KISA STARS, ULIMWENGU AIKACHA AL HILAL YA SUDAN
Ikiwa imesalia siku moja pekee kuelekea mechi ya kimataifa kuwania nafasi ya kufuzu AFCON, Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Thomas Ulimwengu amesema nguvu zao zote kwa sasa ni kuwakabili Uganda.
Ulimwengu amesema kwa namna walivyojiandaa na mafunzo ambayo wamepewa na Kocha Mkuu, Emmanuel Amunike pamoja na Msaidizi wake Hemed Morocco, anaamini yatawakamilishia malengo yao Jumamosi hii.
Mchezaji huyo ambaye anacheza soka lake la kulipwa nchini Sudan katika klabu ya Al Hilal, amekataa kuzungumzia chochote kuhusiana na klabu yake kwa kueleza akili yao hivi sasa ni mechi dhidi ya Uganda.
Alipoulizwa juu ya namna soka lilivyo huko Sudan na klabu anayoichezea, Ulimwengu alikwepa na kusema hawezi kuongea chochote mpaka mara baada ya kulitumikia taifa lake Jumamosi kwa maana wamejipanga kushinda.
Stars inashuka kesho Jumamosi kukipiga na Uganda ambapo mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Nambole jijini Kampala.








0 COMMENTS:
Post a Comment