September 2, 2018


Moja kati ya michezo inayofuatiliwa kwa wingi zaidi dunia ni soka, hilo halina ubishi mchezo huu unapendwa sana na ndiyo maana hata wawekezaji wamekuwa wakipigana vikumbo kumwaga fedha nyingi zaidi ili kujitangaza.

Angalia jezi wanazovaa wachezaji, vifuani mwao kuna wadhamini ambao wanamwaga fedha nyingi sana, mikononi pia, mgongoni yaani sehemu kubwa zimetapakaa logo au maandishi ya matajiri ambao wanataka kutangaza biashara zao kupitia wanasoka.

Ndiyo, hata hapa nchini soka linapendwa kwelikweli. Pamoja na wachezaji kulipwa mkwanja mrefu, pia makocha nao wanalipwa fedha ndefu ili tu kupandikiza morali kwa wachezaji wao ambao wanapo-shinda basi kila kitu kinakuwa sawa.

Hapa nchini makocha wengi wanapa-mbana kuhakikisha nao wanazisaidia timu zao kufanya vyema kwani wakifanya hivyo maana yake madau yao yakua hivyo uhakika wa maisha kwa asilimia 100 unakuwepo bila shaka.


Kama ilivyo kawaida Championi Jumamosi, huwa tunakuandalia vitu adimu kuviona kwingine, wiki iliyopita tulikuwa na thamani ya viatu kwa wachezaji nyota wa ligi kuu, leo hii tumeona ni vyema ukajua makocha wanapewa mshahara kiasi gani kwenye timu zao za ligi kuu. Chini ni uchambuzi wa mishahara ya makocha Bongo:

HANS VAN DER PLUIJM- AZAM FC
Moja kati ya makocha wenye mafanikio kwenye soka la Bongo hasa akiwa anakinoa kikosi cha Yanga, msimu uliopita aliifundisha Singida United na sasa yupo Azam FC. Akiwa Yanga alitwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo na Kombe la FA huku akiipeleka timu hiyo hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya kuondoka Yanga ambayo ilikuwa kwenye hali mbaya kiuchumi wakati huo, Mholanzi huyo alitua Singida United ambapo dola 9,000 (Tsh Mil 20.5) kwa mwezi, Azam walivutiwa na ufundishaji wake hivyo wakamvutia waya na kumwambia watamuongeza na dola la 10,000 (Tsh Mil 22.7) babu hakuwa na subira akaenda zake Chamazi na ameanza vizuri tu ligi.

PATRICK AUSSEMS- SIMBA
Uongozi wa Simba uliamua kuachana na Mfaransa, Pierre Lechantre kutokana na mshahara mkubwa ambao alikuwa akichukua kwa mwezi kiasi cha dola 13000 (Tsh Mil 29.6) msimu uliopita.
Baada ya mkataba wake kumalizika tu Simba ikaachana naye na kwa wakati huo alikuwa ndiye kocha aliyekuwa akichukua fedha ndefu kati ya makocha wenzake Bongo. Simba sasa imemshusha Mbelgiji, Patrick Ausssems ambaye inaelezwa anachota dola 10,000 (Tsh 22.7mil) kwa mwezi.

JUMA MWAMBUSI– AZAM FC
Huyu ndiye kocha aliyeipandisha Mbeya City msimu wa 2012/13 na kuifanya timu hiyo iwe na soka la kuvutia na kasi muda wote bila kuchoka, baadaye alitua Yanga kama kocha msaidizi chini ya Hans Pluijm lakini ghafla akawa amepotea kwenye soka baada ya kuachana na Yanga msimu uliopita.

Kocha huyo mwenyeji wa mkoani Mbeya kwa sasa anashikilia mikoba ya usaidizi akiwa na swahiba wake, Pluijm ambapo amekuwa akikunja kibindoni mshahara wa kiasi cha dola 3500 sawa na Sh Mil 7.9 za Kitanzania.

MASOUD DJUMA- SIMBA
Huyu ni Kocha Msaidizi wa Simba, raia wa Burundi ambaye inadaiwa kwa sasa hana uhusiano mzuri na uongozi wa timu hiyo na wakati wowote huenda akachimbishwa kwenye timu hiyo kutokana na mgogoro wa chini unaoendelea kwenye timu hiyo.
Djuma ambaye pia ni kocha wa zamani wa Rayon Sport ya Rwanda na akifanikiwa kuipa ubingwa wa nchi hiyo, anachota kitita cha Sh mil 13.6 ndani ya Simba kwa kila mwezi ikiwa sawa na dola 6,000.

MWINYI ZAHERA- YANGA
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo ambaye amechukua mikoba ya Mzambia, George Lwandamina, taratibu Zahera ameanza kuifanya Yanga kuwa moto wa kuotea mbali ambapo kwa mwezi kocha huyo anachota Sh mil 6.8.

NOEL MWANDILA- YANGA
Noel Mwandila raia wa Zambia amedumu Yanga kama kocha msaidizi licha ya bosi wake, George Lwandamina aliamua kuondoka zake kwa sasa anafanya kazi yake chini ya Zahera ambapo kwa mwezi anachukua shilingi milioni saba.
SOCCOIA LIONEL-AFRICAN LYON
Lionel ni kocha mpya wa African Lyon iliyopanda daraja msimu, kocha huyo raia wa Ufaransa mwenye Leseni A ya ukocha kutoka katika Shirikisho la Soka Ulaya ‘Uefa’ kwa mwezi anachukua mshahara wa Sh.Mil15.

HEMEDI MOROCO – SINGIDA UNITED
Kocha mpya wa Singida, Hemed Moroco amekubali dili la kuifundisha timu hiyo akichukua mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijm kwa mshahara wa dola 3000 ambao sawa na Sh mil 6.8.

SELEMAN MATOLA- LIPULI
Moja kati ya makocha vijana wanaofanya vyema, huyu yupo Lipuli FC ya Iringa. Akaunti yake kila mwezi huwa inasoma Sh Mil 4 ambayo ni malipo kutoka kwa mabosi zake wa Lipuli.

ETIENNE NDAIRAJIGE- KMC
Ngairagije ni Kocha Mkuu wa KMC ambaye hivi karibuni alikabidhi mikoba ya kukinoa kikosi hicho kwenye msimu huu wa ligi akitokea Mbao FC ikiwa siku chache tangu timu hiyo ipande ambaye inaelezwa anachota Sh mil 4.

MALALE HAMISI- NDANDA FC
Wengi huenda hawamfahamu kocha huyu lakini ukienda Zanzibar, ukakatiza Mitaa ya Darajani, Forodhani, Mwanakwerekwe na kule Uwanja wa Amaan hasa pale kwenye kijiwe cha kawaha basi hapo utapata habari zake vizuri kabisa, lakini waulize kwa jina la Keha ambalo ndiyo maarufu eneo hilo.

Huyu ni Malale Hamsini Kocha Mkuu wa Ndanda, anasifika kwa soka la pasi lakini kutokana na uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa pamoja na kazi ngumu anayofanya yeye mwisho wa mwezi anawekewa Sh mil 1 kwenye akaunti yake huku mchezaji anayeongoza kwa mshahara mkubwa klabuni hapo akipewa Sh 600,000.

Makocha wengine wamekuwa wakilipwa Sh Mil mbili ambao ni Amri Saidi wa Mbao FC, Mbwana Makata (Alliance), Hitimana Thierry (Biashara), Ally Bizumungu (Mwadui).
Wengine ni Amars Niyongabo wa Stand United, Bakari Shime (JKT), Abdulmtik- Haji (Ruvu Shooting), Juma Mgunda (Coastal), Abdallah Mohammed (Prions), Ramadhan Nsanzarwimo (Mbeya City), Zuber Katwila (Mtibwa Sugar) na Mecky Maxime wa Kagera Sugar.

CHANZO: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic