August 21, 2018




Na Saleh Ally
HADITHI ya maisha ya mshambuliaji Romario raia wa Brazil wakati akiwa FC Barcelona ya Hispania iliwahi kuwashangaza watalaamu wengi wa mchezo wa soka.

Hali hiyo iliyotolewa na aliyekuwa kocha wake, Bobby Robson ilizua mjadala mkubwa na kuwachanganya watalaamu wa soka, hali ambayo mwisho iliacha makundi mawili, wanaoamini na wanaopinga.

Gumzo kubwa lilikuwa ni neno “Flexibility”, hali ya kuacha nafasi au kukubaliana na jambo kulingana na hali halisi. Makocha wangetaka kuwa na msimamo katika uendeshaji mambo kitaalamu. 

Lakini wakati mwingine inaonekana utaalamu unaweza kukaa kando na kuangalia hali halisi kwa lengo la utimizaji wa mambo.



Marehemu Robson alikuwa kocha wa kwanza Muingereza kufanya kazi Hispania na kufanya makubwa. Wakati huo msaidizi wake alikuwa kocha Jose Mourinho ambaye alianza kama mtafsiri wake wa lugha kwa kuwa ilikuwa kwake ni vigumu kuzungumza “Spanyola”.

Katika hadithi yake kuhusiana na Romario, alieleza alikuwa ndiye mchezaji mvivu kuliko wote wa kikosi chake. Mara nyingi alisingizia kujisikia vibaya, alitegea mazoezi ya mwanzoni mwa wiki ambayo huwa magumu na pia mazoezini alikuwa wa mwisho.

Mazoezi pekee aliyopenda ni soka, yaani kuuchezea mpira. Angeshiriki hata kama alikuwa amepangiwa kufanya hivyo kwa saa tatu. Robson aliamua kufanya kila kitu kwa kufanya utaratibu sahihi, kwamba anayefanya mazoezi kwa uhakika au vizuri ndiye mwenye nafasi ya kucheza.

Washambuliaji wenye juhudi za mazoezi kila alipowapanga, walishindwa. Alipompa nafasi mvivu Romario angalau dakika 20, alifunga mabao angalau mawili. Mwisho akaamua kuachana na sheria za shule na kuangalia hali halisi, hii ikaisaidia Barcelona kufanya vema kuliko ilivyotarajiwa.

Kwa walimu wanalazimika kufanya kazi ya ziada kuvunja utaratibu kama huo, ndiyo maana Robson alizua huo mjadala kwa kuwa kundi kubwa la makocha, lilimpinga likiamini anayepaswa kupewa nafasi ni yule anayefanya vema mazoezini.

Ninaamini hata Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems hawezi kukubali kuungana na falsafa ya Robson kwa kuwa atataka kuwa kama makocha wengi walivyofundishwa katika mafunzo yao kwamba mwenye nidhamu, mwenye juhudi na anayemsikiliza mwalimu anataka nini huku akiongeza yaliyo sahihi ndiye mwenye nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.



Kama ni hivyo, basi mapema kabisa nianze kuzungumza na kijana wa Kitanzania, Hassan Dilunga, kijana ninayeamini ana kipawa cha juu kabisa kati ya wachezaji wengi wa Kitanzania.

Dilunga ndiye mchezaji ‘aliyesahaulika’ na timu za nje ya Tanzania, nimekuwa nikiamini siku nyingi alipaswa kuwa angalau Afrika Kaskazini akifanya yake na kwa mafanikio makubwa.

Ameendelea kubaki Tanzania akihama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine na mara nyingi yuko Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, huenda anaamini inatosha.

Alipotokea Ruvu Shooting, alipokuwa Yanga na baadaye Mtibwa, nimekuwa nikimfuatilia na sifa yake kuu nimeelezwa ni uvivu, si mtu anayevutiwa na mazoezi ya nguvu kama wachezaji watatu wanne ninaowajua wa Tanzania wenye vipaji, lakini wangependa kucheza bila ya mazoezi magumu.

Kocha mmoja wa zamani wa Dilunga (nisingependa kumtaja), alinieleza namna alivyokuwa akivutiwa na Dilunga, aina ya uchezaji wake na kusisitiza, Tanzania inahitaji wachezaji wengi kama Dilunga lakini akaonyesha kusikitishwa na hali hiyo.

Siku nyingine nikazungumza na kiungo mmoja wa zamani wa Yanga aliyekuwa akicheza na Dilunga. Alinieleza mengi sana hasa masikitiko yake kwa Dilunga, kwamba analaumu kuonewa na kutopewa nafasi lakini ugumu anauweka yeye kutokana na uvivu wa mazoezi.

Bado naye, suala la uwezo wa Dilunga kisoka akasema unamshangaza huku akisema, wachezaji kama Dilunga Tanzania ni wachache sana.

Mwisho nimegundua, kila Dilunga anapojiunga na timu hasa msimu wa kwanza, anakuwa anaonyesha kiwango cha juu na bora kabisa. Pale anapozoea tu, anajisahau na kuanza kutaka kufanya anachotaka kwa kuwa tayari ni “Father”.



Nimeona wakati ameingia Simba, hakuna ubishi ukiachana na wageni mfano Meddy Kagere huyu Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda na Cletus Chama kutoka Zambia, hakuna mwenye mgeni katika kikosi cha Simba kajihakikishia namba isipokuwa Dilunga.

Kikosi cha Simba kupata namba ni lazima uwe kamili kweli kwa kuwa walio katika namba zao wako vizuri hasa. Lakini kwa uwezo alionao Dilunga, Aussems asingependa kumkosa.

Sasa kwa kuwa Dilunga ametoka Mtibwa Sugar akiwa mchezaji bora wa msimu, ameingia Simba kajihakikishia namba na umeona mechi ya juzi ya Ngao ya Jamii, pamoja na kucheza vizuri, ametoa pasi ya bao la kwanza alilofunga Kagere na yeye kufunga la pili, basi asirudi nyuma.

Nasema asirudi nyuma kwa kuwa mara nyingi ameanza vizuri, akizoea anaporomoka, akienda timu nyingine anaanza vizuri, akizoea yaleyale. Nafikiri sasa, iwe mwisho wa yaleyale.


Huu ndiyo wakati wa Dilunga kusonga bila kubadilika, kusonga bila kuchoka na kuachana na Dilunga wa zamani badala yake yule anayewaza kujifunza kupitia makosa likiwa ni jambo la kwanza lakini kukumbuka pia, umri nao si rafiki kwa kuwa muda unakwenda matiti.


Dilunga, anaweza lakini kabla ya kuweka akumbuke makosa yake ya nyuma na kusema basi ili awe tegemeo si Simba tu, badala yake kwa taifa la Tanzania katika timu ya taifa na mhamasishaji wa vijana kwa mazuri atakayokuwa akiyafanya.




2 COMMENTS:

  1. USHAURI MZURI KABISA

    ReplyDelete
  2. Ushauri nzuri kabisa na unaonesha jinsi gani Watanzania tunavyojaliana katika masuala ya kupiga hatua. Nnaimani Dilunga atafuata ushauri kwani anaekupenda ni yule akaekuambia ukweli juu ya madhaifu yako ili uwe bora zaidi. Na pale Simba kama Dilunga ataamua kuwa mgumu na kugangamala hasa basi kama Samata msimu wake mmoja tu anatoka.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic