August 14, 2018


Si bado unakumbuka kuwa hivi karibuni Simba ilitua kutokea Uturuki ilikokuwa imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya? Sasa taarifa nyingine ni kuwa msimu ujao timu hiyo iliyo chini ya mwekezaji bilionea kijana Mohammed Dewji ‘Mo’ itasafiri kisasa zaidi.

Tangu Simba iwe chini ya Mo haina shida za kifedha kama ambazo ilikuwa ikizipata misimu miwili iliyopita.

Unaambiwa kuwa msimu ujao unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 22, mwaka huu, safari nyingi za timu hiyo za kwenda mikoani kucheza mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na zile za Kombe la FA, usafiri utakaokuwa ukitumika zaidi ni wa ndege, kuliko wa basi.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa usafiri wa basi utatumika tu kwa safari fupi kama vile kwenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar lakini pia mkoani Tanga kucheza na Coastal Union.

Inadaiwa kuwa uongozi wa timu hiyo umefikia hatua hiyo ili kupunguza hali ya uchovu kwa wachezaji wao ambayo wanaweza kukumbana nayo, pindi watakapokuwa wakisafiri kwa muda mrefu kwa kutumia usafiri wa basi.

“Kwa hiyo, msimu huu mambo ndivyo hivyo yatakavyokuwa na uongozi umejipanga vilivyo kwa hilo, kwa hiyo wachezaji safari hii wasituangushe na hatutaki visingizio kuwa wamechoka kutokana na kusafiri kwa umbali mrefu kwa kutumia basi.

“Usafiri huo wa ndege wanatarajia kuanza kuutumia kesho (leo) ambapo wataondoka Dar es Salaam na kwenda Arusha kwa ajili ya kambi ya siku chache tu ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar itakayofanyika Agosti 18, mwaka huu huko jijini Mwanza,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Simba imerejea jana Jumapili kutoka Lindi ilikokuwa imeenda kucheza mechi ya kirafiki ya uzinduzi wa Uwanja wa Majaliwa ulioko Kiwangwa ambao umeitwa kwa heshima ya jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alipoulizwa kuhusiana na hilo Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Iddi Kajuna, alisema kuwa wamejipanga kwa hilo na watatumia njia zote mbili za usafiri pale itakapobidi kufanya hivyo.

“Hiyo ni kweli kwani tumejipanga kwa hilo, ila tutatumia usafiri wa ndege na basi pale tutakapoona inafaa kutumia moja ya usafiri huo kwa ajili ya safari zetu,” alisema Kajuna.

CHANZO: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic