Kocha mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema kuwa ana imani na kikosi chake kutokana na kuwa katika ubora wake hivyo kama ni marekebisho atakayofanya kuelekea michezo ya kimataifa hayatakuwa ya kutisha.
Mtibwa ambao wamepangwa kucheza na timu ya Northen Dynnamo ya Shelisheli kati ya Novemba 27 na 28 Tanzania katika uwanja wa Chamazi, wamesema wapo vizuri kiushindani.
Katwila amesema wanatambua wana kazi kubwa ya kupeperusha bendera kimataifa hivyo ni muhimu kuweza kuimarisha kikosi hasa kwa wachezaji kuweza kuwa na mbinu mbadala.
"Kikosi kipo vizuri kwa kuwa wachezaji tulionao wanaweza kutupa matokeo tunayohitaji, kikubwa ni kuwaamini na kuangalia ni namna gani tunaweza kuboresha kikosi chetu hasa kwa kuwapa mbinu pamoja na kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
"Ushindani ni mkubwa ila nasi pia hatuna kikosi kibaya kwa kuwa tunapata matokeo mazuri kwenye ligi wachezaji wanajituma napenda vile ambavyo wanafanya kazi yao kwa umakini hivyo makubwa zaidi yanakuja hakuna haja ya kuwa na hofu, mashabiki watupe sapoti," alisema.
Mtibwa iliwahi kufungiwa kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kushindwa kusafiri kwenda Afrika Kusini kucheza mchezo wa marudiano na Santos ya Afrika Kusini lakini sasa wamerejea baada ya kumaliza adhabu yao .
0 COMMENTS:
Post a Comment