September 19, 2018


Kampuni maarufu ya vinywaji ya Coca-Cola ni maarufu zaidi kwa kutengeneza soda, lakini sasa inapanga kufanyia majaribio aina mpya ya kinywaji. Kinywaji ambacho kitakuwa na bangi. Lakini je, kitalewesha?

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa BNN Bloomberg, kampuni hiyo itashirikiana na kampuni mwenyeji ya kutengeneza bangi kwa jina Aurora Cannabis. Lengo kuu la kuwa na kinywaji hicho litakuwa ni kupunguza maumivu na si kuwalewesha watu. Kampuni hiyo bado haijazungumzia hadharani mpango huo lakini imekiri kwamba inafuatilia kwa karibu matukio katika sekta ya vinywaji vyenye bangi.

“Kwa pamoja na wadau wengine wengi katika sekta hii ya vinywaji, tunafuatilia kwa karibu ukuaji wa soko la vinywaji vyenye bangi aina ya cannabidiol visivyolewesha kama kiungo katika vinywaji vya kuboresha afya maeneo mengi duniani,” taarifa ya Coca-Cola imesema. Cannabidiol, ni moja ya viungo vinavyopatikana ndani ya bangi, na inaweza kusaidia kupunguza kuvimba, maumivu na kuganda kwa misuli.

Lakini huwa haiwezi kulewesha. Hatua ya Coca-Cola inajiri huku Canada ikijiandaa kuyafuata baadhi ya majimbo ya Marekani ambayo majuzi yameidhinishwa matumizi ya bangi kwa sababu za kujiburudisha, baada ya kukubali matumizi ya bangi kwa sababu za kimatibabu kwa miaka mingi. Hatua hiyo imechangia kuibuka kwa biashara kubwa ya ukuzaji wa bangi, pamoja na kuundwa kwa ushirikiano wa kampuni kubwa katika biashara hiyo.

Mapema mwaka huu, kampuni kubwa ya utengenezaji wa bia ya Molson Coors Brewing ilitangaza kwamba itakuwa ikitengeneza vinywaji vyenye bangi kwa ushirikiano na kampuni ya Hydropothecary, huku kampuni inayotengeneza bia ya Corona, Constellation Brands, ikiwekeza zaidi ya $4bn zaidi katika kampuni ya bangi ya Canopy Growth.


Ushirikiano kati ya Coke na Aurora utakuwa ni kisa cha kwanza kabisa kwa kampuni kubwa ya uzalishaji wa vinywaji visivyolewesha kujiingiza katika biashara hiyo ya bangi.

BNN Bloomberg, wakinukuu wadokezi ambao hawakutaka kutajwa, wamesema Coca-Cola wanafanya mazungumzo “yenye uzito” na Aurora lakini kufikia sasa hawajapata maafikiano yoyote. “Mazungumzo yamepiga hatua sana” na maafikiano yanakaribia kupatikana, mdokezi mmoja alinukuliwa akisema. “Itakuwa ni katika kitengo cha ‘vinywaji vya kuponya’ (au kumpa mtu ahueni),” mdokezi huyo ameongeza.


Aurora, kupitia taarifa wamesema hawataki kuzungumzia mipango yao ya kibiashara hadi ikamilishwe.Lakini aliongeza: “Aurora wameeleza hamu yao kuu katika kutumia fursa ya kibiashara katika vinwyaji vyenye kuongezwa vileo, na tunakusudia kuingia katika soko hilo.”Hisa za Coca-Cola zilipanda bei kiasi mapema Jumatatu.

Kutoka Global Publishers

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic