TAMBWE: UBINGWA UNAENDA YANGA
MSHAMBULIAJI mkongwe wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amesikitishwa na matokeo mabaya waliyoyapata dhidi ya Lipuli FC ya Iringa huku akitamba bado wana nafasi ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Yanga Jumamosi iliyopita ilichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Lipuli katika mchezo wa ligi uliopigwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.
Katika mechi hiyo, bao pekee la Lipuli lilifungwa na Haruna Shamte kwa njia ya faulo iliyopatikana nje ya 18 baada ya kupigwa kiufundi na kumshinda kipa wa Yanga, Klaus Kindoki.
Tambwe alisema bado wana nafasi hiyo ya ubingwa, licha ya kufungwa na Lipuli kutokana na mikakati waliyoiweka.
“Tunafahamu ugumu wa michezo iliyobaki, hivyo tumejipanga kwa ajili ya michezo mingine inayofuata kuhakikisha hatupotezi ili tufikie malengo yetu.
“Kama wachezaji tumeumia baada ya matokeo haya tuliyoyapata ya Lipuli, hatukupenda lakini ndiyo matokeo, kikubwa tuwaombe radhi mashabiki wetu, kocha ameona upungufu wetu, tunajipanga kwa ajili ya michezo ijayo,” alisema Tambwe.
Lakini Yanga imejiweka katika mazingira magumu, kwani kama Simba ikishinda viporo vyake vyote itaiacha Yanga kwa pointi nane, na hata kama ikipoteza viwili, bado itakuwa juu ya vinara hao wa sasa.
Kawaulize Ruvu shooting kwanza waliochapwa na kikosi chapili cha mnyama
ReplyDelete