Kipa wa zamani wa Yanga, Deogratius Munishi 'Dida’, ameweka wazi kuwa hana mpango wa kurejea kucheza tena nchini katika timu yoyote ya Ligi Kuu Bara ikiwemo Yanga kwa kuwa anataka kufika mbali zaidi katika upande wa soka la kulipwa.
Dida ambaye anacheza katika Klabu ya Chuo Kikuu cha Pretoria 'Tucks FC’ inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Afrika Kusini, amekuwa akihusishwa kurejea nchini kujiunga na timu yake hiyo ya zamani ambayo kwa sasa ipo kwenye wakati mgumu wa kiuchumi.
Kipa huyo ambaye yupo nchini katika mapumziko, amekuwa akihusishwa kurejea Yanga ili kuweza kuziba pengo la kipa Mcameroon, Youthe Rostand ambaye ameshindwa kuonyesha ubora uliotarajiwa.
Dida amefunguka kuwa hana mpango wa kurejea kucheza soka Bongo kwa kuwa mipango yake ni kuhakikisha anaendelea kucheza nje kwa kupata changamoto mpya.
"Hizo taarifa kwamba Yanga wanataka nirudi, bado sijazipata lakini mashabiki si ndiyo waliokuwa hawatutaki vipi leo watake turudi! Ila siwezi kushangaa kwa sababu maisha ya soka yapo hivyo, leo wanaweza kukuona hufai ila kesho wakakushangilia.
"Lakini niseme wazi kwa sasa sipo tayari kurejea nyumbani kucheza katika timu yoyote kwa sababu nataka niendelee kucheza nje zaidi ya hapa nilipo na siyo kurudi nilipotoka, hayo ndiyo malengo yangu kwa sasa na siyo vinginevyo,” alisema Dida.
SOURCE: CHAMPIONI
Sema hata ukirudi ujipange kufunga bila kunuwia. Swaumu endelevu bila nia ni ukiukwaji wa haki za binadamu๐๐๐๐
ReplyDelete