June 13, 2018




Na Saleh Ally
KOCHA Dylan Kerr raia wa Uingereza aliondoka nchini akionekana ameshindwa kabisa kupata mafanikio na Simba waliona hakuwa na mwelekeo mzuri.
Kerr aliinoa Simba ikiwa na wachezaji wengi vijana ingawa kulikuwa na mchanganyiko wa wakongwe na bado mambo hayakwenda vizuri.

Viongozi wengi walifafanua suala la kuondolewa kwa Kerr kama kocha ambaye hakuwa makini, alitengeneza urafiki na wachezaji kupindukia hali iliyopunguza umakini na kusababisha kikosi chao kuyumba.

Viongozi wengi wa Simba walionyesha kwamba Kerr alikwama au alifeli, wakaamua kumtupia virago. Lakini misimu miwili iliyopita, ameonyesha ni kocha wa aina nyingine kabisa akiwa na Gor Mahia ya Kenya na sasa anatakiwa nchini Afrika Kusini.

Moja ya klabu iliyovutiwa na Kerr ni Mpumalanga Black Ace ambayo inaamini ataisaidia. Jiulize, kuondoka Simba Kerr amekuwa nyota, kwanini?

Maana ameiwezesha Gor Mahia mara mbili kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Kenya, imebeba Kombe la Shirikisho, pia imebeba misimu miwili Kombe la SportPesa Super Cup na kuweza kubeba kitita cha fedha na pia sasa wanatarajia Julai mwakani kwenda nchini England kuwavaa Everton ya England.

Huyu ndiye yule Kerr aliyekuwa Simba? Nini alikikosea alipokuwa Simba na kipi amekipatia akiwa na Gor Mahia?



SALEHJEMBE imefanya mahojiano ya ana kwa ana na Kerr ambaye ameelekeza lawama zake nyingi kwa viongozi wa Simba huku akisisitiza suala la mabadiliko.

Kerr anasema anaweza kurejea siku moja Simba lakini sharti lake kubwa ni kuona viongozi kadhaa wa Simba wakiondolewa kwa kuwa anaona ni wakwamisha maendeleo.

Kerr anawaona viongozi hao akiwataja kwa majina ni tatizo kubwa na wataifanya Simba iendelee kubaki ilipo. Anaona viongozi hao wanafanya kazi kwa ajili yao na si klabu, ndiyo maana anasema kutakuwa na maendeleo Simba hadi wakiondoka.

Nimeona niufikishe ujumbe huu kama sehemu ya barua, maana maneno yake mengi niliyaona kama mtu anayeandika barua akitaka kufikisha ujumbe wake.

Kuingilia kazi ya kocha:
Kerr anaamini Simba ni timu kubwa na inahitaji kufanya mambo kitaalamu. Viongozi hawapaswi kuonekana wanajua zaidi ya kocha kwa kumtaka afanye wanavyotaka wao.
Anamtaja kiongozi mmoja ambaye sasa hafanyi kazi za Simba kwamba alikuwa tatizo kubwa kwa kuwa alipenda kufanya kila jambo na kuwa na uwezo wa mambo kuliko kocha.
“KIla mara anataka nifanye anavyotaka yeye, haiwezi kuwa sahihi. Hakuna maana ya kuwa na kocha wakati kuna kiongozi ana uwezo kikazi zaidi ya kocha, wabadilike,” anasema.

Kuchagua wachezaji:
Kerr anasisitiza, suala la kuchangia mchezaji gani acheze linabaki kuwa la kocha na si kiongozi.

“Kuna mchezaji usipomchezesha mechi mbili tatu, atakulaumu. Inawezekana aliwaaminisha viongozi wenzake ni mchezaji mzuri wakatoa fedha nyingi.
“Usipompanga wanakuona kama wewe ni tatizo, kumbe kweli hana uwezo. Ukishikilia msimamo wako, basi kuanzia hapo hamtaelewana na ugomvi unaanzia hapo,” anasema.

Ugomvi na wachezaji:
Kocha huyo mzaliwa wa mji wa Leeds nchini England anaamini wanadamu kupishana kwa mambo kadhaa au hata kauli ni jambo la kawaida.

Lakini anataka mambo yawe na mwisho, kama mlipishana basi mnaweza kuendelea na maisha kwa kurudisha uhusiano.

“Lakini viongozi wanagombana na wachezaji, baada ya hapo wananuniana. Niko Simba kuna kiongozi alikuja akitaka nisiwe namchezesha mchezaji fulani kwa kuwa alimuonyesha dharau. Nikamuambia ni suala la kiuongozi kama anaweza kuadhibiwa ni sawa. Lakini kabla, nitaendelea kumtumia kwa kuwa ana msaada na timu. Kuanzia hapo sikuelewana tena na kiongozi huyo. Kama bado wanafanya hivi, wabadilike.

Hawajui,wanajua:
Kerr anaweka msisitizo kwamba viongozi wa Simba si wataalamu wa mchezo wa soka ni viongozi na wanaweza kuwa na ushauri mzuri kutokana na uzoefu wao.
“Lakini hawawezi kujua zaidi ya kocha, wanaamini wanajua lakini hawajui. Wanalazimisha vitu visivyo sahihi na wakikataliwa wanadhani wamedharauliwa, jambo ambalo si sahihi.
“Hapa Kenya, nimefanikiwa kwa kuwa uongozi kuanzia kwa mwenyekitu wa klabu wamenipa nafasi ya kufanya kazi yangu, nikikosea basi wanaweza kuhoji lakini hawawezi kuhoji kabla sijakosea.


Kulazimisha usajili:
 Kocha huyo Mwingireza, analieleza suala la viongozi kuwa na wachezaji wao, linaweza kuwa jambo linalomchanganya sana kocha.

“Kiongozi anakulazimisha mchezaji fulani ni mzuri, anataka ajaribiwe. Ukifanya hivyo, utaona anakulazimisha kwamba ni mzuri na wanamhitaji. Mimi naona huyu mchezaji si sahihi, lakini hawanisikilizi na unakuwa unajiuliza, nani hasa ni kocha.

“Haya mambo yanaweza kuwa yanakwenda chinichini na watu hawajui. Lakini si viongozi wote wanaofanya hivi lakini ukweli ni lazima wabadilike ili kuifanya Simba kuwa na maendeleo.
“Kama kiongozi anaongoza Simba, basi ajue anatafuta maendeleo ya Simba na si maendeleo yake yeye binafsi na familia yake,” anasema.

Kerr amesisitiza, kama kocha aliondoka akiwa na uhusiano mzuri na wachezaji na wanachama ambao anaamini Simba ina kati ya wanachama na mashabiki bora kwa kuwa ni watu wenye subira.

“Wanachama na mashabiki wa Simba ni tofauti sana, wasikivu na wavumilivu. Hii ni nadra sana kuwapata watu wa namna hii duniani katika mchezo wa soka. Ndiyo maana nasisitiza, watendewe haki kwa viongozi kufanya kazi yao vizuri na kubadilika mara moja na kama haiwezekani, basi wengi waondolewe ili Simba ikimbie kwa mwendo sahihi kwenda kwenye maendeleo zaidi.”



11 COMMENTS:

  1. Hivi niulize, hayo yanayoandikwa ni ya upande mmoja. Inawezekana Kocha naye alikuwa na mapungufu yake kwani yeye Mungu asiwe na mapungufu? Je Viongozi wa Simba nao wakisema mabaya ya kocha huyo waliyoyaona mpaka kuachana naye, tutakuwa tunajenga au tunabomoa? Kerr anataka kiongozi Simba afukuzwe ndio arudi. Manji anasema viongozi wote Yanga wafukuzwe ndipo arudi Yanga. Staili gani ya kuendesha vilabu? Hivi kocha Omog akiombwa kurudi AZAM anaweza kusema kwanza afukuzwe Bakhresa ndipo anaweza kurudi? Viongozi wa Vilabu wanachaguliwa na wanachama wapo pale kutetea maslahi ya klabu. Sasa kama kuna tatizo kiongozi analifanya ni mapungufu yapelekwe kwenye vikao husika vijadiliwe na kutolea maamuzi, lakini si kutoa sharti la kuwang'oa viongozi kwa matakwa ya mtu binafsi,tusivuruge vilabu vyetu vya mpira.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nakubaliana na msimamo huo. Vilabu wenyewe ndio wenye kauli za mwisho sio kocha wala mtu binafsi aweke masharti hapa, sio sahihi.

      Delete
  2. Mwandishi ndio anamjaza upepo. Ni kocha wa kawaida sana.

    ReplyDelete
  3. Kwa hivyo kwa mtazamo wazi kabisa bila ya kocha kerry Simba haiwezi kupata mafanikio? Na kwa kigezo gani unaifananisha simba ya sasa kiungozi na wakati kerry akiwa kocha? Au kwa kuwa mzungu sasa kila analosema inakuwa mada ya kitaalam hata kama anachuki zake binafsi? Viongozi wa SIMBA sidhani kama wanamango nae isipokuwa kiherehere chake na hao wapambe wake anatakiwa kumovi forward na achane na Simba kwani kwsasa hawamuhitaji.

    ReplyDelete
  4. Aliyoyasema Kerr ni kweli tupu. Nimeshuhudia baadhi ya wazazi wasio na ujuzi wa kazi ya mwalimu ambaye ameisomea kazi hiyo kwa mafanikio na uwezo wa miaka mingi wakiingilia wazazi kazi za waalimu shuleni wakiwalaziimisha kuasomesha na kusahihisha na mitihani kwa njia wazitakazo wao na matokeo ni kuanguka viwango na kuwafanya wanafunzi kuwabeza walimu wao. Hilo kweli ni kosa ambalo pia huwaharibia makocha wenye ujuzi na kusabsbisha uharibifu wa viango.Hayo tusiyapinge na ni juu ya Mo na viongozi wa Simba mpya kuyajuwa hayo kwa makocha wajao ikiwa Kerr au mwengineo na kuwamurika wanaotaka uongozi kwa kujaza matumbo yao na tujue sasa Simba ina wenyewe na sio shamba la bibi kwani watatimuliwa kama paka wadokozi tuusikie mngurumo wa Simba wakiitikisa Africa

    ReplyDelete
  5. Ameonge aliyoyashuhudia lakini, kocha anaweza kwenda sehemu fulani akafanikiwa na kocha huyohuyo akaenda sehemu nyingine akafeli.

    ReplyDelete
  6. Huyo kiongozi anayependa kuingilia makocha mbona hatajwi jina? bila kumtaja si ugonjwa unaendelea kuwa sugu usiotibika?
    Anasema kiongozi huyo kwa sasa hafanyi shughuli za Simba...sasa na Kocha Linchtre ameondoka kwa kuhitilifiana na hawa viongozi walioko madaraka?maana Bw.Saleh Jembe nimesoma makala zako nyingi ambazo zina mkakanganyiko na nakala zako nyingi ni sawa na panya anayeuuma na kupuliza usisikie uchungu.Usiangalie upande mmoja wa shilingi tu.Tukubali mazingara ya ufundishaji soka ktk Tanzania ni magumu hasa viwanja.Unapofungulia TV Azam ili uone mechi inayochezwa pale Songea, njombe au shinyanga inasikitisha...viwanja vya ajabu vya ligi kuu.
    Miaka ya 1970 ukienda kuangalia mazoezi ktk viwanja lukuki vilivyokuwa pale bonde la jangwani hutaamini ambavyo hivi vya njombe havioni ndani kwa ubora.Basi kwa nini makocha kina Victor stansclaus, Naby Camara, Tambwe Leya waliweza kupata mafanikio ktk ufundishaji soka enzi hizo za miaka ya mwisho ya 60 na hadi miaka ya mwisho 70?

    ReplyDelete
  7. tufike mahala tukubaliene na ukweli ambao ni uongo. Hapo simba viongozi ni wafanya biashara kwa manufaa yao sio klabu. nimepitia hapo kam mkurugenzi nimeona kwa macho yangu sio kusikia. Tuko mbali sana maana wanalipwa nini au wanachama wameidhinisha mshahara upi kwa viongozi wao? wanaishi kivipi? wachezaji wanalipwa vipi pesa za usajili? mkurugenzi wa timu yuko wapi? hawataki kuulizwa maswali hasa kuhusu pesa. kwanini waingilie kocha?

    ReplyDelete
  8. kwa nini hawataki kunisikia hao viongozi? kweli katika historia ya simba mimi simo? msimamo wangu ndo umefanya waninyime kadi mpya wakisema nisubiri mchakato mpya ambao nina imani nitaongoza kundi la wanachama kutetea haki yao ya msingi kwa maana thamani ya simba sio TZS 40Billion

    ReplyDelete
  9. Sasa afadhali mmenena kuhusu Simba tu angalau ile Yanga viongozi wake waliokuwa hawaingili kazi za kocha inafanya vizuri sasa? SIMBA ni klabu ya mfano sasa mnatakiwa kushata ap.acheni ucoga wenu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic