December 21, 2018


Hivi majuzi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao aliitisha mkutano wa waandishi wa habari kueleza mambo mbalimbali na mengine kutolewa ufafanuzi wake.

Lakini katika kikao hicho, Kidao alitumia muda mrefu kutisha vyombo vya habari vinavyoisema vibaya mamlaka hiyo ya soka Tanzania na akasema wataviandikia barua vyombo husika kuvionya.

Kidao, mtendaji wa TFF hakuna shaka huo ndiyo msimamo wa chombo hicho kinachosimamia mpira na hakuna shaka Rais wa TFF, Walace Karia ndiye kamtuma afikishe ujumbe huo kwa vyombo vya habari.

Nimwambie Karia kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida katika uendeshaji wa vyombo hivyo vya mpira, na ukosoaji ndiyo unasaidia kuwafanya mjipange upya na mjiangalie wapi mmeteleza.

Yapo mambo kwa dhamira nzuri kabisa TFF ya Karia imefanya na yanafaa kuwa pongezi kwao lakini yapo ambayo siyo mambo mazuri yanafanyika ndani ya TFF sasa kwa nini yasisemwe?

Karia amezungukwa na watu ambao ama wanampotosha bila yeye kujua au inawezekana yeye anajua na kawaachia wafanye wanavyotaka.

Kidao alijaribu kutoa ufafanuzi kuwa eti siyo Mtibwa Sugar tu wanaodai fedha za ubingwa wa Kombe la FA pekee yao, hata Simba wakati ule walivyotwaa kombe hilo hawajalipwa mpaka leo. Hivi haya maneno unaweza kusema mtendaji namna hii? Maana unahalalisha walichofanyiwa Mtibwa Sugar?

Sasa kuna haja gani ya kushiriki kombe hilo kama zawadi zake hazitoki? Ndivyo mlivyokubaliana na wadhamini? Mbona hayo ya Simba hatujawahi kusikia wakilalamika kuwa walitwaa ubingwa wa michuano hiyo ya Azam na zawadi yao hawajapata?

Wadhamini Azam Media walishawahi kuhojiwa kuhusu fedha za Mtibwa na kusema wao walishawapa TFF sasa je, wametudanganya? Kidao hizi ni zama za kusema ukweli na siyo kudanganya maana watu wana uelewa mkubwa, hawadanganyiki kirahisi.

Bado tunahoji ziko wapi fedha za ubingwa za Mtibwa Sugar? Maana taarifa zilizopo ni kuwa fedha hizo mlizitumia kwa masuala mengine huku mkiwaahidi Mtibwa kuwa mtawapa, hali ya kifedha itakapokuwa nzuri TFF.

Sasa leo unatuletea habari za Simba nao hawakupewa? Siye tunataka kujua za Mtibwa Sugar kwanza ziko wapi?

Yako mengine pia yanaendelea ndani ya TFF kuhusu matumizi mabaya kama siyo ubadhirifu ndani ya TFF, je, nayo tusiseme? Kwa hiyo tukisema ndiyo mtishe watu kuwa mtaandika barua katika vyombo vyao? Kubalini kukosolewa.

Mje na majibu sahihi mnapoitisha mikutano na waandishi wa habari na siyo kwenda kuwatisha wasiwe wanasema yale yaliyopo ndani ya TFF.

Hizi ni zama za uwazi, kila kitu kinachokwenda tofauti ni lazima tuwakumbushe kama siyo kwa njia ya kawaida basi kalamu ya mwandishi itatumika kuwakumbusha.

Nanyi mnapaswa kusikiliza au kujibu hoja kwa mtiririko mzuri pale mnapoona kalamu iliteleza basi semeni kuwa jambo fulani mwandishi alikosea lipo hivi na vile.

Hutakiwi kumtisha mtu anayekusaidia kukuambia pindi unapokwenda kinyume, ifikie wakati kusiwe na kuogopana bali kila mmoja apongeze panapostahili na pale anapokosea akumbushwe.

TFF msiogope pindi mnapoambiwa ukweli, mlichaguliwa hadharani kwa hiyo mnapokosea kubalini kuambiwa hadharani, msiwatishe watu wanaowaambieni ukweli kwani kuna msemo unasema ‘mficha uchi hazai’.

Lazima kila mmoja afanye kazi kwa umakini mkubwa.

1 COMMENTS:

  1. hao tff hawajajifunza kwa fifa iliyoondoolewa ya Sep Blater kama fedha za mtibwa zilitolewa walipwe sio kuleta vitisho visivyo na kichwa wala miguu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic