July 9, 2018


NA SALEH ALLY
KATI yetu sisi hakuna anayejua kipaji cha kiungo wa zamani wa Simba, Haruna Moshi maarufu kama Boban.

Binafsi naweza kusema kipaji chake ilikuwa zawadi ya Watanzania kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Naamini kingemfaidisha yeye kwanza kwa kuwa ndiye aliyepewa.

Lakini Boban alikuwa na nafasi ya kuifanya Tanzania kufaidika kutokana na kipaji chake kuwa msaada kwa Watanzania wengine hasa kama angetuliza akili na kufanya vizuri.

Kila mtu anaweza kusema lake kuhusiana na Boban, najua hakuna anayeweza kunizuia kutoa maoni kutokana na ninavyoona na ninaweka msisitizo, kwamba Boban hakukiona kipaji chake, au amechelewa kukiona ndiyo maana leo unasikia habari za yeye kusajiliwa Yanga kama si jambo kubwa sana.

Moja ya magazeti yaliandika kuhusiana na meneja wake, Harry Chibakasa maarufu kama Harry Mzozo, akionyesha kutofurahia namna ambavyo Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera anavyotaka kumjaribu Boban.

Zahera ameweka msisitizo anataka kumuona Boban tena na tena. Mzozo amesema tayari alishamuona hivyo kutaka kumuona tena na tena wakati naye anamuamini anaona kama si sawa.Nafikiri Mzozo anatakiwa kuwa na subira kwa kuwa inaonyesha, Zahera ni kocha makini na angependa kujiridhisha kuhusiana na mchezaji ambaye anamsajili kwa ajili ya kujenga kikosi chake.

Hawezi kuwa kocha anayesajili kwa maneno au hadithi. Inawezekana kaona kitu na angependa kujiridhisha na hili jambo kwa kocha ambaye anataka kufanya jambo kwa ajili ya kikosi anachokifundisha.

Binafsi nimeshangazwa sana kuona Boban akitaka kurejea na kujiunga Yanga. Ninaamini kabisa ana uwezo lakini hata akifanya vizuri, hatakuwa na muda mrefu wa kuendelea kutamba, nitakueleza kwa nini.

Suala la kipaji katika soka ni kubwa sana, lakini haliwezi kuwa kubwa kuliko nidhamu. Kabisa, nidhamu ni muhimu ndiyo mchezaji mwenye kipaji cha kawaida anaweza kufanya vizuri kuliko mwenye kipaji cha juu kabisa kama atakuwa na nidhamu.Boban alipoteza muda mwingi, huenda aliamini muda uko palepale. Ninaamini sasa umri unamtupa mkono wakati hapa katikati alipoteza muda akicheza ndondo na kuona ni sahihi.

Katika mpira kuna ushabiki, wako ambao hushabikia wachezaji na kuona kila wanachofanya ni sahihi. Huenda walimshabikia Boban katika mambo kibao ikiwemo kuona ni sahihi alirejea nyumbani kwa vitimbi akiacha kucheza Sweden alikokuwa na nafasi ya kufika mbali.

Sasa wakubali, waliomuunga mkono wakati huo walimpoteza, walikuwa washauri wabovu na sasa mambo yake yanayumba na wao si wahusika tena na utaona wachache wamebaki kusumbuka kumrejesha kama anavyohangaika sasa Harry Mzozo. 

Kwa wale ambao wanachipukia na wenye nia ya kwenda mbali na kujiendeleza katika mchezo wa soka, Boban awe somo kwao kwamba kipaji si kila kitu.

Boban alikuwa na uwezo wa kucheza nje ya Sweden na ikiwezekana hata nchini England, lakini nafasi hiyo aliikosa kwa kuwa aliona hakuna kisichoshindikana kwake na ikishindikana pia siyo ishu pia.

Wangapi wanaona kuwa na vipaji ndiyo kila kitu? Wengi wao wamekwama mwishoni na wameishia kuhangaika mwishoni kwa kuwa sote tunajua, kazi ni kazi tu na kama unaitegemea, hauwezi kukwepa umuhimu wake. 

Kuamini ni jambo jema, lakini kumbukeni kujituma ni maumivu na yanahitaji uvumilivu na nia ya kutaka kutimiza pale unapotamani kufikia. Neno kutamani nalo ni muhimu sana kwa kuwa ni msukumo wa kukufanya usichoke au kukata tamaa ili kufikia unapotaka kwenda.

Bila ya juhudi, kukubali kukosolewa au kuelekezwa kwa usivyojua, hauwezi kwenda. Boban angekuwa makini, angekuwa na washauri wazuri asingekuwa mtu wa kusubiri aonwe na Zahera, badala yake kocha huyo Mkongo, angejivunia moja kwa moja kumpata Boban.

1 COMMENTS:

  1. Kabisa wabongo wakijazwa sifa za mashabiki wa Simba na Yanga wanaona washaweza. Vijana wetu bado ni walaini sana hata wa akili. Mfanao mzuri kama mashindano ya sports pesa ingekuwa ndio usaili wa kugombania kusajiliwa na tumu ya Uingereza hakuna kijana wetu angeliwezakumshawaishi kocha.Mpira sasa sio kitu cha mchezo mchezo ni kitu cha kulazimisha piga ua garagaza kwa kijana mwenye nia ya kweli ya kutaka kutoka. Kwa bahati vijana wengi wa kiafrika wana vipajai vya asili sawa na almasi aridhini lakini nchi zilizoendelea hata siziso endelea wale wazazi wanaofahamu umuhimu wa kuwa na mtoto professional footballer hutumia mamilioni ya pesa kuwandaa watoto wao kuja kuwa wanasoka wenye mafanikio. Nasaha tu kwa vijana wetu wasiakate tamaa na si lazima wote wakacheze ulaya lakini kitakwimu katika ukanda wa Afrika mashariki Tanzania ni nchi duni zaidi yenye wachezaji wanaofanya kazi nje pengine tumepitwa hata na somali na sudani kusini kwani hizi nchi pamoja na Comoro wana wachezaji wengi tu wnaongara ulaya sema wamekimbia na kuukana uraia wa nchi zao. Na lazima tujiulize tunakosea wapi?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV