December 21, 2018






NA SALEH ALLY
DUNIA tunayoishi sasa, mambo yamebadilika sana. Hauwezi kufananisha angalau miaka mitano tu iliyopita.

Mambo yanakwenda haraka na mipango mingi imekuwa inajumuisha utaalamu sana kuliko yale mambo ya “kiimla” ambayo watu wamekuwa wakifanya siku nyingi zilizopita.

Kipindi hiki unapaswa kuwa mbunifu sana ili mambo yaende vizuri katika mpangilio ambao ni sahihi au mafanikio ambayo yanatakiwa.

Binafsi nitajikita katika suala la viwanja. Nikimaanisha viwanja maalum kwa ajili ya kufanya mazoezi na kucheza mechi.

Kuna ule msemo, hauwezi kujenga nyumba bila ya kuwa na kiwanja. Sote tunakubaliana kwamba kama hauna kiwanja, utajenga nyumba yako wapi?


Hata kama utakuwa na mamilioni ya fedha, unahitaji kuwa na sehemu kwa ajili ya kujenga nyumba ambayo ni kiwanja.
Klabu kubwa na maarufu nchini za Yanga na Simba, tayari zina viwanja ambavyo zinaweza kujenga sehemu maalum itakayotumika kama uwanja wa soka.

Simba wanamiliki uwanja eneo la Bunju nje ya Jiji la Dar es Salaam na watani wao Yanga, pia wana uwanja wao ambao ni mkongwe na umewahi kutumika kama sehemu maalum ya kuchezea soka. Huu ni Uwanja wa Kaunda, ulio katikati ya jiji pale Jangwani jijini Dar es Saaam.

Sasa jiulize, Yanga na Simba wataendelea hadi lini kuwa wanalipa Sh hadi 300,000 kwa ajili ya bajeti ya kutumia uwanja kwa ajili ya mazoezi? Maana yake kwa mwezi wanaweza kulipa hadi Sh 3,000,000 kwa ajili ya mazoezi tu.

Angalia timu za vijana za Yanga na Simba, zinawezaje kupiga hatua katika suala la ukuzaji wa vijana bila ya kuwa na sehemu maalum kwa ajili ya kukuzia vipaji na vipaji vinakuzwa kwenye viwanja vya soka?

Hii imekuwa ni aibu ambayo inaendelea miaka nenda rudi na viongozi wote wa Yanga na Simba wanapaswa kuona aibu. Hii si sahihi na inawezekana inaonekana ni poa tu kwa kuwa mashabiki hawapigi kelele kwa kuwa hata wao hawalioni kama ni baya kwao.

Mashabiki wa soka wa Tanzania, wanachojali wao ni timu yao kushinda tu, haya ndiyo maendeleo. Viongozi nao wamejikita huku wakiona kwamba ni sahihi kupata ushindi bila ya kuwa na lolote la maana au kukuza thamani ya klabu kwa ajili ya miaka mingine mitano, kumi au mia ijayo.

Hakuna mipango madhubuti kwa ajili ya kuthibitisha ukubwa wa klabu zenyewe ambazo zimebaki zinalindwa na historia pekee. Baada ya pale zinabaki kuendelea bila ya kuwa na lolote.

Sote tunakubaliana uwanja kama watakuwa nao Simba au Yanga ni biashara. Ni zaidi ya biashara kwa kuwa pamoja na kutumia wao, wanaweza wengine kutumia na wao kuingiza fedha.

Inawezekana kwa mazoezi au mechi nyingine. Lakini pia kwa watu wengine kuingia na kuweka matangazo yao ambayo yatakuwa yanaingiza fedha katika klabu. Hili linawezekana na sote tunatambua.

Sasa vipi suala la kumiliki uwanja limeendelea kuwa kizungumkuti kwa Yanga na Simba kwa miaka yote hii na kwa nini hakuna mpango sahihi na bora unaostahili kufanyika ili kufanikisha hili?

Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza ni siasa? Maana hata pale inapoonekana suala linakaribia kupata mwafaka, kunaingia vipingamizi vingi sana. Nakuwa naona kama kuna watu wanaofaidika na Simba au Yanga kutokuwa na viwanja vyao.

Inaonekana kama ndani ya viongozi kuna mradi. Maana inashindikana vipi kutumia wawekezaji au makampuni ambayo yako tayari kujenga uwanja hata majukwaa mawili nayo yakawekeza na kuingiza fedha na baadaye potelea mbali hata wakiwa Simba au Yanga wanachukua asilimia 30 tu hadi watajapomaliza deni.

Huu ni mfano lakini kuna njia nyingi za kufanya hivi kujaribuni kupata wabia na kuzisaidia hizi klabu, jambo ambalo halijawahi kufanyika na hatujaelezwa haliwezekani. Mtakwenda hivi kwa kuunga hadi lini? Badilikeni.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic