July 22, 2018






Na Saleh Ally
FAMILIA ya kina Ng’olo Kante ni ile inayoishi kwa miongozo hasa ya Dini ya Kiislamu. Kumbuka nchi ya asili ya kiungo huyo ni Mali barani Afrika.


Mali ni kati ya nchi zenye Waislamu wengi zaidi. Kante ni kati ya waumini wa dini ya Kiislamu ambao husali swala tano na hata kama itakuwa ni Ligi Kuu England amekuwa akicheza huku amefunga.


Kante si mpenda makuu, dini yake inamuelekeza hivyo. Hata furaha yake imekuwa ni vigumu kuigundua kwa wengi, lakini kawaida hupenda kusikiliza mawaidha na vitu vinavyohusiana na Dini ya Kiislamu.


Suala la umbo lake limekuwa tatizo kubwa sana kwake, maana tangu akiwa mdogo amekuwa akicheza soka na watu wanaomzidi maumbo na mara nyingi wamemuona ni kichekesho.


Wakati wa mahojiano yake baada ya kusajiliwa na klabu yake kubwa ya kwanza mabayo ni Bolougne ya kwao Ufaransa, Kante alisema angeweza kukata tamaa kama asingekuwa anaamini sana kwa Mungu.


Kante anaamini angekata tamaa kwa kuwa angeamini Mwenyezi Mungu amekosea, lakini hakujaribu hata kidogo kufikiria hivyo kwa kuwa anajua Mungu huwa hakosei. Alichotaka ni kuendelea kufanya vitu vyake kwa juhudi.


Wakati fulani, Kante aliwahi kulaumiwa na ndugu zake kutokana na tabia yake ya ukimya hata pale alipoonewa. Mchezaji mmoja wa timu pinzani alimsukuma na kumkanyaga kifuani lakini mwamuzi hakuona naye aliumia sana.


Baada ya kupata nafuu, alisisitiza kuwa mchezaji huyo alipaswa kusamehewa kwa kuwa wachezaji huwa katika hali inayoweza kuwa si ya kibinadamu kwa kuwa huwaza zaidi kushinda kuliko kitu kingine.


Wakati akiwa Leicester City, Kante aliiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England huku akiwashangaza wengi katika namba sita aliyokuwa akicheza.


Umbo dogo lakini uwezo wake uliwachanganya hata viungo nyota wa England. Angalia, Kocha Antonie Conte wa Chelsea, alipotua tu Chelsea akitokea Juventus, alichofanya ni kumchukua Kante.


Conte anatambua, hakuna timu England iliyowahi kubeba ubingwa bila kuwa na ‘Hub’ ya uhakika. Alipoangalia, aliona ubingwa wa Leicester ulitokana na Kante ambaye alikuwa ‘Hub’, yaani sehemu inapozungukia timu.


Utaona, Roy Keane na Manchester United au Arsenal ya Patrick Vieira. Na Kante alipotua Chelsea, akabeba ubingwa wa England tena na kuwa amechukua ubingwa mara mbili.


Najua unakumbuka namna Kante, alikuwa akitumia gari ya Mini ambayo ilizua gumzo. Ilikuwa si kawaida kwa mchezaji anayelipwa mshahara wa pauni 120,000 (Sh milioni 355) kwa wiki, yaani pauni 480,000 (Sh bilioni 1.4) kwa mwezi.


Kumbuka ana magari matatu, thamani yake jumla ni takribani pauni milioni 1 (Sh bilioni 2.9). 


Lakini hata kuyaona imekuwa shida na waandishi wa England wamekuwa wakipata shida kumuona akiendesha. Mercedez Benz, Range Rover na Aston Martin lenye thamani ya dola milioni 1.5 (Sh bilioni 4.4).


Mwaka 2013, Kante alinunua jumba la kifahari katika mji aliozaliwa wa Paris. Thamani ya nyumba hiyo wakati huo ilikuwa dola milioni 1.36 (Sh bilioni 4), lakini aliiboresha zaidi na sasa thamani yake ni dola milioni 2 (Sh bilioni 6).


Kwa mwaka baada ya kukatwa kodi, inaelezwa anaingiza dola milioni 4 (zaidi ya Sh bilioni 12). Utajiri wake unafikia hadi dola milioni 15 (zaidi ya Sh bilioni 44.4).


Kumbuka Kante ambaye kitaalamu ni mhasibu wa ngazi ya diploma ni yatima baada ya kufiwa na wazazi wake wote na ndugu muhimu kwake amekuwa ni dada yake ambaye kutokana na maisha yake ya ukimya, hajawahi kuonekana.

Si mtu anayependa kujikweza au kuonyesha furaha yake kwa kila mtu. Ni mtu ambaye amekuwa hapendi kukera watu au wenzake. Mfano, angalia baada ya Ufaransa kubeba Kombe la Dunia, Kante alizua kituko cha ajabu.

Wakati wachezaji wakishangilia na Kombe la Dunia baada ya kuichapa Croatia kwa mabao 4-2 katika mechi ya fainali, Kante alionekana kama mgeni. Alikuwa kimya akiangalia mambo yanavyoendelea.


Kiungo mwenzake, Steven N’zonzi ndiye aliyeshituka na kumuuliza kama alishapata nafasi ya kupiga picha na kombe hilo, alimjibu hapana.


N’zonzi aliamua kuwakimbilia wenzake na kuwaomba wampe kombe apige nalo picha na wote walibaki wakimuangalia huku wakimfundisha aina ya mapozi ya kupiga nalo picha. Tena walilazimika kumfundisha aina ya mapozi mbalimbali ili aweze kufanya vema.


Kante amekuwa ni mchezaji wa wachezaji kwa kila timu aliyocheza. Wachezaji kadhaa wamewahi kupishana naye akiwa uwanjani kwa kuwa anakaba kwa nguvu sana, lakini baada ya hapo, ni mtu asiye na habari na maisha ya mtu mwingine.


Kocha Conte wakati wakiwa pamoja Chelsea, alikutana na mzozo na wachezaji wa timu hiyo baada ya kumtukana Kante. Baada ya kutukanwa, Kante alionekana kutofurahia, akawa amenyong’onyea sana na kila alipopiga mpira kama alivyotakiwa alikosea.


Jambo  hilo, lilionekana kuwakera wachezaji wa Chelsea ambao waliondoka katika ‘vituo’ vya mazoezi walivyopangiwa kusimama na Conte na kwenda kumpa pole Kante na kumpa moyo na pole.


Jambo hilo lilimshangaza Conte, kawaida haruhusu wachezaji kuondoka katika vituo hivyo bila ruhusa yake au utaratibu mzuri wa mazoezini. Kwake lilikuwa funzo kubwa na baadaye alimuomba radhi Kante mbele ya wachezaji wengine wote.


Kante ameshinda makombe ikiwemo tuzo ya mchezaji kijana wa Ligi Kuu England ambayo Waingereza wangependa iende kwa wachezaji kutoka kwao au washambulizi hatari na si viungo wakabaji, lakini kwa Kante ilifikia haina ujanja.


Baada ya mechi 31 tu na kikosi cha timu ya taifa ameshinda Kombe la Dunia, amecheza mechi 69 za Ligi Kuu England atika misimu mitatu, yaani 2015/16, 2016/17 na 2017/18 na amebeba ubingwa mara mbili.


Bado anaendelea kuishi maisha yasiyokuwa na mbwembwe. Huyu si mtu wa kawaida, ni mtu wa aina yake ambaye unaweza kuchukua somo kuu la maisha na kuona namna zawadi ya kipaji ulichonacho kutoka kwa Mungu unavyoweza kukitumia vizuri.


Hakuna ubishi kwamba Kante amekuwa na nidhamu ya hali ya juu. Huenda suala la kudharauliwa, kwake amelichukulia chanya na kuligeuza kama sehemu ya hamasa ya kuyafanya maisha yake kuwa bora na ya mapambano kwenda katika ushindi.

Angalia pia, hata alipofanikiwa, basi si mwenye maneno mengi, mbwembwe au anayejikweza. Huenda ana baraka kuu kwa bahati aliyonayo. Bado hata kama hutamfikia, unaweza kufanya mazuri kadhaa kwa kiwango fulani na kuingia katika mafanikio.

Mchezaji kama Kante unaona kabisa ana nafasi kubwa ya kufanikiwa na kufanya vizuri kwa muda mwingi zaidi kutokana na nidhamu yake, kuamini lakini kutokuwa na mambo mengi zaidi ya kazi yake.

Kuamini pia linaweza kuwa somo kwetu kwamba mtu ambaye anamwamini sahihi Mwenyezi Mungu, anaweza kuepuka mambo mengi ambayo yangeweza kuwa sehemu ya kumkwamisha.



1 COMMENTS:

  1. Daaah nahisi ubaridi moyoni mwangu hakika Mungu azidi kumpigania

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic