ALLY Ally ni beki mzuri wa KMC licha ya kushindwa kuhimili mikimikiki ya Yanga anapaswa ajengwe kisaikolojia ili kubaki katika ubora wake, suala la kumlaumu kisa amejifunga naona sio sawa.
Nimeamua nizungumzie suala hili baada ya mijadala kuanza kumzungumzia beki huyu hasa baada ya kujifunga kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambao bao lake alilifunga wakati wa harakati za kuokoa mpira uliopigwa na nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu.
Uongozi wa KMC una falsafa yake ya kutunza wachezaji hasa chipukizi basi waendelee kumuamini na kumpa nafasi beki huyu ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri kwa sasa ikumbukwe kwamba sio mchezaji wa kwanza kujifunga.
Kwa upande wa waamuzi waache kupendelea timu kama ambavyo imekuwa ikielezwa na wengi kwamba wanashindwa kutafsiri sheria 17 hili sio sawa maumivu ni makubwa kila iitwapo leo hasa kwa timu zile ambazo zinahaha kujinasua kutoka chini kwa sasa.
Kinachotakiwa ni kwa kila timu kupambana kutafuta nafasi na kupata matokeo Uwanjani hakuna namna nyingine itakayowafanya wawe sehemu nzuri kwa sasa kwenye ligi kwani kila timu ina nafasi ya kupata matokeo.
Niwakumbushe kwamba tupo kwenye lala salama namaanisha mzunguko wa pili ambao iwe isiwe ni lazima mshindi apatikane na atakayeshuka daraja apatikane.
Bingwa anapatikana kupitia michezo ambayo inachezwa kwa sasa kwenye ligi hivyo kila timu inatakiwa ijitathimini nafasi iliyopo kwa sasa na michezo ambayo imebakiwa nayo mkononi ili kupata matokeo.
Hakuna ambaye anatambua juu ya kitakachotokea kesho ila mipango ya kesho ni lazima ianze kupangwa leo ili ujiandae sawasawa kwani kila timu imeshajua makosa yao inachotakiwa ni kuyafanyia kazi.
kushuka daraja si jambo jema ila haliepukiki sasa njia ya kushinda suala hili ni kupambana na kupata matokeo kwenye michezo iliyobaki na inayoendelea kwenye ligi.
Zile ambazo zinajiaandaa kupanda daraja zitazame namna ligi inavyokwenda kwa sasa ili wajipange sawasawa isije kuwa kichekesho baadaye baada ya kupanda na kurejea kule ambako walitoka.
Ushindani wa ligi kuu ni tofauti na ule wa ligi daraja la kwanza hivyo maandalizi yawe ya uhakika na sio ya kuungaunga hali hii itawapa taabu wakipanda daraja msimu ujao.
Ushindani pia huku Ligi Daraja la Kwanza nao unavutia hivyo niwakati wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwekea mtazamo mkubwa kwenye mashindano haya ambayo nayo yana changamoto zake pia.
Kwa upande wa wakilishi wetu kimataifa Simba, tunaona namna ambavyo wanapambana kutafuta nafasi ila matokeo wanayoyapata inaonekana si malengo yao kwa sasa hasa kwenye michezo ya ugenini.
Kwenye kundi D ghafla tu mambo yamebadilika Simba wameshushwa kutoka nafasi ya pili na kwa sasa wapo nafasi ya nne ikiwa namaana wanaburuza mkia kwenye kundi lao wakiwa na pointi sita tu walizovuna nyumbani.
Hali si shwari hasa kwa mashabiki na wachezaji kutokana na matokeo haya ila kikubwa wanachotakiwa ni kutokata tamaa na kuamini kwamba inawezekana kurejea kwenye ubora wao.
Ugenini kupata matokeo inawezekana ila namna ya kujipanga na kuamua kujitoa kwa kuwa tayari imeshatokea hakuna namna zaidi ya kuwapongeza kwa kupambana kwani tumeona namna mlivyofanikiwa kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa.
Ikumbukwe kuwa Simba ilikusanya jumla ya mabao 10 awali ugenini ambapo ilifungwa na AS Vita bao 5-0 na Al Ahly bao 5-0 ugenini ila kwa JS Saoura imefungwa mabao 2-0.
Nafasi yenu inabaki moja na kazi yenu kubwa ni kujipanga kupata matokeo mbele ya AS Vita mchezo wenu wa mwisho jumamosi ambao mtacheza Uwanja wa Taifa.
Mashabiki msikate tamaa mjitokeze kwa wingi Uwanja wa Taifa kuipa sapoti timu ya Simba. Kama sera inavyosema nguvu moja basi na iwe hivyo kwa wote kujitoa na kupambana kwa pamoja kuishangilia timu yenu.
Kwa kufanya hivyo kutawapa nguvu Simba kupambana na kutafuta matokeo Uwanjani hali itakayosaidia kukata tiketi ya kwenda moja kwa moja hatua ya robo fainali jambo ambalo linawezekana.
Kiushindani AS Vita si timu ya kubeza hapo ndipo maandalizi ya Simba yanatakiwa yaanze, wachezaji waandaliwe kisaikolojia na wawe na nidhamu kucheza na wapinzani wao kwani ikitokea wakajawa na kiburi hiyo inakuwa njia nyepesi kwa wapinzani wao kupenya.
Kufungwa, kufunga na sare haya ni matokeo ambayo ni lazima yatokee hasa timu zinapokuwa Uwanjani hakuna namna ya kuanza kutafutana uchawi kwa sasa zaidi ya kutafuta ushindi.
Benchi la ufundi linapaswa liangalie kwa ufudi makosa ya wachezaji wake hasa kuanzia beki pamoja na washambuliaji wao namna ya kujilinda na kutumia nafasi ambazo washambuliaji watazipata.
Endapo kila mchezaji atatitimiza majukumu yake uwanjani inakuwa rahisi kupata matoeko ila kama kila mmoja atacheza anavyojua yeye tutarajie maumivu, wakati ni huu sasa wa kutumia Uwanja wa nyumbani.
0 COMMENTS:
Post a Comment