September 20, 2018


Cristiano Ronaldo alitokwa na machozi baada ya kuoneshwa kadi nyekundu katika njia ya utata wakati wa mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya Juventus na Valencia nchini Uhispania.

Mshambuliaji huyo wa Ureno alikuwa anawachezea Juve mechi yake ya kwanza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tangu ajiunge nao.

Alionekana kushika nywele za beki wa valencia Jeison Murillo wawili hao walipokuwa wanang'ang'ania mpira dakika ya 29.

Mwamuzi mkuu wa mechi hiyo Felix Brych alishauriana na mwamuzi msaidizi kabla ya kumuonesha Ronaldo kadi nyekundu moja kwa moja.

Juve, ambao walikuwa wamesalia na wachezaji kumi uwanjani, walijizatiti na kuchukua uongozi muda mfupi kala ya kipindi cha kwanza kumalizika kunako dakika ya 45 kupitia mkwaju wa penalti uliofungwa na Miralem Pjanic.


Muda mfupi baada ya kipindi cha pili kuanza, kiungo huyo wa kati wa Bosnia alifunga bao jingine kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 51.

Valencia baadaye walizawadiwa penalti lakini kipa wa Juve Wojciech Szczesny akaokoa mkwaju huo wa Daniel Parejo na kuwawezesha Wataliano hao kumaliza mechi bila kufungwa bao.

Yalikuwa ni marejeo ya machungu kwa Ronaldo Uhispania, baada yake kuhamia Juve kutoka Real Madrid kwa £99.2m majira ya joto.


Alikuwa ameanza kutamba kwenye mechi pale alipojaribu kufikia krosi, lakini akazuiwa na Murillo aliyekuwa anaanguka.

Alimwashiria Murillo ainuke na alionekana kuvuta nywele za beki huyo kala ya kuondoka, na kuonekana mwenye kutamauka.

Huku uhasama ukizidi, wachezaji hao wapinzani walikabiliana kwenye eneo la hatari na mwamuzi akashauriana na msaidizi wake kwa kipindi kirefu kidogo kabla ya kuchomoa kadi nyekundu.

Ronaldo, anayeshikilia rekodi ya ufungaji mabao Ligi ya Klabu Bingwa, alionekana kughadhabika sana na alijaribu kujitetea kabla ya mwishowe kuondoka uwanjani akitokwa na machozi.


Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kwake kufukuzwa uwanjani mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Cristiano Ronaldo atazuiwa kucheza mechi gani, na je, kun auwezekano wowote wake kuikosa mechi dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford? Manchester United wamo kundi moja ya Juve pamoja na Young Boys na Valencia. United walishinda 3-0 mechi yao.


Tofauti na Ligi ya Premia ambapo marufuku ya kadi nyekundu ya moja kwa moja huwa ni kutocheza mechi tatu, adhabu ya Uefa huangazia kwa kuzingatia kisa chenyewe.

Marufuku ya kutocheza mechi moja huwa ni lazima, na hakuna haki ya kukata rufaa. Lakini kanuni za Uefa nambari 50.01 zinazosimamia michuano hiyo zinasema "iwapo kosa litakuwa kubwa sana, jopo la Uefa linaloangazia udhibiti, maadili na nidhamu lina haki ya kuongeza adhabu hiyo."

Ronaldo, 33, bila shaka ataikosa mechi itakayofuata ya Juve Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambayo itakuwa dhidi ya Young Boys mnamo 2 Oktoba.

Iwapo marufuku itaongezwa na kuwa mechi mbili, basi ataikosa mechi dhidi ya klabu yake ya zamani Manchester United mnamo 23 Oktoba uwanjani Old Trafford.

Na iwapo atapewa marufuku ya mechi tatu, basi ataikosa hata mechi ya nyumbani dhidi ya United mnamo 7 Novemba.


Juve wanatarajiwa kukata rufaa dhidi ya jaribio lolote la kutaka kuongeza marufuku hiyo.

Kiungo wa kati wa zamani wa Man Utd Darren Fletcher anatarajia Ronaldo atacheza mechi zote mbili.

"Ilikuwa adhabu kali kwa kosa ndogo kwa Ronaldo, lakini kwa kufuata sheria kikamilifu hauruhusiwi kufanya hivyo (hilo ni kosa), kwa hivyo nafikiri marufuku ya mechi moja itasalia," mchezaji huyo wa Stoke kwa sasa aliambia BBC.

"Atajihisi ni kama aliwakosea wachezaji wenzake, lakini natarajia acheze mechi zote mbili dhidi ya Manchester United."


Beki wa zamani wa United Rio Ferdinand aliandika kwenye Twitter kwamba hana shaka kwamba Juve watakata rufaa. Lakini mshambuliaji wa zamani wa Celtic Chris Sutton anaamini Ronaldo anaweza tu kujilaumu mwenyewe.

Teknolojia ya kutumia video kuwasaidia waamuzi, maarufu kama VAR haitumiki katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu.

Ronaldo alinusurika kuonyeshwa kadi nyekundu akichezea Ureno dhidi ya Iran katika Kombe la Dunia pale VAR ilipoonyeshwa alihitaji tu kuonyeshwa kadi ya manjano.


Na meneja wa Juve Massimiliano Allegri alisema baada ya mechi ya Jumatano kwamba VAR ingelisaidia uamuzi wa refa.

"Kuwa na wachezaji 10 katika mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kosa kama hilo ni jambo la kusikitisha. Tulihatarisha sana usiku wa leo kutokana na hili, na tutamkosa sana katika mechi zifuatazo pia.


"Alikuwa na masikitiko, lakini huchukua muda kutulia. Ni lazima aukubali uamuzi huo na awe tayari kwa mechi ya Jumapili, [dhidi ya Frosinone], hata ingawa kuna mambo yanayokuacha na machungu sana."

Kutoka BBC

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic