KOCHA COASTAL AFUNGUKA KUHUSU HATIMA YA ALI KIBA
Kocha wa Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda, ameweka wazi kuwa nyota wake mpya, Ally Salehe Kiba ‘Ali Kiba’ ana nafasi kubwa ya kucheza mechi zijazo licha ya kuwa na majukumu mengine ya kimuziki chini Canada kwa sasa.
Hadi sasa licha ya Coastal Union kucheza michezo yake miwili ya Ligi Kuu Bara, Kiba hajaonekana uwanjani kutokana na kubanwa na shughuli zake za kimuziki. Alikwenda Canada tangu wiki moja iliyopita na inaelezwa kuwa jana Jumapili alitoka huko kuelekea Afrika Kusini kumsalimia rafiki yake Ommy Dimpoz ambaye amelazwa kutokana na tatizo la koo, na hali yake ni tete.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Mgunda amesema amefanya mazungumzo ya kina na Kiba na ana nafasi kubwa ya kuwepo kwenye kikosi kitakachotumika katika mchezo ujao dhidi ya KMC Jumamosi hii, na kudai kuwa hana wasiwasi na uwezo wake kwa kuwa anafahamu ni mchezaji mwenye kiwango cha hali ya juu.
“Labda nikuambie tu sisi tumesajili wachezaji zaidi ya 30 akiwemo Ali Kiba, hivyo wote wana nafasi ya kucheza kwenye timu yetu.
“Na kuhusu Kiba, hapana shaka kuwa atacheza mechi zijazo kwa sababu nishafanya naye mazungumzo na ninajua ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa,” alisema Mgunda.
0 COMMENTS:
Post a Comment