September 28, 2018


Huu ni mwendelezo wa Gazeti la Championi kukuletea mfululizo wa makala zinazohusu matawi ya timu za Simba na Yanga kama ambavyo ilianza wiki kadhaa nyuma.

Kupitia Championi Ijumaa tunakuletea Tawi la Simba lijulikanalo kwa jina la Simba Home Boys ambalo licha ya kuanzishwa miaka ya karibuni lakini ni miongoni mwa matawi ambayo yana nguvu kubwa kutokana na kuwa bega kwa bega na timu yao hasa kwenye suala zima la kuipa sapoti kwenye mechi zake.

Tawi hilo ambalo lipo Tegeta Wazo Hill Mtaa wa Msikitini jijini Dar es Salaam, linaongozwa na mwenyekiti wake, Hassan Keya Kaniki sambamba na katibu ambaye pia ni mweka hazina wa tawi hilo, Abubakari Said Shaban.

Wawili hao wanafunguka kama ifuatavyo: “Tawi letu lilianzishwa na wapenzi wa Simba kwa ukanda huu wa Wazo Hill Agosti, 2014 na lina jumla ya wanachama 165 ambao wana kadi za uanachama wa Simba. “Wengine zaidi ya 200 wanatambulika na tawi lakini bado hawana kadi za uanachama wa klabu yetu,” anaanza kufunguka

Abubakari Said kabla ya kumpa kijiti mwenyekiti wake, Hassan Kaniki ambaye yeye anaelezea mambo mbalimbali ya tawi hilo.

MUUNDO WA UONGOZI UPOJE KATIKA TAWI LENU?

“Muundo wa uongozi katika tawi letu ni uleule wa kawaida, kuna mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu ambaye ndiye mweka hazina, wajumbe na kamati za utendaji.

SHUGHULI GANI MNAFANYA KULIENDESHA TAWI LENU?

“Sisi kama tawi tumeandaa katiba ambayo itatutambulisha kama kikundi cha wajasiriamali ambayo ishapelekwa kwa msajili, ikishakamilika ndipo tutaweza kufanya shughuli nyingine za kijamii licha ya kuwa tunajishughulisha zaidi na michezo ambayo itakuwa inaleta manufaa katika timu.

MNATOA SAPOTI GANI KWA TIMU YENU?

“Sisi tunatoa sapoti ya aina yoyote ambayo inahitajika kutoka makao makuu kama kuna suala la kuchangia timu na kutoa msaada wowote utakaohitajika. “Pili huwa tunakwenda katika mechi yoyote ambayo timu yetu inapocheza, sisi tupo tofauti na matawi mengine kwa sababu huwa hatuchagui mechi za kwenda, tunakwenda katika kila mechi hata za mikoani na utakuta tambara letu lenye nembo ya

MNAJISHUGHULISHA NA MIRADI GANI KATIKA KUJIINGIZIA KIPATO?

“Hatuna shughuli nyingine zaidi ya sisi wenyewe kujichangisha pale tunapokuwa tunahitaji fedha kama tukiwa tunahitaji shilingi laki tano au milioni moja basi tunaitana na kuchangishana na kisha tunaweka kwa mweka hazina, inaenda kufanya ile kazi tunayohitaji ifanyike.

FEDHA ZA KUSAFIRI KWENDA KWENYE MECHI MNAZIPATAJE?

“Tulikubaliana kuwa baada ya kutegemea zile fedha ambazo huwa tunachangishana kila baada ya muda na kuziweka kwa mweka hazina, haziguswi, badala yake tunakuwa tunachangishana nyingine kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kwenda kwenye mechi. “Baada ya kwenda, wakirudi tunapiga mahesabu na kujua kiasi gani kimetumika na kujua wapi kulikuwa na mapungufu tunaelekezana lakini pia wakati wa kuchangishana ikitokea  imepungua basi huwa tunakamatana viongozi na kufanya utaratibu wa kuiwezesha safari.

MNAJIVUNIA KITU GANI MLICHOKIFANYA KWA SIMBA MPAKA SASA?

“Kwanza tulikuwa na ahadi ya kutoa mifuko 200 ya sementi

kuchangia ujenzi wa uwanja kule Bunju, hivyo ahadi yetu ipo palepale pindi ujenzi ukianza tutaitana na kutoa mchango wetu kama tulivyoahidi, kwani hatuwezi kupeleka sasa hivi tunahofia haitotumika katika lengo ambalo tumelikusudia.

MAPATO YENU KWA MWAKA YAPOJE KATIKA TAWI LENU?

“Hatuna kitu ambacho kinatuingizia mapato kwa sasa hivi kwa sababu hatujaanza biashara bado, ila kwa kuwa tumeshaandaa katiba tumekubaliana kila mwanachama awe anachangia kiasi fulani cha fedha ambacho tutafungua akaunti benki na kuhifadhi. 

“Tuna malengo ya kufanya kazi za kijamii, mfano kuna masuala ya kuzoa taka tunaweza tukanunua kifaa cha kubebea taka hizo na kuweka jiji letu safi katika mitaa mbalimbali na fedha zote zikipatikana zitaenda benki,  zitatusaidia kuliendesha tawi letu.

MALENGO YENU NI YAPI? “Malengo yetu ni kumiliki basi letu wenyewe ambalo litakuwa linatusaidia katika kufanya safari zetu za mikoani katika kuisapoti timu. 

“Ila hilo haliwezi kukamilika mpaka katiba yetu iwe tayari kwa sababu tunapata vikwazo fulanifulani katika kuyafikia malengo kwa kuwa katiba yetu bado haijakamilika.

TOFAUTI YENU NI IPI NA MATAWI MENGINE? “Tofauti ipo kwenye malengo, kwa sababu sisi tawi letu hatutaki kuishia kuwa kundi la ushangiliaji peke yake, tunataka tufanye masuala mengine ya kijamii katika eneo husika au mkoa husika kwa kufuata kanuni za kikatiba.



MMEJIPANGAJE KUELEKEA MECHI DHIDI YA YANGA?

“Tumeshaanza kuandaa hamasa katika tawi letu kuelekea mchezo huo wa Jumapili hii, lakini pia tunaandaa tisheti ambazo zitavaliwa na wanachama kwa sababu tuna mashine ya kuchapisha hizo tisheti. 

“Pili tuna mpango wa kuleta mashine ya kukatia tiketi hapahapa kwenye tawi letu ili wanachama wetu wasipate taabu ya kwenda mbali kufuata tiketi za mchezo huo.

“Pia tunaandaa utaratibu wa usafiri, tunataka tuwe na usafiri wa uhakika huku tukitengeneza ushirikiano na matawi mengine ili kuhakikisha timu yetu inapata ushindi siku hiyo,” anasema Kaniki na kuongezea: 

“Niwaombe wanachama wenzangu wa Simba kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu yetu, mimi kama kiongozi wa Home Boys, pia niwaombe Watanzania kwa jumla tutengeneze umoja ili tuweze kufikia malengo yetu na kufanikisha mabadiliko na kupata viongozi bora watakaoendesha vizuri klabu yetu.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic