August 27, 2018



NA SALEH ALLY
KWELI kujiendesha katika Ligi Kuu Tanzania Bara ni gharama. Lakini niwe wazi kwamba nimekuwa nashangazwa na udhaifu wa kimfumo wa klabu za ligi hiyo.

Nasema nashangazwa kwa kuwa sioni kuwa viongozi wanaoongoza klabu hizo huwa wanajua kushiriki ligi ni sawa na kuendesha biashara fulani.

Hakuna timu inayoshiriki ligi kwa lengo la kukaa au kubaki tu ligi kuu wakati inakuwa haiingizi faida. Viongozi wengi wa ligi kuu wamekuwa ni wale wenye mawazo ya kizamani na wengi hawajakubali kuingia kwenye mfumo sahihi, mfumo ambao watajiendesha kibiashara.

Hii ni ligi ta ridhaa, lakini mambo mengi yanakwenda kwa mfumo wa ligi ya kulipwa. Lakini hata kama ingebaki kuwa ligi ya ridhaa hasa, basi haizuii kuwa na watu wabunifu au vitengo sahihi vinavyoweza kutengeneza mwendo mzuri wa kifedha katika klabu husika.
Hakuna klabu inayotakiwa kucheza ligi kuu huku ikiingiza hasara kwa misimu mfululizo. Kama ipo, basi viongozi wao watakuwa si wenye malengo na vichwani mwao wamebaki na hisia za kale kuwa soka ni mchezo wa kujifurahisha.

Hali kadhalika, kama kutakuwa na timu inaendelea kuingiza hasara na viongozi wao wanaona sawa au wanapigania kuendelea kubaki ligi kuu wakiwa hawana malengo ya kuingiza faida, basi ni viongozi wenye hesabu mbovu zaidi duniani, nitakuambia kwa nini.

Kila mwanadamu anayejitambua hufikiria mambo mengi sana hasa muda wake. Kupoteza muda kwa ajili ya furaha inawezekana kwa kuwa mwanadamu ataamua kujipumzisha, kwenda kwenye muziki au kuangalia filamu.

Lakini mwanadamu anayepoteza muda wake kwa kufanya mambo ya ujenzi wa jambo akiwa hana lengo la kuingiza faida, huku akijua anapoteza muda, huyu ni mtu aliyetakiwa kuishi zamani sana. Kama yupo, awape watu nafasi, waendeleze anachokifanya.
Soka ni fedha na ndiyo mchezo unapendwa zaidi. Klabu za Tanzania zinajua Watanzania wanapenda fedha na zina nafasi ya kuingiza fedha nyingi kupitia nyanja mbalimbali. Lakini kosa kuu limekuwa ni mawazo yaleyale kwa zaidi ya miaka 20 na viongozi wengi ni walewale.

Nimesikia malalamiko ya baadhi ya klabu za ligi kuu kuwa baada ya kuona hakuna mdhamini,. zingependa kuona ule mfumo wa timu mwenyeji kuchukua mapato yote unabadilishwa na kuwe na mgawanyo.

Lakini wakati zinalia hivyo, hatujasikia klabu yoyote ambayo imeonyesha umakini na umahiri wa kuhakikisha unakuwa na kitengo bora cha masoko kitakachoendelea kuitafutia klabu wadhamini ambao wataisaidia kupunguza gharama za uendeshaji na ikiwezekana siku moja, gharama zote za uendeshaji, ziwe ziko chini ya wadhamini.

Maana yake, klabu inaweza kutafuta wadhamini ambao kama ni sita au saba, kila mmoja kwa fedha anazotoa ndiyo ziwe zinakamilisha gharama zote za uendeshaji. Ukijumlisha kiasi kidogo cha wadhamini wa ligi, klabu inaanza kuingiza faida kuanzia hapo na fedha za viingilio hata kama ni kidogo, zinakuwa sehemu ya faida.

Baada ya hapo, kitengo cha masoko kinaanza kubuni mipango ya kuhakikisha kila timu yake inapocheza, kifanyike nini watu wengi kwenda uwanjani. Kuvuta watu wengi, kutaisaidia klabu kupata fedha nyingi.

Kitengo cha masoko, kinaweza kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu ili kuiondoa klabu katika maisha ya utegemezi na ulalamishi au kila mara kuendesha maisha ya timu kupitia misaada na mifuko ya wenye huruma ambao baadaye hugeuka na kuwa sumu.
Jifunzeni, Ulaya klabu zinajiendesha vipi, halafu tumieni mfumo wa Kiafrika au Kitanzania kujua mtatengeneza vipi fedha badala ya kushiriki ligi kuu kama sehemu ya kujifurahisha.

Timu ina zaidi ya misimu sita ndani ya ligi kuu  na haijawahi kuingiza faida. Hii ni alama ya kutokuwa makini au kujitambua kwa wasiwasi.


4 COMMENTS:

  1. Klabu za wananchi wawekezaji hawaruhusiwi kumiliki zaidi ya 50% tuombe miujiza tu itokee hata akiwa kiongozi ni malaika bila klabu kubinafsishwa hatutavuka huo ndio ukweli zaidi ya hapo ni siasa. Tutazame klabu zinazofanikiwa ili tujifunze

    ReplyDelete
    Replies
    1. TAUCHEN TULIVYO KLABU YA WANANCHI TUNAENDELEZA MICHANGO YETU TUTAFIKA TU TULISHAWAHI KUWA NA HALI NGUMU KULIKO SASA TUSHAFUKUZA WAFADHILI WOTE ENZI HIZO NA WACHEZAJI WOTE TUKAFUKUZA IKAZALIWA PAN SISI YANGA AFRIKA TUKAKAZA BUTI LEO HII NI MAPITO TU KIDOGO

      Delete
  2. Kuwa na wewe kiongozi wa timu moja utuonyeshe mfano

    ReplyDelete
  3. Mfumo wa uendeshaji vilabu ubadilishwe haiingii akilini Club kuendelea kumilikiwa na Wananchi halafu Mwekezaji anapewa 49%!. Mwekezaji aruhusiwe kuwekeza hisa kiasi chochote hata kama ni 100%. Dalili zinaonesha mwaka huu ligi haitakuwa na ushindani kabisa kwa Timu kukosa uwezo wa kifedha kutokana na kukosekana kwa udhamini. Ni kweli viongozi hawana ubunifu hata kidogo ni mradi maisha yaende kila mwaka ni kushiriki tu, hakuna ubunifu wa kuingiza mapato au faida ili kuwezesha vilabu kujijenga kiuchumi>

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic