April 8, 2019



MAMBO ni mengi ila muda tu unakimbia, hivyo na mipango yetu pia inapaswa itazamwe namna inavyopangwa na kuisimamia mpaka itimie ili kwenda sawa na muda.

Kwa sasa kwenye ulimwengu wa soka tayari ligi imerejea huku ushindani ukizidi kupamba moto hilo ni jambo la msingi kwa kila timu kutambua wajibu na majukumu yao.

Tatizo la ukata ambalo lipo limekuwa sugu lisiwe chanzo cha kufanya mechi kuwa hazieleweki yaani kitaalamu tunasema zikauzwa ili mshindi apatikane hili sio sawa.

Timu iliyojiandaa ndiyo inapaswa ipate matokeo na hakuna timu yenye nafasi ya kushinda michezo yote kwa sasabu mpira unachezwa uwanjani na sio mdomoni tunaamini wasimamizi watalitazama hili.

Imenibidi nizungumzie hilo kidogo kutokana na umuhimu wa maendeleo ya ligi yetu sasa narejea kwenye mada ya leo ndugu  msomaji ambayo nimekuaandalia inayohusu ligi ya vijana chini ya miaka 17.

Ligi hii zamani ilikuwa inajulikana kama Uhai Cup na sasa imefanyiwa maboresho makubwa imekuwa ni ligi ya Vijana Tanzania, hatua kubwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya jambo la muhimu kama hili.

Maboresho hayo yameanza kucheza na mpangilio wa mashindano namna yatakavyokwenda tofauti na msimu uliopita timu zilikuwa zinaweka kituo sehemu kisha mchakato wa kutafuta bingwa unaanza kufanyika.

Ila kwa sasa tumeona namna mpya ambayo imeanza kutumika kwenye mashindano haya ni kama kwenye Ligi Kuu Bara, jambo hili linastahili heko kwa TFF kwani limeimarisha mashindano na kuongeza ushindani.

Hali hii pia itafanya kila mmoja kujiaanda vema na kuepuka yale mazingira ya kubebana kutokana na uwepo wa ushindani wa kweli na kila mmoja kutambua maana halisi ya ushindani wa ligi ya vijana.

Naona namna vijana watakavyopata fursa ya kufika mikoa mbalimbali kufanya utalii wa ndani pamoja na kuyajua vema mazingira halisi ya Tanzania yetu.

Wapo vijana wengi wanapenda kusafiri na kujifunza ila wanakosa fursa huenda hii ikawa ni sehemu yao ya kujifunza.

Kujifunza kwao kunapaswa kuwe na matokeo chanya sio kwa kuwa unapata fursa ya kusafiri basi unakwenda kurukaruka, hapana nenda sehemu mpya ukaonyeshe ushindani wa kweli ili uache alama sehemu uliyokwenda.

Pia vijana ni wakati wenu kutambua kwamba mashindano hayo kwenu ni makubwa na muhimu kuwafikisha kule mnakofikiria kwenda msiyapuuzie onyesheni uwezo wa kweli na juhudi.

Nikukumbushe kwamba bingwa mtetezi wa kombe hili ni Mtibwa Sugar ambaye aliibuka kidedea mbele ya Stand United kwenye mchezo wa msimu uliopita na wakabeba kombe na kusepa nalo.

Hivyo ushindani ulioonekana msimu uliopita unatakiwa uwe mkubwa zaidi msimu huu ili kumpata mshindi wa kweli atakayejivunia kulipata kombe kwa kupambana kiukweli.

Mfumo wa kucheza nyumbani na ugenini kwa ligi ya vijana ni mzuri na unapendeza ila cha kuangalia hapa ni mipango makini kwa kila hatua ambayo itafanyika kwa sababu kuandaa mashindano ni jambo linalohitaji mipango ya kweli. 

Imani yangu ni kuona kwamba morali itakuwa kubwa kwa vijana kuonyesha uwezo wao hasa katika michezo yote ambayo watacheza kwa sasa tofauti na  msimu uliopita.

Pia mchakato mzima wa kumtafuta mshindi utazamwe kwa ukaribu na kila mmoja bila kusahau TFF ambao ni wahusika wakuu wasiyaache haya mashindano yakajiendesha kibubu italeta balaa.

Maboresho katika kila sekta yanapaswa yaboreshwe kutokana na utofauti wake hasa upade wa kuziandaa mechi pamoja na viwanja kuna ulazima wa kutazama namna bora itakayokuwa rafiki kwa kila timu kufikia malengo.

Tukumbuke kwamba kitu kilichonyuma ya mafanikio ya timu yetu ya Taifa Stars ni uwekezaji mzuri wa wachezaji vijana ambao walianza kukua katika vituo hivi na kuonekana kwamba wanaweza na hatimaye klabu zikawaona vijana zikawasajili.

Mwisho wa siku tunaona wachezaji wanakuwa na mwendelezo mzuri kila hatua haya ni matunda ya kujivunia tuna kazi ya kutengeneza watu wengi makini maalumu kwa ajili ya kupokea vijiti vya wenzao.

Pia hata matokeo ya Simba kufanya vizuri kwa kutinga hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa pia yanachangiwa na timu za vijana kwani huku ndiko ambapo wametokea wachezaji wengi wanaoipeperusha vema Bendera ya Tanzania sasa ili tupate timu nzuri, lazima wachezaji waandaliwe vizuri.

Matokeo makubwa ya wachezaji ambao watapatikana iwe ni nafasi ya kuwapa uhuru vijana kuonyesha kile walichonacho pia kunahitajika kituo maalumu kitakachowasaidia wao kulinda vipaji vyao na kutazamwa kwa ukaribu ili wasipotee.

Wengine ambao wamekuwa chipukizi mara nyingi wamekuwa wakishindwa kupata nafasi hali ambayo inaua uzoefu wao katika ulimwengu wa soka kwa sasa.

Kwa mtazamo wangu TFF  wameona mbali kwa kuanza kuboresha kwanza mashindano ya vijana hali ambayo itafanya Taifa liwe na hazina kubwa  kwenye uwanda wa vijana wachezaji na wenye vipaji isiwe mwisho wanaishia kupotelea kule ambako hatufikirii itakuwa ni anguko kwetu.

Kama tumeanzisha jambo la msingi basi tuwe na mipango endelevu ambayo itasaidia kukuza na kutunza hawa vijana ambao tutawapata watimize majukumu yao huku wakitambua kwamba Taifa linawategemea na kuwatengeneza kuwa vijana wapambanaji hapo baadaye.

Wachezaji wanatakiwa wajitambue kwa sasa dunia imekuwa ni kijiji kazi yao itaonekana na dunia nzima hali itakayowafanya waingie kwenye soko la ushindani mapema kutokana na wengi kufuatilia ligi za nyumbani

Leo hii hatua iliyopiga Tanzania kwenye sekta ya michezo sio sawa na jana kila mtu anaifuatilia kila hatua kila sehemu hali itakayofanya milango mingi ya mafanikio kwa vijana kufunguka haraka.

Vijana wafunguke macho waone kwamba milango ya mafanikio imefunguliwa kwao hasa kutokana na ukaribu wao na wale ambao wamefanikiwa nikimaanisha wale ambao wanawatazama kuweza kutambua uwezo wao.

Wakumbuke kwamba mashindano hayo yatarusha na kwenye TV hali itakayowapa fursa kutazamwa na wengi duniani moja kwa moja wanajiingiza sokoni wao wenywe bila kujua hivyo wanapaswa washtuke na wajitume kweli.


1 COMMENTS:

  1. Orodha iliyotoka katika kuchukua fomu za kugombea uongozi katika uchaguzi wa Yanga inaonekana kuna watu/waliochukua fomu baadhi yao hata uhalali wa uanachama/upenzi wao katika klabu ya Yanga una ulakini.... walakini....mfano sijui kama Dk Mshindo Msola na Fredrerick Mwakalebela ni Yanga. Pia kuna waliochukua fomu ambao walishashindwa kuongoza taasisi mbalimbali za serikali au michezo huko nyuma na kukumbwa na kashfa mbalimbali zikiwemo Ubadhirifu wa pesa, kutoa ama kupokea rushwa lakini nao pia wamejitokeza....wanachama wa Yanga wanatakiwa kuwa makini mno....kuchuja mamluki na wale ambao hawana maslahi na klabu na maendeleo ya mpira wa miguu nchini....Viongozi wanaotakiwa ni wale ambao ni waadilifu na walio na vision na ubunifu katika katika kuitoa klabu hapo ilipo na kuipeleka katika level ya juu ya maendeleo kulingana na ukubwa wa klabu ulivyo....na kuifanya ijitegemee...wanachama lazima watambue walipotoka wapi walipo na wapi wanataka kwenda....historia yao ya uanachama wa Yanga, historia ya mgombea mmoja mmoja lazima iainishwe na iwekwe wazi ushiriki wake huko nyuma katika kuisaidia klabu kimawazo, fedha na hali yoyote ile...ili wapimwe uwezo wao kabla ya kupewa madaraka!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic