September 23, 2018






NA SALEH ALLY
VIONGOZI wa siasa wengi sana wamefeli katika mambo yao baada ya wananchi kuwachoka kutokana na kutokuwa wakweli.
Kawaida mwanadamu anapodanganywa mara moja au mbili, huamini ni bahati mbaya. Lakini ahadi za uongo zinapozidi huanza kuhisi anadharauliwa.

Sijui ni kwa nini, mwanadamu akihisi anadharauliwa huingiwa na hasira na wakati mwingine kujenga chuki au tabia ya kupuuzia au kutoliamini kila linalozungumzwa, hasa na mtu au watu ambao wamewahi kumuahidi kwa muda mwingi bila ya kutekeleza.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, imetekeleza ahadi zake ambazo zinaifanya kuwa gumzo au kusimamisha mijadala mingi ambayo mingi ilizungumzia kutowezekana kwa kile kilichokuwa kikitolewa kama ahadi.

Ilikuwa ni rahisi sana kuamini ahadi inayotolewa isingewezekana kwa kuwa awali limekuwa ni jambo la kawaida, kutoka kwa ahadi na utekelezaji ukawa ni hadithi tu.
Moja ya ahadi zilizoonekana zisingewezekana ni daraja la mchepuko wa juu katika eneo la Tazara. Daraja hilo maarufu kama Flyover ni la kwanza la magari la aina hiyo hapa nyumbani na hata kama yapo, huenda yanafanana lakini si kwa eneo kama hilo.

Baada ya utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo linalosaidia kupunguza msongamano katika eneo hilo, huenda utakuwa wakati mzuri sana kwa Wanasimba na Yanga kupata angalau nafasi kidogo wakapite juu ya daraja hilo.

Wakati ukiwa unapita jaribu kujiuliza maswali na moja wapo ni lile la kuvunja utamaduni wa viongozi wanaotoa ahadi bila ya kutekeleza na utaratibu wa kuamini mambo fulani ni magumu na hayawezekani.

Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli, imebadili upepo na kuonyesha mambo yanawezekana na inakuwa sahihi kuamini inawezekana ili kufanyia utekelezaji.

Aidha, huu ni ujumbe kwa viongozi wa Yanga na Simba ambao mmekuwa mkitoa ahadi rundo na utekelezaji unakuwa kiduchu kama ambavyo imekuwa tabia ya wanasiasa wengi.

Sasa mambo yamebadilika, kwamba unapoahidi, basi tekeleza kwa kuwa kuendelea kuahidi bila ya kufanya utekelezaji ni uongo, udanganyifu na dharau kwa mashabiki na wanachama wanaokuamini.
Simba na Yanga kumekuwa na ahadi nyingi kuhusiana na viwanja vya mazoezi, jambo ambalo limekwenda miaka nenda rudi bila ya kufanyiwa utekelezaji.

Ahadi hiyo imetumika kwenye uchaguzi, imetumika kupoza mambo wanachama au mashabiki wanapocharuka na kadhalika lakini mambo yamekuwa yanakwenda kimyakimya.

Viongozi wanapoona kama kuna tatizo, hutembelea viwanja vyao kama wanafanya ujenzi au kufanya usafi na baada ya hapo huwapoza wanachama wao kupitia kuonyesha kama kuna jambo walikuwa wanafanya.

Wamekuwa wakifanya hivyo miaka nenda rudi lakini inaonyesha wazi hawako sahihi na wanajua wanadanganya na bila ya haya wamekuwa wakiendelea kufanya namna hiyo.

Kama hiyo haitoshi, tabia hiyo mbaya imekuwa ikienda kwa urithi. Kwa kuwa viongozi wanarithishana maana wanaoondoka huwaachia wanaoingia, mwisho walioingia nao huwa ndani ya mkumbo wa kufanya yaleyale ya ahadi bila ya kutekeleza.

Leo ni zaidi ya miaka 30 Simba na Yanga wanazungumza kuwa na viwanja. Yanga wanao lakini hawawezi kuujenga. Simba wanao hali kadhalika hawana nguvu ya kuujenga!

Wanataka nini? Vipi maneno mengi bila ya utekelezaji? Kama daraja la Tazara lingeongozwa na maneno, lingeisha lini? Hakika mnapaswa kujitafakari na kuachana kabisa na longolongo ili mjenge viwanja kwa ajili ya timu zinazomilikiwa na klabu zenu.

Acheni mawazo hasi ya kuhisi ukifanya jambo fulani litawafaidisha wengine wakati wewe haupo. Jengeni viwanja ili muweze kujivunia utekelezaji baada ya maneno kama ambavyo mnaona Serikali ya awamu ya tano inavyojivunia kazi nzuri ya daraja ililoahidi na baadaye kukamilisha ujenzi wake.



2 COMMENTS:

  1. Tabu sana kumpata kiongozi mzalendo atakae weka ubinafsi wake pembeni na kuweka maslahi ya taasisi anayoiongoza mbele. Simba wanaweza kufanikiwa sana tu kwa sasa na hii inatokana na kiongozi wao mkuu kwa sasa amabae ni muekezaji wao Mohamedi Mo kuwa ni mkeretwa na mwenye mapenzi ya dhati kwenye ile timu. Watu watasema watakavyo kuhusu Mo kwakuwa kuna baadhi ya watu walishajaribu au kufanikiwa kumuekea vigingi Mo asikaribie pale Simba hapo awali.Hao ni watu ambao walitaka Mo awe mfadhili asiekuwa na dhamana ndani ya Simba lakini wakati huohuo viongozi hao wawe na dhamana na ufadhili wake ndani ya Simba. Kitendo cha kupata uwekezaji ndani ya Simba kitampa nafasi Mo ya kusimamia na kuhoji pale atakapoona kuna walakini katika uendeshaji wa timu. Kazi ya uekezaji si tu kutoa na kilipia mishahara ya wachezaji na kugharamia gharama za usajili bali kazi kubwa ni kubuni na kuanzisha na kuendeleza hata kugharmia miradi ya maendeleo ndani ya timu kuhakikisha klabu inakuwa imara kiuchumi na kumudu gharama za uendeshaji kulingana na mahitaji ya timu kama vile kugharamia gharama za kulea kikosi cha ushindani. Kwa hivyo uwekezaji ndani ya timu zetu ni muhimu wameanza Azam na kila mtu shahidi jinsi timu ile ilivyo tulia katika kujiendesha na licha baadhi ya wadau kuhoji mafanikio ya Azam ndani ya uwanja lakini kitakwimu Azam ipo juu ya Simba na Yanga kama utachukulia umri wa Azam na mafanikio yao na umri wa Simba na Yanga yao tangu kuanzishwa kwa vilabu hivyo. Viongozi wengi wa timu zetu ni wababaishaji na ni wajanja wa mjini wanaohangaikia dili zao kwa kupitia timu wanzoziongaza na wakati wa mageuzi umefika ili kupata viongozi sahihi wenye nia ya dhati katika kuleta maendeleo ndani ya timu zetu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic