April 3, 2019


KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu, anasubiria kutambulishwa Simba, ni baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kuichezea timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.

Ajibu anajiunga na Simba msimu ujao wa ligi baada ya mkataba wake Yanga kumalizika mwishoni mwa msimu. Kiungo huyo anarejea Simba baada ya kuondoka mwaka 2017 na kusaini miaka miwili Jangwani.

Kiungo huyo aliyepiga asisti 15 hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara, anajiunga na Simba kutokana na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kumruhusu kufanya mazungumzo na kusaini mkataba wa awali, kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hilo, mchezaji akibakiza miezi sita, anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote.

Ajibu ambaye tangu ajiunge na Yanga amefunga jumla ya mabao 13 kwenye ligi katika kipindi cha misimu miwili, anatua kuichezea Simba baada ya mwekezaji bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ kumvuta akiamini kuwa ataiimarisha safu ya kiungo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata, Mo amemtengea Ajibu kitita cha shilingi milioni 150 ili kiungo huyo asaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Simba.

Taarifa ambazo limezipata gazeti hili na ambazo tulizidokeza wiki iliyopita, ni kuwa kiungo huyo tayari amesaini mkataba wa awali wa miaka miwili kwa siri, Simba, lakini suala hilo limefichwa sana huku kila upande ukitaka lisijulikane.

Katika kuthibitisha hilo, kiungo huyo inaonekana kama ameanza kuidengulia Yanga kwa kugomea kucheza baadhi za mechi za ligi na Kombe la Shirikisho la Azam Sports huku sababu akitaja ni maumivu ya nyonga. Mchezo wake wa kwanza kudaiwa kugoma kucheza wa ligi ni wakati timu hiyo ilipocheza dhidi ya Lipuli FC ya Iringa huko Samora ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.

Kiungo huyo inaelezwa aligoma dakika za mwisho kusafiri kwenda Iringa akiwa amefanya mazoezi kwa siku zote kwa asilimia 90.

Haikuishia hapo, kiungo huyo alijitoa tena kikosini katika mazoezi ya mwisho wakati timu inakwenda Mwanza kucheza na Alliance katika mchezo wa Kombe la Shirikisho. Ajibu alijitoa kikosini na kwenye msafara wa timu akitaja sababu ileile ya maumivu ya nyonga wakati kwa siku zote alifanya mazoezi vizuri.

Kwa maana hiyo, kiungo huyo ni rasmi anakwenda Simba, licha ya taarifa hiyo kufichwa kwa hofu ya Yanga kushtaki TFF na baadaye kupigwa faini kwa kumsainisha kimakosa akiwa ndani ya mkataba.

Jana taarifa zilisema kwamba kuna tajiri mmoja wa Yanga baada ya kusikia Ajibu anarudi Simba ameweka mezani Sh milioni 80 ili kumbaki
za, lakini huenda asifanikiwe.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, aliliambia gazeti hili kuwa: “Ruksa kwa Ajibu kwenda, sitaweza kumkataza au kumzuia mchezaji yeyote kuondoka Yanga akiwemo Ajibu ambaye nimepata taarifa za kusaini tayari Simba pamoja na wachezaji wengine.”

Ajibu alipotafutwa juzi na gazeti ndugu na hili, Spoti Xtra, linalotoka Alhamisi na Jumapili, hakuwa tayari kuweka wazi kwa undani, badala yake alisema: “Mimi ni mchezaji wa Yanga, na mkataba wangu bado haujaisha, utakapoisha ndiyo nitajua nitakwenda wapi lakini si sasa.”

Itakumbukwa kuwa wakati Ajibu akiondoka Simba miaka miwili iliyopita, aligoma kabisa kuwa hayupo kwenye mpango wa kuondoka hadi dakika ya mwisho alipotambulishwa rasmi kuwa ni mchezaji wa Yanga.

5 COMMENTS:

  1. sasa kama ni siri mbona wewe unaweka hadharani honi unachochea moto kwa mashabikiwa yanga kuanza kumchukulia ajibu kivingine?. subiri tu maaana bado kama mechi nane tu mbona ukweli utajulikana?

    ReplyDelete
  2. Yote mema, mpira ni kazi kama kazi zingine na kuhama kwa mchezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine ni kawaida lakini hii huwa ina faida na hasara kwa wote, anayehama, anakohamia na anakohama. Tumuombee Ajibu apate nafasi ya kucheza huko Simba, vinginevyo ninavyoijua Simba hii ya sasa...anaweza kupakumbuka Yanga...Labda kwa vile ni maslahi

    ReplyDelete
  3. Ingependeza zaidi angepata timu nje ya nchi kwa kiwango chake huko anakoendaaa naona anaenda kuua kipaj chake... Wako wap akina Salambaaaa

    ReplyDelete
  4. muhimu ni masilahi kwa mpira wa kileo.Na isitoshe huyu Ajib ameanzia soka lake pale Simba B...tatizo nini akiamua kurejea kwenye klabu yake iliyomkuza?

    ReplyDelete
  5. Akifika simba aongee na kocha ambadilishe namba , kama ni kiungo atapata tabu sana kuingia kikosi cha kwanza

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic