ZAHERA ATOKWA NA MACHOZI YANGA KISA HIKI
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo, amefunguka kuwa wachezaji wake ni wavumilivu na amekuwa akiwasikiliza kila mara mpaka machozi yanamtoka kutokana na matatizo waliyonayo licha ya kuwa mashabiki wamekuwa wakiwasema bila kujua wanapitia hali gani.
Yanga imekuwa ikipitia nyakati ngumu hasa kiuchumi tangu mwishoni mwa msimu uliopita hali ambayo inadaiwa ilichangia wao kutofanya vizuri ingawa msimu huu mpaka sasa imekuwa ikipambana kufanya vizuri chini ya Mkongo huyo.
Mkongo anayejulikana kwa ‘kutoumauma’ maneno, amesema anatamani kuona mashabiki wa timu hiyo wakitembelea mazoezi ya timu hiyo na kupata nafasi ya kuzungumza na wachezaji kujua nini kinawasumbua.
“Katika wachezaji ambao nimewahi kufanya nao kazi wachezaji wangu hawa wa Yanga ni wavumilivu sana, kuna wakati huwa nawasikiliza mpaka machozi yananitoka kutokana na matatizo ambayo yanawakabili.
“Lakini bado mashabiki hawahawa wamekuwa wakiwanyooshea vidole na kuwasema vibaya sababu hawajui wachezaji wanapitia vitu gani na ninaomba mashabiki wetu wa Yanga waje hata katika mazoezi ya timu wapate kuongea na wachezaji wao wajue nini kinawakabili.
“Sababu hawajui huenda wakaumia kwa kuwa walikuwa wananiambia kocha sisi tunaumizwa na matokeo ya wachezaji wetu lakini hawajui wachezaji wanapitia matatizo gani, wajaribu kuwasikiliza wachezaji labda na wao roho zitawauma.
“Wachezaji wanaendelea na magumu yao huku mashabiki nao wanasema waendelea kupambana na Tanzania mashabiki wa mpira ni wengi ila wanataka kuongozwa kwa miujiza ya Mungu jambo ambalo ni gumu,” alisema Zahera.
Zahera tangu aanze kukinoa kikosi hicho, msimu huu katika mechi 10 hajapoteza mchezo hata mmoja na amefanikiwa kutoa sare mechi mbili na timu ina pointi 26 sawa na Simba.
Hivi karibuni kocha huyo alinukuliwa kuwa yeye ataendelea kuifundisha Yanga bila kujali analipwa kiasi gani sababu maisha siyo fedha peke yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment