April 7, 2019


UNAMKUMBUKA yule bodigadi matata wa staa mkubwa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Mwarabu Suleiman Mirundi almaarufu Mwarabu Fighter?

Basi leo amedondoka kwenye Ijumaa ShowBiz na kufunguka mambo kibao ikiwemo ishu ya kuondoka Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Diamond ambaye ni bosi wake wa zamani, twende pamoja;

Ijumaa ShowBiz: Mwarabu umebadilika sana baada ya kunyoa mandevu kiasi cha baadhi ya watu kushindwa kukutambua. Nini kimetokea?

Mwarabu: Sasa hivi nimebadilisha mwonekano. Wakati nikiwa na mandevu nilikuwa ninamlinda msanii (Diamond). Sasa hivi ninafanya kazi tofauti baada ya kuanzisha kampuni yangu ya ulinzi. Sasa ni mkurugenzi wa kampuni. Lazima kuwe na utofauti kati ya kipindi kile na sasa.

Ijumaa ShowBiz: Ilikuchukua muda gani kubadilika?

Mwarabu: Ni ishu ya muda mfupi tu pale mtu anapotaka kubadilika.

Ijumaa ShowBiz: Je, kumlinda Diamond ndiyo basi tena?

Mwarabu: Nina mwaka sasa tangu nimeacha kumlinda Diamond na kufungua kampuni yangu ya Securiy, Management and Guarding (SMG). Sasa hivi sifanyi kazi na msanii mmoja. Nafanya na mastaa wengi kama Uwoya (Irene), Hamisa (Mobeto), Nabii Shillah na watu binafsi.

Staa yeyote akinihitaji nipo tayari. Hata kama ni Diamond akihitaji ulinzi nipo tayari ilimradi tu kuwe na mkataba wa siku moja au hata wiki. Staa au mtu yeyote akiwa na mtoko wake wa kwenda sehemu fulani, hakuna shida, atapata ulinzi kutoka kwangu kwa makubaliano tutakayokuwa tuyafikia. Lakini ikifika mwakani nitaacha kulinda mimi kama mimi badala yake kazi hiyo itafanywa na vijana wangu ambao wapo kwenye mafunzo chini yangu.

Ijumaa ShowBiz: Uhusiano wako na WCB kwa sasa ukoje?

Mwarabu: Naongea sana na watu wa Wasafi kama Rayvanny, Lavalava hata meneja wao, Babu Tale. Unajua Wasafi chini ya Diamond ndiyo wamenifikisha hapa nilipo. Wanafurahia sana mimi kuondoka Wasafi kwa sababu ndiyo imekuwa fursa ya kuanzisha taasisi yangu maarufu kwa jina la Mwarabu Security. Wasafi wanaona hiki ninachofanya wanajivunia na nitaendelea kufanya nao kazi, bila wao hasa Diamond nisingejulikana hivyo wana heshima zangu zote. Nipo nao vizuri sana.

Ijumaa ShowBiz: Kuna umuhimu wowote wa msanii kuwa na bodigadi?

Mwarabu: Msanii kuwa na bodigadi ni kitu cha muhimu sana. Msanii mkubwa akiwa na mashabiki wengi huwa upendo unaongezeka dhidi yake.

Katika hali kama hiyo, shabiki anaweza akamrukia na kumuumiza, siyo kwa ubaya, lakini ni kwa mapenzi tu. Msanii lazima awe na bodigadi ili kuangalia mazingira hatarishi kutokana na upendo kuzidi hivyo siyo ishu ya kujionesha, ni huduma anayohitaji msanii kwa usalama wake.

Kwa mfano kuna mahali atataka kupiga picha na mashabiki wake, sasa hawawezi kwenda tu wote, lazima wapangwe mmojammoja na kazi hiyo haiwezi kufanywa na msanii mwenyewe, badala yake itafanywa na bodigadi wake.

Ijumaa ShowBiz: Anamchukuliaje msanii mkubwa ambaye hana bodigadi?

Mwarabu: Tanzania tulikuwa hatujafikia huko, lakini kwa sasa naamini muda umefika kwa msanii kuona umuhimu wa kuwa na bodigadi.

Ijumaa ShowBiz: Ukikutana na Rais John Pombe Magufuli, utamwambia nini?

Mwarabu: Nitampongeza kwa hatua aliyofikia. Nitamwambia ameifanya Tanzania kuwa juu. Ametengeneza ajira kutokana na miradi mbalimbali inayoendelea nchini kama barabara za juu, ndege na nyinginezo. Kiukweli Rais Magufuli atabaki kuwa juu na mimi ninamkaribisha Mwarabu Security tupo tayari kumpa huduma ya mazoezi na ulinzi bure kama sehemu ya kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Ijumaa ShowBiz: Mtu akihitaji huduma za Mwarabu Security anafanyaje?

Mwarabu: Ofisi za Mwarabu Security zipo pale Dar Free Market na mazoezi au mafunzo ya ubodigadi tunafanyia pale Colosseum Hotel, Oysterbay.

Ijumaa ShowBiz: Unawaambia nini mashabiki wako?

Mwarabu: Mimi napenda kutumia usafiri wa kawaida wa bodaboda, Bajaj au daladala, huko ninakutana na watu wengi na wananipenda sana. Ninachowaomba wazidi kuwa na upendo wa dhati.

Ijumaa ShowBiz: Hivi mtu akikuchokoza huwa unachukua hatua gani?

Mwarabu: Zamani nilikuwa napigana na kupiga sana watu nikichokozwa, lakini baadaye nilikuwa nikikaa najuta kwa nini nimempiga mtu. Unajua kazi hii inahitaji sana busara na hekima. Nashukuru siku hizi nafanya mazoezi na kukutana na watu waelewa hivyo mambo ya uchokozi hakuna na hata mtu akinichokoza siwezi kumpiga kwani nina busara. Kazi yangu ni kuhakikisha kunakuwa na amani na siyo uvunjifu wa amani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic