September 19, 2018


Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera amewaambia mabeki wa timu pinzani kuwa yeye hana hofu wao waendelee kumkaba mshambuliaji wake Heritier Makambo kwani wapo Ibrahim Ajibu na Mrisho Ngassa wenye uwezo mkubwa wa kufunga.

Kauli hiyo aliitoa baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kumalizika kwa Yanga kuwafunga Stand United mabao 4-3 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, mabao ya Yanga yalifungwa na Andrew Vincent ‘Dante’, Deus Kaseke, Ngassa na Ajibu huku mabao matatu ya Stand yakifungwa na Alex Kitenge.

Zahera alisema anafahamu hivi sasa mshambuliaji wake Makambo anapaniwa na kila timu inayokutana naye kutokana na kutajwa kwenye vyombo vya habari na kusababisha kuzua hofu.

Zahera alisema, alichokifanya hivi sasa ni kutengeneza washambuliaji wengine watakaofanya kazi ya Makambo ambayo ni kufunga mabao katika kila mechi baada ya kuona mshambuliaji huyo kapaniwa na mabeki wa timu pinzani.

Aliongeza kuwa, amefurahishwa na jinsi washambuliaji wake wengine Ajibu, Ngassa na Kaseke anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, kufuata maelekezo yake aliyowapa kwa kufanyia kazi na kupata ushindi huo wa mabao 4-3.

“Lipo wazi kabisa, kila timu tunayokutana nayo hivi sasa inamuangalia Makambo pekee, wenyewe wanaamini wakimzuia huyo ndiyo basi Yanga hatuwezi kupata ushindi, kitu ambacho siyo.

“Hivyo, niwaambie kuwa, wao waendelee kumkaba Makambo na wawaache wachezaji wengine waendelee kufunga mabao, ninaamini kwa wachezaji hawa nilionao nina uhakika wa kupata matokeo mazuri katika kila mechi.

“Nimefurahishwa na safu yangu ya ulinzi inayocheza kwa kujiamini na kutengenezeana nafasi za kufunga kama ilivyokuwa mchezo wa ligi na Stand ambao wachezaji wangu walitumia vema kila nafasi waliyokuwa wanaipata.

 “Naamini mimi nina wachezaji wengi ambao wanaweza kufunga mabao, ukimzuia Ajibu atafunga Makambo, ukimzuia Makambo atafunga Ajibu, hivyo sina shida,” alisema Zahera.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic