MOJA ya timu zilizokuwa zikionekana kuwa na nafasi ya kupanda daraja hadi Ligi Kuu Bara ni Arusha United. Lakini hata kabla ya Ligi Daraja la Kwanza kufikia ukiongoni, imejitoa.
Arusha United ni ile iliyokuwa inaitwa JKT Oljoro, timu iliyokuwa inamilikiwa na jeshi na iliwahi kucheza Ligi Kuu Bara kwa ushindani mkubwa kabla ya kuporomoka na kuzama madaraja ya chini.
Ilionekana wazi wameshindwa kurudi katika kile kiwango kilichokuwa kimezoeleka na kuwapa sifa ya ubora kwa muda mrefu. Wakati wakiendelea kusuasua, uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo ukaamua kuichukua timu hiyo.
Hamu ya Gambo ilikuwa ni kuona Arusha wanakuwa na timu ya Ligi Kuu Bara. Hili ni jambo zuri kwa maana ya maendeleo lakini pia suala la burudani na muunganiko wa pamoja wa Wanaarusha kwa kuwa mchezo wa soka huunganisha watu.
Gambo alikuwa na wazo zuri ambalo lingekuwa na faida kubwa kwa mkoa wake lakini pia hata kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kwa maana ya kuwa na timu katika mikoa mbalimbali ya Tanzania badala ya sasa inaonekana mikoa kadhaa kuwa “imejilimbikizia” nafasi ya timu za ligi kuu.
TFF wala TPLB haziwezi kuwa na mkono wa kusambaza timu kwa mikoa, badala mikoa yenyewe kupambana kwa kuwa na timu bora zitakazopanda na kupanga mgawanyiko bora.
Huenda Arusha wangeweza, mwisho imeonekana kuwa na ugumu na walilalamika kwa muda mrefu kwamba katika mechi zao wamekuwa wakiambulia vitisho na vitendo vya kihuni, wakasambaza video wachezaji wao wakishambuliwa na hata waandishi wa habari kupigwa kisa eti walikuwa wakiripoti mechi ambazo zilikuwa zina vurugu.
Kwa kuwa vitendo hivyo vilikuwa vikifanywa na askari, TFF waliendelea kuwa na ukimya na inaonekana TPLB ndio walipaswa kusimama na kusema jambo. Wameendelea kuwa kimya hadi hapo Arusha United walipoamua kusimama na kutangaza kujitoa wakiona hakuna msaada wowote kwa wahusika.
Wakati wamejiondoa na TPLB ikiwa bado kimya na hakuna lolote angalau kwa wakubwa wa mpira wenyewe kwa maana ya TFF, juzi tumeona Arusha United ikirejea uwanjani na kucheza mechi dhidi ya Pamba ya Mwanza.
Baada ya mechi hiyo, Arusha United wameibuka na kusema timu yao walishaivunja kwa kuwapa wachezaji barua za kuvunja mikataba na wakamalizana nao. Kilichowashangaza ni kusikia Arusha United ikiwa uwanjani na wao hawaitambui.
Kinachowaliza ni kwamba, hawakuwahi kusaidiwa chochote wakati wakiwakilisha malalamiko yao lakini ajabu hata baada ya kuwa wamewasilisha barua ya kujiondoa na imepokelewa na wahusika, ajabu wameona timu ikicheza mechi dhidi ya Pamba na kupoteza, jambo linalofanya wahisi kumekuwa na njama za makusudi za kuwaangamiza na TPLB inafahamu lakini imeamua kuweka ndita katika masikio yake.
TPLB walikuwa kimya hadi Arusha United wakaamua kujitoa, sasa wako kimya hadi timu isiyotambuliwa na wamiliki imecheza tena ikiwa wao tayari wakiwa wameamua kuandika barua kuirudisha jeshini.
Kwa nini TPLB wameendelea kuwa kimya katika sakata kama hili linalowapaka matope na kuwafanya waonekane si watu makini, wasiojali au wenye dharau? Kwa nini wasisimame na kutoa ufafanuzi ili ijulikane mwenye madudu haya ni wao au Arusha United wenyewe na kama ni wale askari, vipi wasichukuliwe hatua?
Tunajua sote, kama timu fulani mashabiki wake walifanya vurugu, hatua za adhabu zinaiangukia timu husika. Au TPLB nao wanaogopa askari watukutu? Ukimya huu unazidi kutanua wigo wa udhaifu na haya yanaudhoofisha mpira nchini. Simameni mtueleze.
Imefika mahala hata TPLB na TFF wanaogopa wasiojulikana. Na huu ni udhaifu mkubwa sana kwenye soka la nchi hii. Kipindi TFF wanaingia madarakani kwa matamko yao tulidhani mambo ya ajabu kwenye soka la Tanzania yamekwisha, kumbe wapi bana wao wana dili na wala hela tu za shirikisho lkn madudu mengine bado yapo vile vile.
ReplyDeleteYaani hawa wamepwaya kwenye hii nafasi kuliko wakati wowote ule.