MZIGO ambao kwa sasa wanao Simba wataubeba kama wataamua wenyewe kufikiria kwamba wana makosa makubwa na kuamua kujipa hukumu.
Kilichowakwamisha kushindwa kupenya mchezo wa kwanza wa robo fainali wakiwa nyumbani ni papara na uhitaji wa kufunga mabao mengi hapo ndipo tatizo lilianzia.
Endapo wachezaji wangetulia na kucheza Kwa hesabu kali za ushindi na sio kutafuta mabao mengi mchezo ulikuwa mkononi mwao na wangepata ushindi mapema.
Licha ya kushindwa kushinda bado wanastahili pongezi Kwa kucheza na timu ngumu na kutoruhusu wao kufungwa tena na timu ambayo ina utulivu wa kutosha.
Kinachofuata ni mpango mpya kwa mwalimu wa Simba kujipanga upya akiwapa wachezaji morali na mbinu mpya za kutafuta matokeo inawezekana.
Uwezo walioonyesha wachezaji ni kiwango cha ushindani hawakuleta uzembe licha ya tabia ya baadhi ya wachezaji kukaba Kwa macho bado timu ilicheza Kwa ufanisi.
Papara ilikuwa kwa wachezaji wote na ndio maana walipata kadi za njano kuliko wapinzani na kucheza bila kuwa na utulivu licha ya kuwa nyumbani hali ambayo inapaswa ifanyiwe kazi.
Mbelgiji hana rekodi nzuri kwa mechi za ugenini Kwa uwezo alionao na aina ya wachezaji alionao anatakiwa aonyeshe ulimwengu kuwa kila kitu kinawezekana.
Kupoteza mechi tatu za ugenini na kupachikwa zigo la mabao ni mbaya na inapaswa ifutwe rekodi mbaya iandikwe rekodi mpya.
Rekodi inawekwa ili ivunjwe, muda huu macho ya Watanzania na maskio ya watanzania ni kuona timu inapenya hatua ya nusu fainali na uwezo upo mikononi mwa Simba wenyewe.
Mwaka 2003 tulianza Kwa kuangukia pua Kwa kuchapwa bao moja tena nyumbani na Zamaleki hivyo tukawa na bonge moja ya kazi ya kufanya.
Sasa kwenye mechi ya marudio tulikaza na tukatupia bao moja, haikuwa rahisi tulipambana kufa na kupona mpaka kuweza kupenya hatua inayofuata.
Mwisho wa siku tulipata ushindi kwenye hatua ya matuta rekodi mpya ikaandikwa ulimwengu ukaitambua Simba ni timu ya aina gani.
Nina imani na Simba kwani viongozi wengi ambao tulikuwa nao kipindi kile bado wapo ndani ya Simba wanajua walifanya nini.
Hivyo licha ya miaka kwenda mbinu za mpira kubadilika ila ile asili haipotei ule moyo wa kupambana na kutokata tamaa bado upo ndani ya Simba.
Hivyo Uongozi wa Simba ni muda wa kutulia na kutafakari mbinu kali na mpya zitakazowapa ushindi mkiwa ugenini kwenye hatua hii ya robo fainali.
Ule utani unaoendelea juu ya nahodha wa Simba John Bocco kukosa penalti hauna maana hasa kwa mchezaji mwenye uwezo na anaaminika na mwalimu.
Mashabiki msisahau kuwa hata nyota wakubwa kama Cristiano Ronaldo na fundi Lionel Messi huwa wanakosa penalti tena kwenye michuano mikubwa sasa Bocco ni nani?
Kikubwa ni kuwapa moyo wachezaji na kuachana na masuala ya penalti mara sijui ipo Kigoma ama Mwanza si sawa kulizungumzia hili muda wake umeisha.
Kwa Bocco hapaswi kulaumiwa ni sehemu ya mchezo na haikuwa lengo lake mapambano lazima yaendelee, apewe moyo aendelee kupambana na kuongoza kikosi cha Simba akiwa ni nahodha.
Tumeona kumekuwa na majibizano baada ya kubadilishiwa waamuzi wa mchezo ni suala la msingi ila lisipewe nafasi kubwa kuwavuruga msifanye maandalizi.
Mpira ni mchezo wa wazi haujifichi hivyo timu itakayojiaandaa ndiyo itaibuka na ushindi uwanjani na sio kucheza na mwamuzi hausiki katika kutafuta ushindi.
Waamuzi ni sehemu ya mchezo ila anayetafuta matokeo ni mchezaji mwenyewe uwanjani kinachotakiwa ni mipango na kuwa na nidhamu kwa wapinzani.
Wachezaji wekeni kando papara na hofu ambayo inawasumbua bebeni Bendera ya Taifa ili kuona ni namna gani mtarejesha furaha iliyopotea kwa mashabiki.
0 COMMENTS:
Post a Comment