DUH!! KAKOLANYA AWASHTUA VIONGOZI YANGA
Kipa namba moja wa Yanga msimu huu, Beno Kakolanya amewashtua baadhi ya viongozi wa timu hiyo ikiwa ni siku chache tu zimepita baada ya kuibania Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wamekumbwa na mshtuko huo kutokana na kitendo chake cha kuamua kuweka wazi mipango yake aliyokuwa nayo hapo awali ambapo uongozi wa klabu hiyo ulikuwa ukimchukulia poa na kumuona kama kipa wa kawaida asiyekuwa na msaada wowote ndani ya timu hiyo.
Kakolanya alisema kuwa baada ya mechi ya Simba alikutana na viongozi hao na kuwaambia mipango yake hiyo aliyokuwa nayo wakati walipokuwa wakimuona kipa wa kawaida.
Aliwaambia kuwa baada ya kuona mambo hayamwendei sawa, alikuwa katika harakati za kutaka kujiunga na JKT Tanzania ambayo ilionyesha nia ya kutaka kumsajili lakini wakala wake alimwambia atulie na asiwe na haraka ya kuondoka klabuni hapo.
Jambo hilo liliwashtua viongozi hao na kujikuta wakimwambia asahau hayo na kuendelea kuitumikia timu yake hiyo kwa moyo mmoja kama alivyofanya dhidi ya Simba lakini pia katika mechi nyingine zilizopita.
“Tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale ndipo nilipowagusia kuwa nilitaka kwenda JKT Tanzania na kama asingekuwa wakala wangu kunizuia ningeshaondoka, ndipo wote kwa pamoja walionekana kushtuka,” alisema Kakolanya.
Kabla ya mechi ya jana, Kakolanya alikuwa ameshaitumikia timu hiyo katika mechi tatu za ligi kuu, mbili kati ya hizo ilipata ushindi na moja ilipata sare, lakini pia ameweza kuruhusu bao moja tu golini kwake.
0 COMMENTS:
Post a Comment