Serengeti Lite wameinogesha Ligi Kuu ya Wanawake ambayo msimu huu imekuwa na mengi ya kuvutia. JKT Queens ndiye bingwa mtetezi wa ligi hiyo, anazidi kuonyesha kuwa alistahili kuwa bingwa kutokana na uwezo mkubwa alionyesha mpaka hivi sasa miongoni mwa timu zote 12 zinazoshiriki.
Imecheza michezo nane na kushinda yote,ina pointi 24. Imeweka rekodi ya kushinda mabao 16-0 kwenye mchezo mmoja.
Nyuma ya mafanikio hayo yupo Straika wao tegemeo Fatuma Mustapha ambaye mpaka sasa ameshatumbukia kambani mara 17.
Ikumbukwe msimu uliopita Fatuma aliibuka mfungaji bora wa ligi hiyo baada ya kufunga mabao 18.
Amebakiza bao moja pekee ili kufikia rekodi yake ya mwaka jana na endapo atafanikiwa kufunga bao kwenye mchezo wa leo dhidi ya Marsh Quuens ya Mwanza,atakuwa amevunja rekodi yake na kuanza safari ya kutengeneza ufalme mwingine kunako ligi hiyo.
Spoti Xtra limepata nafasi ya kuzungumza naye na hapa anaanza kufunguka mambo kadhaa.
“Kwa sasa nina miaka 22 na ninacheza ligi kuu ya wanawake zaidi ya msimu wa tatu,nimekuwa nikiinjoi zaidi kucheza mpira wa miguu kwa sababu ni moja ya vitu ambavyo navipenda sana.
NANI ALIKUSHAWISHI KUCHEZA SOKA?
“Hakuna aliyenishawishi kucheza soka ni kipaji tu ambacho mungu alinipa na ndiyo hivi tena mpaka leo nipo hapa.
KATIKA FAMILIA YENU WATU WANGAPI WANACHEZA SOKA?
“Kama wote hivi, isipokuwa dada yangu mkubwa yeye anacheza mchezo mwingine tofauti na mpira wa miguu, kwetu tumezaliwa watano wanne tu.
NANI ANAKUPA SAPOTI KWENYE MAISHA YAKO YA SOKA?
“Familia yangu ni watu wa kwanza ambao siku zote huwa wananipa moyo na kunisisitiza nipambanie kile ambacho nakiamini.
“Kitu kingine ni walimu wangu walionifundisha toka naanza soka la utotoni mpaka hapa nilipofikia leo ni watu ambao wamenisaidia kwa kiasi kikubwa.
ULIANZIA WAPI KUCHEZA SOKA?
“Nilianzia mtaani kwetu Urafiki Manzese,kwenye timu ya Future FC ambayo ipo mtaani kwetu kabisa,kisha nikajiunga na Sayari FC, Mburahati FC na leo nipo JKT Queens.
UMEFUNGA MABAO 17 KWENYE MECHI SITA NINI SIRI YA MAFANIKIO?
“Kujituma na kumsikiliza mwalimu pamoja na kuwa na ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzangu hicho ndiyo kitu kinachonipa mafanikio.
TIMU GANI NYINGINE AMBAYO UNATAMANI KUCHEZEA?
‘’Kwa hapa nyumbani hakuna kwa sababu muda siyo mrefu nitakuwa kamanda hivyo sidhani kama inaweza kuwa rahisi mimi kuchezea timu nyingine zaidi ya JKT Queens labda ije timu kutoka Ulaya naweza nikaangalia kama tunaweza kukubaliana.
MCHEZAJI GANI MWINGINE ANAKUPA CHANGAMOTO KWENYE LIGI YENU?
“Hakuna mchezaji ambaye ananipa changamoto kwa sababu mimi najiamini na nina uamini uwezo wangu.
CHANGAMOTO ZIPI MNAKUTANA NAZO KWENYE LIGI?
“Wadhamini ndiyo changamoto kubwa sana kwenye soka la wanawake, kwa sababu utakuta timu inakosa hadi chakula, wakati mwingine inapata ugumu wa kusafiri kwenda kucheza ugenini mfano nje ya mkoa na sehemu zingine ambazo inalazimika kusafiri.
KWANINI WACHEZAJI WENGI HUJIWEKA KAMA WANAUME?
“Muonekano tu na mtu anavyopendelea kuvaa,mbona kuna ambao wanacheza soka na wanavaa sketi mi nafikiri ni mtazamo tu wa watu.
VIPI KUHUSU KUWA NA MAHUSIANO YA JINSIA MOJA KWENYE TIMU ZA WANAWAKE?
“Siyo kweli nayo ni maneno tu ya watu, mimi binafsi yangu sijawahi kukutana na mambo kama hayo kwa muda wote niliocheza soka ila inawezekana yakawepo kwa jamii nyingine tofauti na hii ambayo naishi mimi.
UNATAMANI KUOLEWA?
“Ndiyo, lakini kwa mbeleni huko lazima nitakuwa na familia yangu pamoja na watoto ila siyo kwa sasa hivi muda bado wa kufanya hivyo.
UNABOYFRIEND?
“Ndiyo,tena ninao wengi tu!
MIPANGO YAKO MSIMU HUU IPOJE?
“Kuchukua tena ubingwa na kuwa mfungaji bora kwa mara ya pili mfululizo hayo diyo malengo ambayo nimejiwekea lakini kubwa zaidi nataka nifunge mabao mengi zaidi ya msimu uliopita na kujiwekea historia ambayo itakuwa ngumu kufikiwa na mtu yoyote.”
0 COMMENTS:
Post a Comment