Baada ya Simba kuamua kuachana na Kocha Masoud Djuma, mwenyewe Amefunguka huku akisisitiza asingependa kuzungumza maneno mengi, lakini alipoulizwa suala la yeye kuhusishwa na Yanga alisema kwa mshangao mkubwa: “Naenda Yanga mimi!”
Djuma raia wa Burundi, mkataba wake umesitishwa na klabu ya Simba, ingawa mambo yamekuwa ni ya siri sana lakini imeelezwa hakuwa na maelewano na Kocha Mkuu, Patrick Aussems.
Kocha huyo ambaye si mpenda makuu, ameliambia Championi bado yuko jijini Dar es Salaam na angependa kuaga kabla ya kuondoka lakini akalizungumzia suala la kwamba anahusishwa kwenda kuifundisha Yanga huku akionyesha kushangazwa nalo.
“Sipendi kuzungumza mambo mengine hapa, nisije nikazungumza jambo likatafsiriwa tofauti. Lakini bado nipo Dar es Salaam, nikitaka kuondoka nitaaga maana sijaiba wala sina ugomvi na mtu,” alisema Djuma akionyesha kuwa mtulivu.
Alipoulizwa kuhusiana na kuhusishwa na suala la kutua na kuinoa Yanga, Djuma alisema: “Naenda Yanga mimi! Sijui mnatoa wapi mambo ya Yanga, mimi najua Yanga ina kocha wake, wako wasaidizi wake. Sasa mimi naenda vipi Yanga, kukaa wapi pale.
“Unajua kama unamuachamke, kesho unaoa mwingine maana yake ulikuwa naye. Nafikiri unanielewa ninamaanisha nini. “Kama nitaenda Yanga leo, maana yake nilikuwa nina ukaribu nao. Kwa kweli hilo halipo,” aliongeza taratibu.
Hata alipoulizwa amepanga kuaga siku gani, kama ni siku ya mechi au siku maalum, Djuma alisema: “Nafikiri masuala ya Simba kama nilivyokuambia, nisingependa kuyazungumzia. Sipendi tena kuonekana nimesema jambo litakalopokelewa tofauti.”
Alipoulizwa suala la timu anayokwenda baada ya Simba kuamua kuachana naye. Djuma amesisitiza suala la kumuamini Mwenyezi Mungu. “Mungu ndiye anayepanga riziki ndugu yangu, siku ikifika tutajua maana yeye ndiye mkuu wetu sote.”
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Rayon Sports ya Rwanda kwa mafanikio makubwa, amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba. Wengi wameonyesha kutofurahishwa na kuondoka kwa Djuma ambaye kabla alikuwa chini ya Mfaransa, Pierre Lechatre.
Championi ndiyo lilikuwa gazeti la kwanza kuandika habari ya Djuma kuachana na Simba kwa kuwa ilielezwa hawezi kufanya kazi na Patrick Aussems huku akionekana kuchochea wachezaji kufanya vibaya ili bosi wake huyo afukuzwe na yeye awe kocha mkuu.
Habari hiyo ya Championi toleo la Jumatatu ya Agosti 27, 2018 ilizua mjadala mkubwa lakini mwisho wa siku kile ambacho gazeti hili lilikiandika, kimejithibitisha. Djuma sasa anasubiria alipwe chake asepe kwa amani, baada ya Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ kukiri kwamba wameshindwa kuwapatanisha na Aussems.
Djuma aliwahi kuwa kocha mkuu katika mechi tatu tu za ligi kuu Msimbazi kwa takriban mwezi mmoja kati ya Desemba 30 na Januari 27, ambazo zote alishinda dhidi ya Ndanda, Singida na Kagera. Pia aliiongoza Simba kwenye mechi 4 za Kombe la Mapinduzi.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment