October 31, 2018



Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI Emmanuel Okwi wa Simba, tayari amepachika mabao saba katika mechi 10 ambazo Simba wamecheza katika Ligi Kuu Bara.


Katika mechi hizo, Okwi amecheza mechi nane kwa kuwa moja alikuwa benchi na moja hakucheza kabisa.


Simba ndio mabingwa watetezi katika ubingwa ambao yeye alitoa mchango mkubwa akimaliza ligi katika nafasi ya mfungaji bora.


Okwi huyu ndiye yule ambaye Simba imewahi kuingiza fedha nyingi kupitia yeye mara mbili, mara ya kwanza ikiingiza dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 680) Simba ilipomuuza katika Klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia na baadaye dola 105,000 (zaidi ya Sh milioni 240), kwenda katika Klabu ya Sonderjyske FF ya nchini Denmark.


Mchezaji huyu mmoja, amekwenda na kurejea Simba mara mbili na kila aliporudi ameonyesha kweli yeye ni muhimu na ana msaada mkubwa.


Okwi amekuwa mchezaji ambaye anabandikwa maneno mengi ya kishabiki. Mfano aliporejea mara ya pili, wengi wakambandika jina la "mzee". Lakini pamoja na yote, yeye ndiye alikuwa chachu ya Simba hatimaye kurejesha ubingwa akishirikiana na kikosi kizima kwa ukaribu na umoja wa hali ya juu.


Simba ilikuwa na hamu kuu ya kuona ubingwa unarejea. Kikosi bora cha Simba ni wakati Okwi akiwa Tanzania, wakifanikiwa pia kuweka rekodi ya kuitesa Yanga kwa kuifunga mabao 5-0. Wakati mwingine hata Yanga walifaidika kumnunua kabla ya yeye kuamua kurejea Simba ambao walifanikiwa kumuuza Sweden.


Biashara ya Simba na Okwi imekuwa ni nipe nikupe, upate nipate na yote yamekuwa yakifanikiwa.


Leo, Uganda inakaribia kufuzu Afcon mwakani huko Cameroon. Okwi anayetegemewa na Uganda anatokea nyumbani hapa Tanzania ambako ndiko anakocheza soka na sisi tunasema kiwango chetu ni duni.


Okwi anayecheza hapa ni tegemeo hapa nyumbani na nje. Sisi kwa nini tuwe na kiwango duni na kwa nini Okwi awe bora katika ligi yenye kiwango duni?
Tayari Okwi amefunga mabao 51 ya Ligi Kuu Bara katika nenda rudi yake katika soka hapa nchini. Kati ya hayo, inaonekana 49 amefunga akiwa Simba na mawili alipoichezea Yanga kwa kipindi kifupi.


Idadi hiyo ya mabao 51 inazidi kunifikirisha kama kweli ukiachana na John Bocco, hakuna mchezaji mwingine anaweza kuwa na uwezo wa kufunga kama Okwi!


Okwi huyu ndiye ananifanya nianze kujiuliza maswali mengi kuhusiana na Jerry Tegete, kwamba kakimbilia wapi, yuko wapi na kwa nini kapotea?



Nani aliyemmaliza? Jerry kaonewa au kajionea mwenyewe? Wako wapi washambulizi wengine Watanzania ambao tuliamini wangekuwa hatari baada ya muda na sasa hawapo tena baada ya kutamba misimu mitatu tu?
Kwa nini Okwi yeye anaweza kuendelea kutamba tu kwa zaidi ya misimu saba sasa? Okwi anazidi kuwa zaidi ya wa zamani na utamu wake kikazi unaendelea kupanda.


Hata zile juhudi za mashabiki wa Kitanzania "kuwazeesha" wachezaji kadhaa wa Kitanzania ambao waliwaua kisaikolojia imeshindikana kwa Okwi. Maana pamoja na kumbandika, yeye ameendelea kuchapa kazi na anafanikiwa.


Mko wapi nyie, mimi ninahoji kuhusiana na Okwi, najifikirisha na mawazo yangu yanakuwa kwa sauti ya juu kabisa. Wewe kama mchezaji, umewahi kujiuliza kuhusiana na Okwi ambaye tunasema ni mzee lakini anatusua na kupasua na mafanikio yanaonekana!


Kiwango chake kilekile au zaidi ya kile. Maana tokea wakati huo anaitwa hatari, leo hii na inawezekana kesho tunaendelea kumuita hatari. Sasa vipi hatari wa Kitanzania, hawana hata misimu minne, walishapotea na sasa hata kwenye biashara ya mpira wamebaki katika mabonanza?
Ukitaka kujifunza kama wewe ni mdau wa soka, uwe shabiki au mtaalamu, basi ondoa suala la mapenzi, utajifunza mengi sana.


Kwanza, ni namna Okwi alivyoweza kutengeneza fedha hapa Tanzania. Mnapaswa kumuonea wivu, lakini uwe wivu wa maendeleo kwamba anawezaje na nyie mfanyeje?
Msimuonee wivu wa ‘kimbwiga’, muanze kumsema, kumsengenya, kuamini alienda kwa sangoma na kadhalika. Badala yake muigeni, jifunzeni na muone mlipopungukiwa.


Ligi yetu si duni, si laini kama mnavyofikiri, ndio maana inatoa mchezaji tegemeo katika taifa lake na anategemewa kuivusha nchi yake kwenda kucheza Kombe la Mataifa Afrika. Pia mjue kama Okwi anaweza na anatokea ukanda wetu wa Afrika Mashariki, basi Tanzania kuna wengi wa namna hiyo lakini wameshindwa kujitambua na wanapaswa kujifunza kwake.


Kujifunza hakuna aibu, kama utaona aibu za bila sababu, utaendelea kubaki ulipo. Ninaamini wengi ambao hawajawahi kufikirishwa na Okwi hasa wachezaji, bado wapo walipo kwa kuwa pia hawajawahi kutafakari kuwa kwa nini bado wapo hapo walipo.











0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic