May 29, 2018




Kwa mara nyingine tena michuano ya SportPesa Super Cup inarejea kwa kishindo ambapo safari hii mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa yatafanyika nchini Kenya kuanzia Juni 3-10.


Mashindano hayo yalianza rasmi mwaka jana ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji ikishirikisha vilabu nane kutoka Kenya na Tanzania.


Katika kuleta msisimko wa soka nchini, timu za Tanzania zinazodhaminiwa na SportPesa za Simba, Yanga na Singida United sambamba na timu mwalikwa, Jangómbe Boys zilicheza dhidi ya Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars sambamba na timu mwalikwa, Tusker FC.

Hatimaye walikuwa ni Gor Mahia FC walioibuka mabingwa baada ya kumcharaza hasimu wao mkuu, AFC Leopards kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la Uhuru na kujikatia tiketi ya kucheza dhidi ya klabu ya Everton kutoka nchini Uingereza.


Tanzania Iliteleza
Kama kuna jambo liliacha alama ya maumivu kwenye mioyo ya wapenda soka nchini ni jinsi ambavyo wawakilishi wa Tanzania walishindwa kutamba kwenye michuano hiyo.

Ni Yanga pekee ambayo ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali lakini hata hivyo waliishiwa kutolewa kwa mikwaju ya penati na AFC Leopards huku Simba na Singida United wakiaga raundi ya kwanza baada ya kufungwa mikwaju ya penati huku Jang’ombe nao wakifungwa magoli 2-0 na Gor Mahia.

Ni kuteleza huko ndiko kulifanya timu za Tanzania kupoteza nafasi ya kucheza na Everton Uwanja wa Taifa Julai 13 mwaka jana na kuiacha Gor Mahia ikijizolea umaarufu duniani kote kupitia vituo mbalimbali vya televisheni duniani viilivyorusha mchezo huo ambao Wayne Rooney alivaa uzi wa Everton kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004.

Tulichukulia poa
Achilia mbali michuano kufanyika kwenye tarehe ambazo Ligi ya Tanzania ilikuwa imeisha huku wachezaji muhimu wakiwa wameenda makwao, lakini pia vilabu vyetu havikuipa uzito michuano hiyo  labda kwasababu ndio ilikuwa inaanza kama anavyosema mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi.

“Mwanzo tuliyachukulia haya mashindano kama kitu cha kawaida, tukaona kwamba tutaenda kucheza tu lakini baadae tukaja kuona umuhimu wake.

“Mimi naamini kama tungepata nafasi ya kucheza na Everton basi sasa hivi ingekuwa ni mazungumzo mengine kwani tungeweza kuweka historia ya kucheza dhidi ya Wayne Rooney”, alisisitiza Mahadhi.



Nafasi ya Pili
Waswahili wanasema kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ndio kosa na hivyo ndivyo timu za Tanzania zinaweza kusema kuelekea michuano ya SportPesa Super Cup mwaka huu.

Simba, Yanga, Singida United na JKU ni timu ambazo zitaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya mwaka huu itakayofanyika kwenye mji wa Nakuru nchini Kenya kuanzia Juni 3-10

Timu zetu za Tanzania zitapambana na wenzao wa Kenya ambao ni bingwa mtetezi, Gor Mahia FC, AFC Leopards, Kariobangi Sharks pamoja na Kakamega Homeboys 

Mbali na kujizolea dola 30,000 (Sawa na Zaidi ya Shilingi Milioni 68 za Kitanzania), bingwa wa michuano ya mwaka huu ataenda nchini Uingereza kucheza dhidi ya klabu ya Everton kwenye dimba la Goodison Park.

Hii ni nafasi pekee ya kurudisha heshima ya Tanzania kwenye michuano hii ambapo bila shaka mwaka huu hakutakuwa na kisingizio chochote kama anavyohitimisha kiungo wa klabu ya Yanga, Pius Buswita.

“Sasa hivi tumetilia mkazo kwenye haya mashindano na mimi kama mchezaji binafsi nahakikisha tunaenda kufanya vizuri ili tuweze kuitangaza timu yetu vyema na kupata nafasi ya kuonekana kimataifa.

Twenzetu Kenya!



1 COMMENTS:

  1. Kabisa yale masuala ya msimu uliopita ya kuwakilishwa na Gormahia kwenye ardhi yetu yalikuwa ni ya aibu.Inawezekana sisi kama watanzania tukaichukulia powa kwakuwa kila kitu sisi kwetu ni powa mwisho wa siku tunaonekana ni watu wa hovyo. Mara hii haya mashindano yatakuwa magumu zaidi hasa kutokana na uimara wa Gormahia umeongezeka zaidi halafu kwa kiasi fulani yale mashindano kama yamepanda thamani kwa hivyo timu zetu zinatakiwa kujipanga au wajiandae kwenda kutalii Kenya.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic