September 1, 2018



*Zinafanyika Nigeria, ndiyo zile walizoshinda Lulu, Richie

Na Saleh Ally, Lagos
UKISEMA wakati mwingine tena wa tuzo kubwa zaidi za filamu barani Afrika hautakuwa umekosea.


Huu ndiyo huwa wakati ambao bara zima la Afrika husimama hasa kwa upande wa sanaa za filamu kutaka kujua nini kinaendelea. Kwa Nigeria hapa, ndiyo tamasha lenye msisimko mkubwa zaidi kwa kuwa huwakutanisha mastaa wengi sana wale wa filamu na muziki.


Tamasha la African Magic Viewers Choice Awards (AMVCA) linafanyika hapa katika miji ulio katika Kisiwa cha Victoria na hii ni sehemu ya Jiji la Lagos. Tuzo ambazo, watazamaji wanakuwa na nafasi kubwa kwa kuwa wanapiga kura kuwachagua ambao wanaamini ni washindi.


MultiChoice, imekuwa ikifanya kazi kubwa kuhakikisha tuzo hizo chini ya chaneli maarufu zaidi ya filamu barani Afrika ya African Magic, imekuwa ikihakikisha kila kitu kinakwenda salama salimini.


Watanzania wawili wataiwakilisha Tanzania katika tuzo hizo ikiwa na kumbukumbu kushinda tuzo mbili katika tuzo za mara ya tano baada ya Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Single Mtambalike ‘Richie’ kila mmoja wao kuibuka na ushindi.


Hizi ni tuzo za mara ya sita na Watanzania watawakilishwa na Amil Issa Shivji, huyu ni kati ya watengeneza filamu bora kabisa ambaye hata tuzo za mwaka jana alikuwa hapa Victoria lakini bahati mbaya hakufanikiwa.


Shivji ni editor na ‘prodyuza’ mahiri, filamu za ‘Samaki Mchangani’ ni kati ya zilizompa sifa kubwa. Iliingia katika tuzo hizi mwaka jana haikushinda, lakini bado ameendelea kufanya vema na filamu kama Who Killed Me na Shoesine, hii ilitoka mwaka 2013.


Matarajio makubwa ya yeye kufanya vizuri katika kipengeleza cha mtengeneza filamu bora huku Watanzania wakiwa na matumaini pia kwa Lester Millado.


Lester Millado, Mtanzania anayefanya kazi zake sehemu mbalimbali. Nyumbani Tanzania, Kenya na pia Canada. Mmoja wa wataalamu wa utengenezaji filamu katika mfumo wa Cinematography. 


Millado amefanya vizuri na Tamthilia ya T-Juncition ambayo imempa nafasi ya kuwania tuzo katika kipengele cha Best Cinematography/TV Series akichuana na Dickson Godwin na Tamthilia ya Idemuze, Rwamasigazi Kyakunzire (The Torture), Yinka Edward (Okafor Laws) na Akpe Ododoru (Tatu).


Inaweza ikawa nafasi nyingine kwa Watanzania hao kuiwakilisha Tanzania kwa mara nyingine ingawa wanaonekana kuwa katika ushindani mkubwa sana.


Kama hiyo haitoshi, idadi ndogo ya Watanzania waliopata nafasi safari hii ni ujumbe kuwa Watanzania wanapaswa kukaza kamba hasa kuhakikisha wanafanya vema.


Tuzo hizo zimekuwa zikizidi kuwa kubwa na maarufu lakini idadi ya Watanzania ambao wamekuwa wanashiriki kama sehemu ya wanaowania tuzo imekuwa ikizidi kuporomoka.

Katika tuzo hizo za leo, pamoja na ushiriki wa nyota wengi wa filamu wakiwemo waigizaji na watengenezaji, lakini kuna wanamuziki walioalikwa kwa ajili ya kutumbuiza na wengine watashuhudia shoo.


Prudyuza maarufu Cobhams Asuquo pamoja na rapa na mtunzi, Falz pia mwanamuziki Adekunle Gold ni kati ya watakaotumbuiza na tayari wamekuwa gumzo kubwa.


Hivi karibuni, Asuquo aliachia video yake ya Wimbo wa 'One Hit’ na ukawekwa rekodi ya kutazamwa kwa haraka na watu wengi zaidi mtandaoni hali iliyozidi kupandisha umaarufu wake kwa Nigeria na Afrika kwa jumla.


Falz maarufu kama The Bad Guy, yeye anajulikana zaidi kwa nyimbo zinazohusu mapenzi lakini mwenye pumzi ya kutosha wakati akipiga shoo jukwaani.


Pamoja na hao, imeelezwa watakuwepo wengine wengi. Katika shoo ya mara ya mwisho, Mtanzania, Ally Saleh Kiba alikuwa kati ya wale waliotumbuiza jukwaani na ikawa baraka Watanzania wawili wakaibuka na ushindi wa tuzo.


Pamoja na burudani zinazojulikana kama za vijana au zinazopendwa na wengi, mara nyingi AMVCA hutoa nafasi kwa vikundi vya kitamaduni kutumbuiza katika tamasha hilo kubwa zaidi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic