February 19, 2019




HAINA shaka tena kwamba uhusiano kati ya kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil, na kocha wake, Unai Emery hauna afya nzuri!

Ozil, 30, alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha Arsenal chini ya Arsene Wenger, lakini sasa akiwa chini ya Emery hana nafasi hata ya kukaa benchi.

Emery amekuja na sheria mpya ya kutumia wachezaji wanaojituma pekee, na anaamini kwamba Ozil hachezi kwa kujituma, hakabi, lainilauni, kwa hiyo ni ngumu kupata nafasi.

Tangu kipindi cha ‘boxing day’, yaani Desemba 26, mwaka jana, Ozil ameanza kwenye mchezo mmoja tu, ingawa mara kadhaa ni kutokana na majeraha, mara nyingi ameachwa kutokana na sababu za kiufundi. 

Huyu ni mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi ya wachezaji wote wa Arsenal, akiwa anapokea mshahara wa pauni 350,000 (zaidi ya Sh bilioni moja) kwa wiki. 
  
Juzijuzi ilikuwa kituko, baada ya Emery kuamua kutosafiri kabisa na Ozil kwenda Belarus ambako Arsenal ilikutana na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa BATE Borisov kwenye Ligi ya Europa.

Gumzo kubwa baada ya mchezo huo, limekuwa ni Ozil kutosafiri kwa ajili ya mechi hiyo, yaani kutopata nafasi hata benchi. Je, ni kweli Ozil anastahili kukosa nafasi hata katika benchi la Arsenal?

Akizungumzia mjadala huo, nyota wa zamani wa Chelsea, Joe Cole, amesisitiza kuwa Emery anatakiwa aliweke pembeni suala la Ozil kutokukaba, badala yake aangalie ufundi uliobebwa na Mjerumani huyo.

"Hii sasa inakuwa kama komedi," anasema Cole. “Tunajua jinsi alivyo na kipaji.

"Kocha ameamua pengine hamtaki kwenye kikosi chake, haonyeshi juhudi za kutosha na kadhalika, lakini wakati mwingine mtu anapocheza kwa raha, baadhi ya wachezaji kwenye timu wataongeza juhudi maradufu ili kuruhusu awe na mpira halafu aonyeshe ubunifu wake.

"Arsenal kwa miaka iliyopita, wakati Wenger akiwepo walifanya hivyo. Unatakiwa kuwachezesha wachezaji wako bora unapowahitaji, na Ozil ni mmoja wa wachezaji bora wa Arsenal.

"Kama ukimuuliza Lacazette na Aubameyang: 'unataka Mesut acheze?' watasema ndiyo nyingi sana! Ni ajabu sana sana."

Naye kocha mkongwe, Neil Lennon, ameongelea mjadala huo na kufunguka kuwa inawezekana suala la Ozil kila mtu ana mawazo yake, lakini akasisitiza kwamba kama Arsenal ikitangaza kuwa inamuuza, klabu kubwa zitajitokeza kumnunua.

"Una mtu mwenye kipaji namna hiyo, kama humtumii, basi ni suala la namna unavyowaongoza wachezaji,” anasema kocha huyo wa zamani wa Celtic.

"Amekuwa ni mtu anayewagawa watu kwa miaka mingi, wengine wanampenda, wengine hawampendi! Kwangu mimi, napenda kumuona akicheza.

"Hukosolewa sana juu ya suala la kujituma, lakini takwimu zake zipo juu kuhusu anavyokimbia umbali mrefu uwanjani. Atapata timu mahali, kwa sababu uwezo anao.”

Kwa upande wake, beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown, amemshauri Ozil apambane ili kuendana na mfumo wa Emery, vinginevyo safari yake Arsenal itakuwa imefikia tamati.

Keown yeye hakubaliani na upambanaji wa Ozil uwanjani, na amemsisitiza ni lazima aongeze juhudi.

“Yeye ni majeruhi? Anaumwa? Moja ya vitu muhimu kwa mchezaji ni kwamba unapaswa kuwa tayari kwa ajili ya kuchaguliwa na kuonyesha mwendelezo wa ubora.

“Amekuwa akishindwa kuonyesha chochote kati ya hayo mawili ili arejee kwenye timu. Hicho ndicho anachotakiwa kufanya na ndicho kocha anataka akifanye. Sasa inakuwa ni kero.”

Sasa Ozil amekosekana kwenye mechi 100 kati ya 313 ambazo angeweza kucheza tangu atue Arsenal, suala ambalo linawachanganya mashabiki ambao wanajua jinsi anavyoweza kuwa bora kwenye siku yake.

Na Keown, amesisitiza siyo sahihi kukosa mechi nyingi namna hiyo.

“Kukosa mechi 100 inashangaza sana. Ninaweza kusema hilo ni suala la kuhoji lakini mchezaji ndiye anayejua kiukweli,” anasema Keown.

Ozil alijiunga na Arsenal kwa dau la pauni milioni 42.5 akitokea Real Madrid mwaka 2013 na hadi sasa amefunga mabao 30 ya Premier katika mechi 155 alizoichezea klabu hiyo.

Katika michuano yote, Ozil amefunga mabao 41 katika mechi 213 alizoichezea Arsenal tangu mwaka 2013.

Ozil anajulikana kwa ubora wake wa kupiga pasi za mabao (asisti).

Msimu mzuri zaidi kwa Ozil tangu awe Arsenal ni ule wa 2015-16 ambapo alikuwa mchezaji bora wa mwaka wa timu hiyo, na ndiye aliyekuwa na pasi za mabao (asisti) nyingi zaidi ya wachezaji wengine wote kwenye Premier.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic