July 9, 2018


Na Saleh Ally
KOMBE la Dunia nchini Urusi kwa kiasi kikubwa limerudisha juu umaarufu wa michuano hiyo kutokana na yanayotokea.

Kwa wachambuzi au wale wanaopenda mpira kumekuwa na ugumu mkubwa kujaribu kubashiri kwa kuangalia timu gani itafanya vizuri zaidi ya timu nyingine.

Angalia wachezaji wengi maarufu wamemwagwa kama maji na wamekuwa wakishindana kurejea nyumbani badala ya kushindana kufanikiwa na kwenda juu kufikia fainali.

Ukianza na nyota wa Ujerumani ambao walikuwa mabingwa watetezi, mapema kabisa hatua ya makundi.

Argentina yenye Lionel Messi na Sergio Aguero ambao walizisaidia timu zao katika La Liga na Premier League kuwa bingwa. Wote wamefungashwa virago mapema.

Achana na wao, Cristiano Ronaldo ambaye alianza kwa kasi, safari imemkuta naye, yuko kwao anashuhudia katika runinga. Afrika ndiyo kama kawaida na nyota wengi akiwemo Mohamed Salah walishindwa kuonyesha cheche.

Kwa asilimia 80, timu nne zilizoingia nusu fainali ni zile ambazo hazikutegemewa kwa zaidi ya asilimia 90 kwamba zingefika hapo. Timu zilizoingia ni England, Ufaransa, Ubelgiji na Croatia.

Croatia na England hazikuwa katika timu zilizopewa hata kufika nusu fainali. Ubelgiji ilionekana ingeweza kufika na kwa mahesabu, timu iliyokuwa kati ya zile zilizokuwa zikipewa nafasi ya kuwa bingwa, imebaki ni Ufaransa pekee.

England pia, ni kati ya zile zilizoonekana kufika nusu fainali si kazi rahisi kwao. Hatua hiyo mara ya mwisho walifika mwaka 1990 katika michuano ya Italia, wakiwa wamewang’oa Cameroon katika robo fainali lakini wakashindwa kwenda fainali baada ya kukutana na mziki wa Wajerumani.

Kombe la Dunia mwaka huu limeongoza kwa ‘surprise’. Kwa kuwa matokeo yake mengi hayakutegemewa na inakuwa vigumu kujua mechi ipi kati ya ile ya Ufaransa dhidi ya Ubelgiji, kesho au England dhidi ya England, keshokutwa.

Mechi ambayo ina mvuto zaidi hasa kutokana na rekodi na mwendo ni Ufaransa dhidi ya Ubelgiji kwa kuwa ni timu zenye ufundi unaofanana zaidi.

Aina ya uchezaji wao na namna ambavyo timu zao zimekuwa zikibadilika kutokana na na timu na zinacheza timu ipi kwa wakati husika.

Kutotabirika mapema, lakini unaona pamoja na ubora wa Ufaransa, lakini Ubelgiji tayari wameongeza kwa kiasi kikubwa cha kujiamini kwa kuwa tayari wameing’oa timu kama Brazil, hawawezi kuwa na hofu na timu nyingine.

Angalia safari ya Ufaransa tokea makundi, walishinda mechi mbili wakatoa sare moja. Kwa ubelgiji, wao wakashinda zote tatu, maana yake imani ya ushindi bado iko juu zaidi, ingawa wakizubaa watakumbana na surprise itakayowafanya wasiamini.

Ufaransa lazima wanajua Ubelgiji ni wazuri lakini katika hali ya kawaida hawawezi kuwa na hofu.

Kiufundi, utaona kuwa ushambulizi kwa kila timu una kasi ya juu kuliko safu za ulinzi ambazo zina wachezaji wengi wakongwe.

Mtu kama Vincent Kompany itabidi afanya kazi ya ziada kumzuia mtu kama Kylian Mbappe na Antoine Griezmann kama ambavyo Samuel Umtiti na wenzke watakavyohangaika na akina Romelu Lukaku, Kevin De Bruyne, Eden Hazard na wenzake ambao mwendo wao ulionyesha ulivyowashinda Brazil waliokuwa na safu ya ulinzi imara.

Mwisho katika timu zote, kila timu ina wachezaji wanaoweza kubadili matokeo nje ya mfumo. Yaani kipaji au uwezo binafsi nje ya mifumo ya walimu, unaweza kubadili mambo kabisa.

Hakika ni mechi ambayo unatakiwa kutulia mapema kwenye kiti chako tayari kuiangalia. Ni mechi isiyo na mwenyewe na huenda mechi zote za nusu fainali zitakuwa hivyo.

Kawaida, timu zinapoingia nusu fainali, uwezo unakuwa hautofatiani sana lakini zinakuwa zimepita misukosuko mingi katika michuano hiyo tokea zilipoanza makundi, hivyo zinakuwa zimeimarika kiakili, kimipango na hali ya kisaikolojia hasa uaminifu na nia ya kufanya vizuri inayokuwa ni pumzi ya imani ya kuwezesha kufikia malengo.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV