October 12, 2018







NA SALEH ALLY
NAJUA hatupendi kuambiana ukweli, kila mmoja hata mimi napenda kusifiwa lakini ukweli unajenga zaidi ya sifa.


Wakati mwingine ni vizuri kuusikiliza ukweli unaoumiza kwa nia ya kujenga. Nimepangilia mjadala kwa lengo la kuwaeleza ukweli makocha wazalendo.

Wazalendo ni makocha Watanzania wenzetu. Tunaweza kutofautiana lakini hatuwezi kupinga kuhusiana na Utanzania wetu na nchi yetu Tanzania.

Nyumbani kwetu ni hapa, kama tutaambiana ukweli kwa nia njema ya kurekebisha na kujenga. Basi tunaweza kufanya mambo mazuri yenye faida hata hadi kwa vizazi vyetu vijavyo.


Makocha wengi wazalendo nimekuwa nikiwaasa kufunga safari na kwenda kufanya kazi nje ya nchi yetu. Angalau hata nchi jirani za Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na DR Congo.

Maana makocha wa nchi hizo nilizozitaja, wengi wamejitokeza na kufanya kazi hapa nchini. Jiulize hadi makocha kutoka Rwanda na Burundi wanaona wanaweza kufundisha Tanzania. Vipi wa hapa nyumbani wawe waoga? Si sahihi.

Hili nimelisema mara nyingi, hapa nilikuwa nakumbushia tu. Kikubwa ninachotaka kuzungumzia ni kuhusiana na beki wa Azam FC, David Mwantika.


Mara kadhaa nimekuwa nikimfuatilia sana kutokana na uwezo wake. Ingawa kuna wakati aliwahi kupata majeraha na kukaa nje kwa muda mrefu, aliporejea ubora wake uliendelea kubaki juu.


Mwantika amekuwa tegemeo Azam FC na mara chache Taifa Stars hasa inapokuwa na makocha wa kigeni. Kama watakuwa ni wazalendo, amebahatika kuitwa mara chache sana.

Hata alipoitwa hakuwa akipewa nafasi mara kwa mara lakini makocha wa kigeni karibu wote ambao walimkuta Mwantika akiwa fiti walimpa nafasi.

Kuanzia Azam FC, kwa makocha wageni, Mwantika amekuwa akipata nafasi ya kutosha kucheza. Hali kadhalika, katika timu ya taifa, hilo limekuwa likiendelea.


Mfano mzuri unaoweza kukumbusha ni sasa. Baada ya Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kutua nchini, Mwantika amekuwa lulu na kocha huyo anamuona yuko vizuri na baada ya kupewa nafasi na yeye anacheza vizuri na sasa ni tegemeo.

Usisahau Amunike amecheza klabu kubwa kadhaa za Ulaya ikiwemo FC Barcelona ya Hispania. Naye ameona Mwantika kuwa anafaa na aina ya mabeki bora wa kati. 


Vipi nafasi hiyo imekuwa ngumu kwa makocha wetu wazalendo. Hata kama wamewahi kumpa nafasi, takwimu zinaonyesha si sawa na wageni ambao wanamuamini zaidi.


Ajabu wanapokuja kutoka nje wamekuwa wakiona Mwantika ana kitu. Tuamini wazalendo hawajui au wamekuwa wanafanya mambo kwa mazoea kwa kuamini aliye Simba au Yanga ndio anaweza kuwa mchezaji au beki bora zaidi?


Kuna jambo la kujifunza hapa kwa kila ambaye aliamua kwa hisia kuhusiana na Mwantika kuwa vipimo vya beki bora vinabaki kuwa vipimo vya kiufundi na si timu anayotokea.



Inawezekana nafasi kwa Mwantika inakuwa si kubwa kwa kuwa hatokei Yanga au Simba. Inaweza kuwa kwa mazoea au hisia zenye mazoea pia.


Ukipata nafasi ya kumuangalia Mwantika akiwa kazini, utakubali ni beki hasa na mtu makini sana. Inawezekana mara moja mbili anaweza kukosea, yeye ni mwanadamu na kucheza soka ni lazima.


Yote hayo sawa lakini lazima tukubali, beki huyo ni kati ya wale tulionao bora maana ana nguvu, ana uwezo mkubwa wa kuruka vichwa, mzuri kwenye kuwahi matendo ya washambuliaji pia ana kasi huenda kuliko washambuliaji wengi sana.


Kama makocha karibu wote wazalendo walimuona hafai na kila wanapokuja wa nje wanaona anafaa. Basi kutakuwa na walakini kama nilivyoeleza hapo awali.


Vizuri pia tuwe tunawaamini wachezaji wetu baada ya kuamua mambo kitaalamu. Anayejua si lazima awe Yanga au Simba pekee.




3 COMMENTS:

  1. Nitofautiane na were kidog,kwann uandike makala hii baada ya kupewa nafas kwann hukuandika kabla?.Duuuh wachambuzi wa bongo in noma.Sikatai mwantika ni mchezaji mzuri lakini tufaham kitu kimoja kuwa kila kocha anakuja na mfumo wake swala LA mchezaji kuwa simba au Yanga si kweli kwani mchezaji kama Nyoni alikuwa azam na aliitwa sana taifa stars bila kuwa simba wala yanga.Nyoni bado ni mchezaji mzuri na Yuki simba na hajaitwa hivyo cha kujua ni mfumo wake kocha na aina ya wachezaji watakaofit mfumo wake.So kwamba wate walioitwa ni wazuri kuliko walioitwa bali ni kuwa mchezaji wa mchezaji unafit mfumo wa mwalimu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic