August 26, 2018



Na Saleh Ally
TAYARI Herietier Makambo amefunga bao lake la kwanza la Ligi Kuu Bara wakati Yanga ikiifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1 katika mechi yao ya ufunguzi.


Makambo alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya 31, maana yake amecheza Ligi Kuu Bara dakika 30 bila bao kabla ya kuandika bao hilo la kwanza linaloingia katika rekodi na benki yake ya mabao.


Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo tayari ni gumzo kuu katika mchezo wa soka kwa kuwa alianza kuonyesha cheche zake wakati wa maandalizi ya msimu mpya licha ya kwamba, Yanga ilionekana haina “maisha mazuri sana”.


Siku moja tulikuwa katika ubora wa mjadala wa Makambo, kwamba ni hatari sana baada ya kufanikiwa kufunga katika mechi dhidi ya USM Alger ya Algeria pia ikiwa ni mechi yake ya kwanza akiichezea Yanga katika mashindano.


Katika mjadala wa kawaida tu wa wadau wa soka, niliwashauri tumsubiri Makambo katika michezo ya ligi na ule dhidi ya Mtibwa Sugar ungekuwa kipimo na baada ya hapo tunaweza kuangalia mchezo mwingine mmoja.


Nasema mmoja, kwa kuwa Makambo amefunga dhidi ya Mtibwa Sugar, timu itakayokuwa ikicheza kimfumo zaidi pia ni timu ya daraja la juu unapozungumzia ligi kuu ikiwa na wachezaji wengi bora na wazoefu.


Lakini bado kuna timu kadhaa hajakutana nazo ambazo ziko zile zilizopanda daraja, zile ambazo mara nyingi hugombea kutoshuka daraja zimekuwa na ugumu wake ambao unakuwa tofauti na unapokutana na Mtibwa Sugar au Azam FC.

Hata  hivyo, tayari Makambo ameonyesha ni mchezaji wa aina yake ambaye kama ataendelea kupata sapoti sahihi, basi atawasaidia Yanga kufanya vema hata kama hawatakuwa na hali nzuri sana kifedha.


Makambo amefunga katika mechi za kirafiki, amecheza mechi moja ya kimataifa amefunga pia lakini amefanya hivyohivyo katika mechi yake ya kwanza ya ligi. Maana yake hakuna sababu ya kuwa na hofu naye.


Unaweza kusema Yanga wamepata mtu wa uhakika na kama ataendelea hivyo, maana yake Makambo atakuwa kati ya usajili mzuri waliofanya katika msimu huu licha ya kuwa na matatizo ya kifedha.


Kocha Mwinyi Zahera lazima alikuwa akijua anahitaji mtu wa namna gani na kamwe ingekuwa vigumu kwake kumpa nafasi mtu anayeona hatakuwa na msaada naye. Tumeliona hilo kutokana na uzuri wa kazi ya Makambo.


Lakini Yanga wanapaswa kuwa makini na ikiwezekana mapema kuanza kujiandaa na hili zaidi litakuwa linamhusu Kocha Zahera ambaye pia ni raia wa DR Congo.

Unaiangalia Yanga kiufundi, katika kiungo unaona ina watu wengi ingawa kwa sasa, Papy Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndiyo wanaonekana kuikamata injini ya timu hiyo.


Kama kutatokea na hitilafu kati yao kwa kuwa majeruhi au ugonjwa, bado inaonekana kuna nafasi kubwa ya kupanga wengine nao wakaendelea kusaidia. Mfano Thabani Kamusoko, Pius Buswita, Said Juma ‘Makapu’ na wengine wanaoweza kuisukuma Yanga ikasonga.

Kwa upande wa ushambulizi, unaona bado kuna tatizo ambalo lazima Zahera aanze kujiandaa sasa. Makambo anaonekana ni mshambulizi hatari wa katikati ndani ya Yanga lakini kunakuwa na shida ya mbadala anayeweza kwenda naye.


Kama Amissi Tambwe angekuwa na utimamu wa asilimia mia, lingekuwa jambo zuri. Wanatoa kifaa wanaingiza kifaa na hii ndiyo maana ya kikosi bora.

Ligi Kuu Bara imeongezwa timu, kuna mashindano ya Kombe la Shirikisho. Kila mechi huwa muhimu na huu unakuwa mtihani mkubwa kwa wachezaji kwa kuwa wana mazoezi, mechi na pia safari. Haya yote ni maumivu.


Kwa mshambuliaji, maisha yake uwanjani mara nyingi anakuwa katika wakati mgumu, anawindwa na kulindwa. Lazima Yanga wajue uhakika wa Makambo kucheza mechi zote hata zile za ligi ni mgumu, hivyo lazima wawe na mbadala.


Angalia katika ushambulizi, Tambwe bado hayuko fiti sawasawa, Matheo Anthony alionyesha ameshindwa kwa makocha tofauti, Zahera ni wa tatu sasa lakini hata Juma Mahadhi alishindwa kuvaa viatu hivyo wakati wa George Lwandamina ambaye aliamua kumtumia kama sehemu ya kuziba pengo na hakuwa na ujanja.


Yupo Yohana Nkomola, huyu bado kinda na kama Zahera ataona anaweza kuwa msaada, lazima awe anapewa nafasi mapema kusudi siku moja awe msaada.

Baada ya kuumia Donald Ngoma, Lwandamina aliamua kumtumia Obrey Chirwa katika nafasi hiyo. Akaendelea kubaki mtu mmoja na alipoingia kwenye mgogoro na uongozi, hakuwa na ujanja zaidi ya kulazimisha.


Hili tatizo kwa kiasi kikubwa liliwaumiza Yanga katika mechi za mwisho za ligi na kuonekana kuwa hawakuwa na kitu. Kitaalamu inaonekana wanataka kulirudia suala hili kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Makambo hataweza peke yake, lakini waliopo pia wanapaswa kuwa angalau na kiwango cha Makambo kwa asilimia 80 ili wakipewa nafasi kama yeye ameshindwa kucheza, wawe msaada mkubwa kwa kikosi.

Zahera anaweza kuwa mwokozi kama ataliona hili na kuanza kufanya maandalizi ya nguvu na kuwapa nafasi wale ambao wanaweza kuwa wabadala wa Makambo, mapema.


Kama watashindwa, basi ajue mapema na wakati wa dirisha basi atakuwa amepata jibu ili mapema aweze kulimaliza kabisa tatizo hilo au la sivyo, mwishoni mwa ligi wakati wachezaji wanakuwa wamechoka na rahisi kupata majeraha, atajikuta katika wakati mgumu sana.





1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic