October 4, 2018


Timbwili kama loteee! Ndivyo walivyosikika wakisema baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Buguruni jijini Dar baada ya kushuhudia vijana wawili ambao majina yao hayakufahamika mara moja wakichapana makonde kisa kikitajwa ni shilingi 200 tu.

Tukio hilo lililotokea juzi majira ya mchana lilishuhudiwa na mapaparazi ambao waliwaona vijana hao wakirushiana ngumi ‘si za nchi hii’ kana kwamba walikuwa wameahidiwa kuwa mbabe atajipatia kitita cha shilingi milioni 1.

Baada ya kuona varangati hilo lilikuwa likileta usumbufu kwa wateja huku bidhaa mbalimbali zikikanyangwa na kusambaratishwa, baadhi ya wasamaria wema waliingilia kati na kuwaamulia bila mafanikio ambapo mmoja alikuwa amempiga mwenzake kabari na mwingine kamshika mwenzake sehemu za siri.

Hata hivyo, ilitumika nguvu kubwa ya kuwaachanisha baada ya kutokea jamaa mmoja ‘mbavu nene’ na wenzake wawili ambao walitumia ubaunsa wao kuwatenganisha huku wote wakiwa nyang’any’anya. Akisimulia chanzo cha timbwili hilo, mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Hamza alisema kuwa, vijana hao walianza kutupiana maneno makali kisa kikiwa ni 200 tu.

“Hili ni tukio la kushangaza sana, hawa vijana wanafanya biashara ya kuuza mifuko sasa kuna muda mmoja wa wateja aliita akionesha anataka auziwe mfuko laini ule wa 200. “Mmoja akawa amewahi pale, si unajua mambo ya kuchangamkia biashara? Basi yule mwingine alipofika na kukuta mwenzake kashauza, ndipo alipoanza kumsemea mbovu mwenzake.

“Wakaanza kuchimbana mkwara palee, mmoja akarusha ngumi, mwenzake akaikwepa, naye akarusha, ikampata ya jicho na hapo ndipo walipoanza kuoneshana umwamba, yaani hakuna aliyeweza kuamini kwamba timbwili lote lile kisa ni 200 tu,” alisema shuhuda huyo.

MWINGINE ADAKIA

Kijana mwingine aliyekuwa eneo hilo wakati mwenzake akimalizia kusimulia kisa na mkasa wa tukio hilo, alidakia na kusema:
“Wale inavyoonekana walikuwa wamezinguana tangu asubuhi, ni kama walikuwa wanawindana. Utoto nao unawasumbua, wee 200 tu ndo utake kumtoa roho mwenzako! Ndiyo maana tulikuwa tunawaangalia tu kwanza waoneshane umwamba.”

AMANI LAMVAA MMOJA
Katika kujua kama kuna kilicho nyuma ya pazia ya timbwili hilo, paparazi wetu alimfuata mmoja wa vijana hao waliokuwa wakipigana aliyejitambulisha kwa jina  Rajabu Juma ambaye alisema kuwa, yeye huwa si mtu wa kupenda ugomvi lakini ilibidi kutokana na maneno machafu aliyoambiwa na mwenzake huyo.

‘’Mimi nilikuwa namuuzia mteja wangu mfuko lakini yeye alikuja kuniharibia biashara ndiyo sababu iliyotupelekea kupigana na kusababisha kunichania mifuko yangu baadhi ambayo nilitakiwa kuuza,’’ alisema Rajabu. Wakati mapaparazi wetu wanaondoka eneo la tukio, ilidaiwa kuwa mmoja wa vijana hao alikuwa amechukua njia kuelekea kituo cha polisi kilicho karibu na soko hilo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic