Na Saleh Ally
NAMNA mambo yalivyo unaweza kusema England wana nafasi kubwa ya kurejesha ufalme wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao ulikuwa kipindi cha Manchester United.
Wakati Manchester United ikitamba na kufanikiwa kuubeba ubingwa mwaka 2008, tena kwa timu mbili za Man United na Chelsea kuingia fainali, kilikuwa kipindi kilichotawaliwa na England.
Hata baada ya hapo, Chelsea ikafanya vema na utaona ilifikia hadi timu nne za nusu fainali, mbili au tatu lazima zitokee England.
Ilionekana ni kama ‘vita’ ya England na Hispania huku Bayern Munich kutokea katika Bundesliga ikionekana kutia mguu mara mojamoja.
Kadiri siku zinavyokwenda, England ilizidi kuporomoka hasa baada ya kuanza kuamka kwa Italia na hasa upande wa Juventus na utaona misimu miwili iliyopita, Ufaransa wamekuwa wakipiga hatua na PSG ambayo imejiimarisha kwa wachezaji wengi ambao wana kariba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu huu, katika timu 16 zilizoingia hatua hiyo ya mtoano baada ya makundi, unaona England inaongoza kwa kuwa na timu nne ikifuatiwa na Ujerumani na Hispania halafu Italia na Ufaransa, kila moja ina timu mbili huku Ureno na Uholanzi kila moja ikiwa na moja.
Maana yake England inaongoza na unaona ina nafasi kubwa ya kupeleka angalau timu tatu katika robo fainali ambayo itakuwa na timu nane.
Itategemea timu za England zitakutana na timu zipi katika hatua hiyo baada ya kupangwa kwa ratiba lakini suala la kudorora kwa Hispania kwa kiasi kikubwa, kunaipa nafasi England iinuke.
Ukisema washindwe wenyewe si vibaya kwa kuwa ukiangalia Hispania kupitia Barcelona, Real Madrid na Atletico Madrid, zimepoteza nguvu kwa kiasi kikubwa na hata ile kasi na muonekano wa bingwa bado umeshuka.
Angalau Barcelona wanaonekana wanaweza kufanya jambo lakini si ile Barcelona inayojulikana. Kwa upande wa Italia, Juventus ndiyo inaonekana yenye nguvu lakini si AS Roma. Hata kama si ya kuibeza lakini haiwezi kuwa tishio kupita kiasi.
Kwa maana ya uimara wa timu zao kwa kipindi hiki, uzoefu au ubora wa makocha walionao na michuano hiyo lakini hata kiwango cha wachezaji wengi, unaona bado nafasi ipo kwa England.
MAN CITY:
Roma, Atletico Madrid, Schalke, Ajax
Ukiangalia katika mfumo wa upangaji, unaona ina nafasi ya kukutana na timu hizo nne na nafasi inakuwa ni kubwa kwa Man City ambao ni vinara wa Ligi Kuu England kufanya vema.
Nguvu ya Man City imekuwa juu ingawa wanabanwa na majeruhi wengi lakini ni timu inayoweza kutinga robo fainali kama kweli itakutana na kati ya timu hizo.
MAN UNITED:
Barcelona, Dortmund, Porto, Real Madrid, Bayern
Haiaminiki katakana na mwendo wake katika Ligi Kuu England. Kocha wake, Jose Mourinho anajulikana kwa kushinda mechi ngumu lakini pia uzoefu wake katika Ligi ya Mabingwa Ulaya unaweza kuwa chachu kama watakutana na moja ya timu hizi ambazo pia zina uzoefu na ngumu.
LIVERPOOL FC:
Barcelona, Dortmund, Porto, Real Madrid, Bayern, Juve
Baada ya kuvuka kwa ugumu, Liverpool wana nafasi ya kufanya zaidi na ukiangalia vizuri, wana nafasi ya kumpunguza mmoja kati ya vigogo ambavyo kama watakutana navyo.
Msimu uliopita waliingia fainali, utaona kikosi chao kilivyo bado wana nafasi ya kufanya vema katika mtoano kwa kuwa wanafunga mabao mengi na hilo ni muhimu katika hatua za mtoano.
TOTTENHAM:
Bayern, PSG, Dortmund, Porto, Real Madrid, Juve
Katika mechi hatua ya makundi walikuwa na Barcelona na wameweza kutoa sare mechi ya mwisho wakiwa Camp Nou na imewavusha hadi 16 Bora. Nani kati ya unaowaona anaweza akawa kipingamizi kwao. Nafasi ipo na katika timu hizo sita kama mmoja wao watakutana naye ile 50-50 inawezekana kabisa.
Hii inaweka nafasi ya England angalau kufikisha timu tatu katika Hatua ya 8 Bora, ikiwezekana timu 2 katika 4 Bora na kujiweka katika nafasi nzuri ya fainali hasa kama timu hizo za England zitafanikiwa kuendelea bila ya kukutana hadi mwisho labda fainali.
NCHI NA TIMU ZILIZOPITISHA
England: 4
Man City, Man United, Tottenham na Liverpool
Ujerumani: 3
Bayern, Dortmund na Schalke 04
Hispania: 3
Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid
Italia: 2
Juventus na AS Roma
Ufaransa: 2
PSG na Lyon
Ureno: 1
FC Porto
Uholanzi: 1
Ajax
0 COMMENTS:
Post a Comment