May 28, 2018





NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na taarifa mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya ana mpango wa kuondoka Simba ndiyo maana amekuwa akisuasua kusaini mkataba mpya.

Kichuya ana mpango wa kwenda nje ya nchi, aachane na Simba sehemu ambayo amepata nafasi ya kujulikana baada ya kufanya vizuri hadi kufikia kuipa Simba ubingwa.


Hakuna ubishi kwa sasa, Kichuya sasa ni moyo wa Simba unapozungumzia kiungo hasa wakati wa kujenga mashambulizi.


Kama ingekuwa ni uamuzi sahihi, basi Simba wanapaswa kumbakiza Kichuya aendelee kuitumikia timu hiyo kwa msimu mwingine hasa ukizingatia wanacheza michuano ya kimataifa ambayo ni migumu zaidi kwa bara la Afrika upande wa klabu.


Maana yake, Simba wanamhitaji zaidi Kichuya kuliko anavyowahitaji yeye kwa kuwa kwa sasa angependa kujiendeleza.


 Ambacho Simba wamejijengea sifa nzuri kwamba wamekuwa ni watu wenye uwezo wa kukubali kuwapa nafasi wachezaji wao inapotokea wamepata sehemu wanatakiwa kucheza na hasa nje ya Tanzania.

Maana yake, Kichuya atakwenda na kwa kuwa hana mkataba na Simba safari hii yeye anakuwa ni mwenye uamuzi wa mwisho kwa vile hana masharti yanayoweza kumbana.

Tukubali Kichuya ni mwanadamu, wakati anatokea Mtibwa Sugar kujiunga na Simba lazima alikuwa na ndoto zake za kufika mbali. Haitakuwa rahisi kuamini alitaka kuishia Simba na safari yake ya soka iwe imefikia tamati.

Kwa wachezaji wengi wa kizazi cha sasa, tofauti na wale wa kuanzia miaka ya 1970 na 1980 wao Simba au Yanga ilitosha sana. Hawa wa kizazi cha sasa, wanataka kucheza nje ya Tanzania na Ulaya ndiyo dili.


Taarifa zinaeleza Kichuya anajipanga kwenda TP Mazembe. Hizi zimekuwa taarifa zinazotokea hapa na kule, upande huu na ule lakini hazijathibitishwa. Katika mpira au michezo ni kawaida taarifa kusambaa kabla ya ukweli kujulikana.



Kama kweli Kichuya anataka kwenda TP Mazembe, kwangu naona kama si sawa kwa kuwa kwa uchezaji wake wa ligi kama ile ya DRC inayotaka nguvu nyingi na kugongana kwa mara kwa mara huenda kutakuwa na ugumu kwake.

Lazima ajue kwa TP Mazembe haishiriki michuano ya kimataifa pekee, haisajili mchezaji kwa ajili ya michuano hiyo pekee. Hivyo lazima itashiriki ligi ya ndani ambayo ina ugumu wa juu sana.


Kichuya ana umbo dogo sana, hana nguvu ya kuvumilia mikiki ya mfano wa ligi hiyo. Inawezekana akawa na nafasi ndogo sana ya kutamba.


Kucheza Mazembe kama historia, yaani jambo lililowahi kutokea inawezekana. Lakini suala la kupata mafanikio DR Congo kwake linaweza kuwa gumu.


Inawezekana si DR Congo, ikawa ni sehemu nyingine lakini bado anatakiwa kuwa makini na kuangalia. Wakati anaondoka Simba anakwenda wapi, timu ipi na ligi ya aina gani na ikiwezekana kujua mapema mambo kadhaa kama uchezaji wa timu yake, akifika atachuana namba na nani na kadhalika.


Wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa wakienda katika timu, ilimradi wanasajiliwa na kupewa maslahi huenda ni mazuri zaidi ya timu wanayotoka.

Wachezaji wanaocheza katika ligi zilizoendelea huangalia mambo mengi sana ya msingi kabla ya kujiunga na timu mpya au inayomuwania hata kama itakuwa imetoa dau kubwa sana.


Utachuana na nani katika namba, utakwenda kucheza katika ligi ya aina gani, timu yako ina uchezaji wa aina gani na kadhalika.



Kichuya anaweza kwenda kucheza nje ya Tanzania na huu ndiyo wakati mwafaka kwake. Lakini lazima aangalie mambo ya msingi kabla ya kuanza safari yake hiyo maana wakati mwingine kuingia kichwakichwa, si sahihi.



6 COMMENTS:

  1. Sioni tatizo kama kichuya akisaini simba mkataba ambao hauta mzuia kama atapata tim ya kucheza nnje ya nnchi aache kushikwa masikio unaweza kwenda mambo ya kawa siomazuri unaludi kwenye club yako hakuna atakaye kataa kumpokea.kuliko kuondoka kwakiburi mfano kesi,singano,gadiel,domayo,hao wanapo taka kurudi kwenye vilabu walivyoondoka kwa mbwembwe hawawezi kuludi.nahata wakiludi hawata pata furaha club uni.

    ReplyDelete
  2. Maoni mazuri Brother Saleih ila nataka kutofautiana na wewe tena sana unaposema SIMBA inamuhitaji Kichuya zaidi kuliko anavyoihitaji yeye. Hapana kabisa isipokuwa Kichuya kwa sasa anaihitaji Simba tena sana kuliko Simba inavyomuhitaji Kichuya . Na sababu ni hizi mtu kuziafiki au kutoziafiki ni hiari yake.
    (1) Umezungumzia kuhusiana na umbo la kichuya kuwa dogo labda atateseka kule Congo kama Ramos alivyonyanyasa Mohamedi Slah kutokana na wakongo kuwa wapo vizuri kimwili. Kwangu mimi hiyo sio hoja ya msingi ya kumzuia kichuya kwenda Mazembe kwani wakongo walikuja hapa Bongo na wakali wao wa ndani na wa nje na kichuya hakuonesha dalili yeyote ya udhaifu wa shibe juu ya wakongo. Point yangu ni subira inaoambatana na malengo siku zote hukusanya baraka. Ulimsikia kapombe?Anafuraha baada ya timu kadhaa za nje kuvutiwa nae lakini kama analalamika hivi ili apatae muda zaidi pale SIMBA wa kujijenga zaidi. Kapombe ni kijana anaejilewa hivi sasa na ni mfano kwa vijana wengine.
    SIMBA kwa mara nyengine itashirki mashindano ya kimataifa kwa wenzetu ulaya mchezaji hata kama alikuwa na malengo ya kuhama timu lakini timu inapopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa hubadilisha mipango na aliekuwa kwenye timu isiokuwa na nafasi ya kushiriki mashindano hayo hufukuzia kusajiliwa na timu zilizomo kwenye mashindano. Kichuya anaweza kwenda kukomazwa Tp mazembe lakini ingekuwa busara kubakia SIMBA pengine japo kwa mwaka mmoja zaidi au dili la uhakika litakapokuja Kujijenga zaidi hasa kifiziko yaani kimwili na hata kimbinu zaidi za mpira.Sio kichuya tu peke yake vijana wetu wanatakiwa kuekeza zaidi katika afya zao. Kwa wenzetu bajeti ya mchezaji katika kuutengeneza mwili ili kumpa mchezaji huduma sahihi anayoihitaji uwanjani inaweza ikakosti nusu ya mshahara wake hasa kwa wale wachezaji wanaochipukia wanaojiandaa kwenda sokoni ambapo mara nyingi mwili imara ni moja ya kigezo kikubwa cha kutupiwa jicho.
    (2) Tp Mazembe inautamaduni wa kulazimisha mikataba ya miaka mingi. Mara nyingi huanzia miaka miatano au minne. Sasa kwa kweli umri kwa mchezaji wa mpira ni pesa.Inaweza ikatokezea nafasi ya kusonga mbele zaidi kwenye maslahi zaidi lakini mkataba ukawa umekubana. Na hasa mchezaji anapoweka malengo ya kupita Tp mazembe kama daraja la kuondokea. Wakati hali kama hiyo kama dili la kweli limekuja SIMBA utasepa tu. Simba kihistoria walishawauza wachezaji wao mahiri kwa mali kauli bila hata senti moja ilimradi wachezaji wao watimize ndoto zao na watu wakawacheka sana,umri mdogo lakini miguu ilitokomaa kisoka ni big deal ulaya.
    (3) SIMBA kwa sasa kiuongozi wapo vizuri kitu ambacho kitaendeleza hali ya utulivu wa kiuchumi klabuni hapo kitu kinachoashiria ushiriki mzuri na wenye ushindani mwakani katika mashindano watakaoshiriki hasa ya kimataifa kitu ambacho kitawatangaza wachezaji wake zaidi. Na Sio kama nataka kuipamba Simba lakini kiuhalisia mchzaji yeyote wa tz hata wa nchi majirani zetu atakaebahatika kuitumikia Simba msimu ujao atakuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye bahati ya kutafuta mafanikio zaidi katika maisha yao soka.

    ReplyDelete
  3. Wote nimewapenda sana kwa ajili ya mchango wenu. Kikubwa hapa ni ushauri ambao kwa mawazo yangu waangalie mbele, kusajili Simba hakutamfunga Kichuya, mbona akina Kapombe, Banda, Samatta, Okwi mwenyewe pamoja na kuwa na mikataba walipelekwa nchi za nje kwa mikopo au mali kauli hadi kuzipata fedha hizo wengine wameingia matatani kwa sasa.
    Ni wazo zuri kwa Kichuya kutafuta timu nyingine kwa sasa hasa nchi za nje, ila ni bora zaidi kuwa na mkataba ambao utampa maslahi bora sana kwake na familia yake. Kuondoka kwa baraka kunaweza kuleta mafanikio makubwa kuliko kama walivyofanya wengine akina Singano, Amis Tambwe,Ibrahim Ajib, Kelvin Yondani, Juma Abdul, Hassan Kessy kwa mifano tu na kujikuta mafanikio yakiwa kidogo sana, na hawataweza kurudi tena Simba "Wekundu wa Msimbazi".

    Protas-Iringa

    ReplyDelete
  4. Ujumbe umewafikia...atafakari..asijiingize kichwa kichwa.

    ReplyDelete
  5. Asifikiri kiingia ndani ya shimo refu pia baada ya kutoyapata aliyotegemea, afikiri namna ya kujitoa. Asisahau usemi, tamaa mbeke mauti nyuma. Wapo wanawake waliowakataa waume zao kwakutamani maisha bora zaidi kwa mwanamme mwengine na upo usemi, kama hunijui, jaribu mwengine Ukitaka mengi utakosa yote.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic