa.
Yanga imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi baada ya kuwaondoa wapinzani wao Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema ana matumaini makubwa ya kubeba Sh bilioni moja kutokana na uzoefu wanaoendelea kuupata katika michuano hiyo mikubwa.
Nsajigwa alisema anaamini wataingia kucheza hatua ya makundi kikosi chao kikiwa fiti kwani tayari baadhi ya majeruhi wao wameanza kupona na kurejea uwanjani, hivyo hadi kufikia kuanza watakuwa fiti.
“Hakuna kitakachotushinda sisi Yanga kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hii tena tumefanikiwa kufuzu makundi tukiwa na kikosi kidogo kutokana na wengi wa wachezaji kuwa majeruhi na kukosekana kabisa katika timu.
“Niwapongeze wachezaji wetu waliopambana tena tukiwa katika hali mbaya ya kiuchumi na kufanikiwa kufika hapa, kiukweli kila mmoja alipambana kwa nafasi yake, ni kitu cha kukipongeza kwao.
“Hivyo, tunakwenda katika hatua ya makundi tukiwa na nafasi za kusajili wachezaji wengine wapya watakaoichezea timu yetu kwa mujibu wa kanuni za Caf ambazo zinaruhusu kusajili wachezaji timu inapofika hatua hii ya makundi, ni matumaini yetu tutasajili wachezaji wengine watakaokiimarisha kikosi chetu ili tufikie malengo yetu,” alisema Nsajigwa.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment