NA SALEH ALLY
KATI ya vitu vinavyotuangusha kwa kiasi kikubwa katika maisha yetu ya kila siku ni lile suala la kiongozi au mkubwa kushindwa kuwa na uamuzi sahihi kulingana na inavyotakiwa kuwa.
Ninamaanisha kuwa na uamuzi sahihi katika wakati mwafaka, hasa linapotokea jambo linalotakiwa kuchukuliwa hatua na kufanyiwa uamuzi mgumu ambao huenda usiwafurahishe wengi.
Viongozi wengi wa klabu hasa kubwa wamefeli katika suala la uamuzi ambao unakuwa ni kwa maslahi ya klabu zao. Mara nyingi wanachukua uamuzi wa kutaka kufurahisha watu.
Wako wamekuwa wakichukua uamuzi wa kutaka kulinda nafasi zao au kutaka kuonekana wazuri kwa lengo la kukwepa lawama. Mara kadhaa najiuliza, kwa nini watu wengi huwa na hofu na lawama?
Lawama inaumiza? Kama ndiyo namna gani na kama hapana, sasa kwa nini watu wanaihofia na inafikia kuwa na nguvu kuliko ukweli au usahihi unaotakiwa kufanyiwa kazi hasa!
Kocha mpya wa Yanga, Mwinyi Zahera huenda atabadilika baada ya kukaa kwa muda na baadhi ya watu ambao wangependa naye awe na tabia ya hofu, kutokuwa mkweli au kunyoosha maneno.
Lakini tayari ameonyesha ni mtu tofauti na kama ataachwa awe alivyo, basi atakuwa msaada ndani ya Yanga kwa kuwa tayari kaonyesha kunapokuwa na jambo sahihi, basi hana hofu kulifanyia kazi.
Juzi, Yanga walisafiri kikosi kimoja kwenda kuivaa Prisons ya Mbeya katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Wachezaji wengine walibaki jijini Dar es Salaam kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.
Uamuzi wa Zahera raia wa DR Congo ilikuwa ni kuigawa Yanga katika vikosi viwili na kimoja kiende Mbeya na kingine kibaki jijini Dar es Salaam, tayari kwa kuivaa Rayon maana Zahera anajua kwamba nafasi ya Yanga kuizuia Simba kuwa bingwa Tanzania Bara ni ndogo sana.
Hivyo moja kwa moja amewekeza sehemu ambayo anaamini yeye watakuwa na faida katika Kombe la Shirikisho ambako tayari wameanza kwa kuvuruga. Ujasiri huu ni ule bila kuogopa kwamba kuna ambao watakasirishwa na matokeo ya Yanga au watakasirishwa Simba kuwa bingwa.
Alichofanya Zahera ameangalia hali halisi kwani wangeweza kupambana kuichelewesha Simba kuwa bingwa, lakini hali halisi inaonyesha wanaweza kuichelewesha na si kuizuia.
Kutumia nguvu nyingi kuichelewesha wakati wanapoteza na wangeweza kuhifadhi nguvu hizo na kurudisha mapambano katika Kombe la Shirikisho ambako wameanza kuharibu, hii ndiyo sahihi na hesabu iliyo na uhakika.
Kinachotakiwa kwa sasa ni kwa uongozi wa Yanga, wanachama wa Yanga na mashabiki kumuunga mkono kocha huyo mgeni ili aweze kutimiza malengo yake.
Ukitaka kujua Zahera ni mkweli, anayeangalia usahihi wa malengo, wakati Yanga imerejea baada ya kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger ya Algeria, wala hakuuma maneno zaidi ya kusema alikuwa na kikosi chenye wachezaji wengi chipukizi na walikuwa na hofu ya mechi.
Kama hiyo haitoshi, Zahera alisema kwamba wachezaji wakongwe na waliokuwa tegemeo waligoma kwenda. Maneno yake ilikuwa ni siku chache baada ya uongozi na wachezaji wenyewe kuwa wanauma maneno tu, mara wana matatizo, mara hivi na vile. Tena lawama zikitupwa kwa kila aliyesema ukweli.
Uongozi uachane na kutanguliza lawama sasa kwa kila mtu, badala yake uangalie kipi ambacho kinaweza kuwa sahihi kutatua tatizo na kutimiza lengo la Zahera kuelekeza nguvu kwenye Kombe la Shirikisho.
0 COMMENTS:
Post a Comment